Na Mwandishi Wetu
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhani Kailima, ameutaka uongozi wa Jeshi la Magereza nchini, kutekeleza kwa wakati maelekezo yanayotolewa. Pia amelitaka jeshi hilo litimize wajibu walionao pamoja na kujitathmini juu ya ujenzi wa miradi mbalimbali.
Kailima aliyasema hayo jijini Moshi, mkoani Kilimanjaro jana baada ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda kipya cha bidhaa za ngozi cha Karanga (Karanga Leather Industries Company Limited (KLICL).
Mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo manne ambayo ni Cutting and stitching building, Lasting building, Warehouse pamoja na Power house. Ujenzi wa majengo hayo ulianza rasmi Oktoba 28,2019 ukitarajiwa kukamilika Februari 2, mwaka huu.
Katika ziara hiyo, Kailima aliutaka uongozi wa jeshi hilo kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana, Wenye Ulemavu, Andrew Massawe baada ya kukagua ujenzi huo.
“Nataka mtoa taarifa kwa wakati na usahihi katika hatua zote za ujenzi, taarifa ni muhimu kwa utekelezaji wa kazi ambazo zinafanyika kwenye mradi,” alisisitiza Kailima.
Awali Mkandarasi wa mradi kutoka Prisons Corporation Sole, Mhandisi SP Julius Sukambi, alitoa taarifa inayohusu maendeleo ya mradi huo akifafanua kuwa, ujenzi unafanyika usiku, mchana.
Alisema nguvu kazi ya wafungwa 170 hushiriki ujenzi huo kuanzia asubuhi hadi jioni, wafungwa 50 huingia jioni hadi asubuhi.
Pia jeshi hilo limeongeza nguvu kazi ya wataalam wakiwemo Wahandisi wanne waliopo eneo la mradi, kuongeza wasaidizi wa Wahandisi (technicians) na kufikia wanane.
“Sambamba na hilo, pia tumeongeza mafunzi wa fani mbalimbali, kwa siku tuna mafunzi wasiopungua 100, jitihada za kuongeza watendaji zimefanyika ili kukamilisha ujenzi kwa wakati.
“Kazi kubwa iliyokuwa inatukabili ya ujenzi wa msingi imekamilika kwa asilimia 95 hivyo tunaamini kazi zilizobaki zitakamilika kwa wakati,” alifafanua SP Sukambi.
Alisema tayari njia ya kuingia eneo la mradi imetengenezwa, mabati ya kuezekea jengo la kupokea mitambo yamepatikana ndani ya siku saba badaya ya 14, jengo limeanza kuezekwa.
Akizungumzia changamoto, alisema ni upatikanaji wa vifaa hasa mvua zinaponyesha vinavyotokana na madini ya ujenzi kama mchanga, mawe, kokoto ambavyo havipatikani kwa urahisi kutokana na magari kushindwa kuingia katika machimbo.
“Kazi zinaendelea kufanyika kwa ufanisi na ubora zaidi, mashine, mitambo ya kiwanda tayari imewasiri Bandari ya Dar es Salaam vikiwa katika ukaguzi kabla ya kuwasirishwa kiwandani.
“Mradi huu kwa asilimia 100 unasimamiwa na wazawa, Timu ya Mshauri mwekezaji wa mradi inashirikisha TIRDO, Chuo cha Kikuu cha Dar es Salaam kitendo cha BICO pamoja na Chuo Kikuu cha Ardhi kitengo cha ABECC.
Januari 15, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alitembelea mradi huo.
Katika ziara hiyo, Mhagama alisema Serikali haijaridhika na kasi ya ujenzi wa kiwanda hicho kilichopo kwenye Gereza la Karanga, kumtaka Mkandarasi akamilishe kazi kabla ya Februari 2, 2020.
“Hakuna sababu ya mradi huu unaotekelezwa kwa ubia kati ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Gereza la Karanga kutokamilika kwa wakati.
“Fedha zote zilizohitajika katika hatua muhimu za mradi huo zimekwishatolewa, mradi huu ni miongoni mwa miradi muhimu ya kimkakati iliyopangwa kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.
“Mkandarasi hana budi kuzingatia masharti ya mkataba uliowekwa ili kuhakikisha kiwanda kinakamilika kwa wakati ili kiweze kuleta tija iliyokusudiwa,” alisisitiza Mhagama.
Aliuagiza uongozi wa jeshi hilo kuhakikisha kunakuwepo vifaa, vitendea kazi na wataalamu wa kutosha katika maeneo yote ya ujenzi ili uweze kukamilika kwa wakati.
No comments:
Post a Comment