|
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Gelasius Byakanwa mara baada ya kuwasili mkoani Mtwara kufuatilia hali ya malipo ya wakulima wa korosho leo tarehe 13 Disemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal). |
Na Mathias Canal, Mtwara
ZAO la korosho katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 limeingiza zaidi ya Bilioni 406.3 kupitia minada sita ambayo imekwishafanyika kwa nyakati tofauti.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 13 Disemba 2019 wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Gelasius Byakanwa mara baada ya kuwasili mkoani Mtwara kufuatilia hali ya malipo ya wakulima wa korosho.
Waziri Hasunga amesema kuwa kiasi hicho kimepatikana kabla ya minada itakayofanyika kuanzia tarehe 13 Disemba 2019 na kuendelea. Amesema kuwa mpaka sasa tayari Tani 163,000 zimekusanywa huku Tani 151,554 zikiwa zimeuzwa kati ya korosho hizo zilizokusanywa.
Mhe Hasunga amesema kuwa muendelezo wa minada ya korosho inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini inatoa taswira chanya kwa wakulima hivyo kuwa na uhakika wa kipato chao kutokana na minada hiyo kuendelea kutoa matokeo chanya hususani kuongezeka kwa bei.
Alisema kuwa Korosho ni zao muhimu na ndilo linaongoza kwa kuiingizia nchi Pato kubwa la kigeni likifuatiwa na zao la Tumbaku.
“Bado hatujamaliza kukusanya korosho, hatujamaliza kuuza korosho na shunguli zingine za serikali kusimamia zao la kilimo ikiwa inaendelea lakini mpaka sasa tumeshakusanya zaidi ya Bilioni 406 hivyo hayo ni maendeleo mazuri kabisa,” Alikaririwa Mhe Hasunga
Ili kuboresha zaidi sekta ya kilimo hususani zao la Korosho Waziri huyo wa Kilimo Mhe Hasunga amesema kuwa serikali imekusudia kusimamia vyema vyama vya ushirika ikiwa ni pamoja na kuboresha sheria yake ili kuboresha weledi wa kiutendaji kwa wananchi.
“Tumeamua kuchukua hatua za dhati kabisa kama serikali za kuhakikisha Ushirika unasimamiwa ipasavyo, Ushirika unaonekana kuimarika zaidi Ruvuma, Lindi na Mtwara kuliko maendeo ya Pamba na Kahawa. Hivyo tuna kila sababu ya kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kuboresha ushirika kote nchini,” Alisema Mhe Hasunga
Amesema kuwa Vyama vingi vya ushirika havina uwezo wa kuweka kumbukumbu sahihi za makusanyo, madai ya wananchi na mauzo ya korosho, baadhi ya viongozi kutokuwa waaminifu na kuwa wabadhilifu wa mali za wananchi.
Waziri Hasunga amesema kuwa tayari wizara ya kilimo imeanza kuchukua hatua za kisheria kwa viongozi wote wa vyama vya ushirika ambao wamepokonya mali za wananchi.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga leo tarehe 13 Disemba 2019 ameanza ziara ya kikazi mkoani Mtwara akiwa ametokea mkoani Lindi na Pwani ambapo pamoja na mambo mengine atakagua hali ya uuzaji wa korosho msimu wa 2019/2020, kukagua hatua zilizofikiwa za malipo ya wakulima wa korosho zilizonunuliwa na serikali msimu wa mwaka 2018/2019 na kukagua skimu za umwagiliaji.
No comments:
Post a Comment