TAFAKURI JADIDI: KUILEWA KONGO- KINSHASA..., NI LAZIMA UUMIZE KICHWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 31 January 2025

TAFAKURI JADIDI: KUILEWA KONGO- KINSHASA..., NI LAZIMA UUMIZE KICHWA

- Kabila ( Baba) alimwandaa Mwanawe Joseph tangu Kunduchi Mtongani.

Laurent Kabila ( Pichani ya kwanza) aliingia Mashariki ya Kongo na karata mbili; ya kwake na ya mwanawe.  Alijaribu kufanya hivyo miaka ya 60 akisaidiwa na mwanamapinduzi Che- Guevara. Alishindwa. 

Kwanini? 

Jibu lake ni simulizi nyingine.

Vinginevyo, mradi mkubwa wa ' Kabila dynasty' ulikuwa ni kujenga ' Democratic Republic of Congo- DRC'. 

Ieleweke hapa, kuwa inapohusu Kongo- Kinshasa,  tunazungumzia himaya tatu zenye kugombea kutoa mtawala: 

BaAlunda, BaAluba na BaHima. Mashariki ya Congo wapo WaAluba. BaHima pia wapo,  bila kusahahau himaya nyingine ndogo ya Bayeke.

Banyamulenge wale walitokea kwenye BaHima. Kagame na Museveni wana asili ya BaHima. Kumbuka watu wa aina ya Sultan Makenge, Bosco Ntaganda na Roland Nkunda. 

Tanzania tulipokwenda DRC na vikosi vyetu kupambana na M23 yumkini ni kwa nadharia pia ya kuwasaidia walio na maslahi kwetu. Kihistoria Wa- BaAluba ni wenzetu. 

Na pale Pierre Nkurunziza alipoandamwa na wenye asili ya Himaya ya BaHima ilimhitaji mwenye kutaka kuelewa  undani wake, atafakari kwa kina. 

Suala la Kongo- Kinshasa  ni gumu lakini linafafanulika. WaAlunda wenye Kinshasa yao wanaongea Kilingala na wanakizungumza Kifaransa cha wakoloni wao. 

Kumbuka, Kabila baba alipouawa, watu wa Kinshasa hawakumpokea vizuri mwanawe,  Joseph Kabila. Mitaani Kinshasa walisema, kuwa Joseph  hajui kuongea Kifaransa. Akawashangaza siku ya kuapishwa kwake alivyozungumza Kifaransa. 

Siri yake?

Laurent Kabila alihakikisha anamwandaa mwanawe  Joseph siku itakapofika kwenda tena Kongo- Kinshasa,  na hususan kupitia Mashariki ya Kongo. 

Ni kwenye  kukamilisha mpango wa tangu enzi za baada ya kuuawa Lumumba. Mpango wa kuirudisha Kongo tena, na mara ya pili ni kwa kuijenga inayoitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo. Kwamba Kongo mpya haitakuwa ya WaAluba tu, ni ya wote. 

Ikumbukwe, Laurent Kabila alikuwa  mfuasi wa Lumumba. Alikuwa Mjamaa ambaye kukimbilia kwake Tanzania baada ya Lumumba kuuawa mwaka 1961, ilikuwa ni jambo lililotarajiwa. 

Joseph Kabila amezaliwa kwenye ardhi ya Tanzania. Ni kizazi cha tatu cha Kongo ya Lumumba. Amekulia Tanzania pia, lakini, Laurent Kabila alikuwa akimwandaa mwanawe kwa ' Wimbi la pili' la Mapinduzi ya Kongo. 

Joseph Kabila mitaani na shuleni alikopitia Tanzania, amekuwa akiongea Kiswahili kama Waswahili wengine, lakini, kwenye familia ya Laurent Kabila,  nyumbani pale Kunduchi Mtongani, kimkakati, kiliongewa Kifaransa.

Ndio  maana watu wa Kinshasa walishangazwa mwaka ule wa 2001 kumwona Joseph aliyezaliwa na kukulia Tanzania, kwamba siku ya kuapishwa aliongea Kifaransa.

Laurent Kabila kwenye kumwandaa  mwanawe Joseph Kabila alihakikisha anapitia mafunzo ya kijeshi pia. Ukiacha JKT ya Tanzania ambayo ilikuwa ni kwa mujibu wa sheria, wakati Laurent Kabila na wenzake wakijiandaa na wimbi la pili la kuingia Kongo, Joseph Kabila alipata mafunzo zaidi ya kijeshi. Baba yake alimpeleka mwanawe mpaka Uchina ili kupata mafunzo ya kijeshi.

Itaendelea.

Maggid Mjengwa

No comments:

Post a Comment