Mwenyekiti wa Chama cha Wasindikaji wa Alizeti mkoa wa Singida (SISUPA), Juma Mene akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha TanTrade na SISUPA kujadili jinsi ya kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti. (Katikati) ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi, Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade Edwin Rutageruka, na Afisa Biashara wa Mkoa wa Singida, Daniel Munyi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TAN TRADE), Edwin Rutageruka akiongoza majadiliano ya wadau wa zao la alizeti mkoani Singida jana, kwenye mkutano uliowakutanisha TanTrade na SISUPA kujadili jinsi ya kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti.
Viongozi wa SISUPA, Tantrade na wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani wa zao la alizeti, wakifuatilia mada mbalimbali kwenye mkutano uliowakutanisha TanTrade na SISUPA kujadili jinsi ya kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti mkoani Singida juzi.
Kaimu Meneja wa Masoko ya Ndani kutoka Tantrade, Gertrude Ng’weshemi, akitoa mada mbele ya wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani wa zao la alizeti mkoani Singida jana. Mkutano huo uliwakutanisha TanTrade na SISUPA kujadili jinsi ya kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti.
Majadiliano yakiendelea.
Farida Muro kutoka Kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha Mt Meru mkoani Singida akizungumza kwenye mkutano huo.
Rehema Mbula kutoka Ilongelo mkoani Singida akizungumza kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa Simsopa, Singida MC, Timothy Kinara akichangia kwenye majadiliano ya namna ya kuongeza tija kwenye uzalishaji wa zao la alizeti mkoani Singida.
Baadhi ya wadau wakifuatilia mkutano huo.
Mmoja wa wajumbe akichangia.
Na Mwandishi Wetu
WASINDIKAJI wa viwanda vya kuzalisha mafuta ya alizeti nchini wameomba serikali kufanyia marekebisho msululu wa tozo mbalimbali, ikiwemo VAT zilizopo kwenye mnyororo wa thamani eneo hilo, ili kuongeza tija, kutokana na tozo hizo kuonekana kikwazo kinachopelekea kufifisha ustawi wa viwanda hivyo na kutoa fursa kwa viwanda vya nje kuchukua nafasi kubwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TANTRADE), Edwin Rutageruka, akitoa taarifa fupi ya mambo yaliyojadiliwa kupitia mkutano wa Chama cha Wasindikaji wa Alizeti Singida (SISUPA) na Tantrade mkoani hapa jana, kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi kuzungumza, alisema kuna haja ya kuongeza tija na uzalishaji wa zao la alizeti kutokana na ukweli kwamba zao hilo kama malighafi bado halitoshelezi.
Akizungumza kwa niaba ya wadau hao, Rutageruka alisema ushuru mkubwa unaotozwa na halmashauri, sanjari na tozo za VAT kwenye bidhaa zitokanazo na zao la alizeti vimekuwa ni miongoni mwa sababu zinazoshusha kiwango cha uzalishaji, kutokana na wasindikaji na wakulima walio wengi kuvunjika moyo na kushindwa kuzalisha kwa tija kukidhi mahitaji ya ndani, sambamba na kukabiliana na ushindani toka nje.
Alisema kulingana na majadiliano ya wadau, sababu nyingine zinazopelekea kufifisha ustawi wa zao la alizeti ni uchache wa wataalamu na maafisa ugani, sambamba na zao hilo kutokuwa na bei elekezi, ikilinganishwa na mazao mengine. Pia uhaba wa maghala ya kuhifadhia malighafi hiyo na teknolojia ndogo kuwezesha kuzalisha bidhaa yenye ubora stahiki kwa ushindani wa soko vimetajwa kama sababu.
Mkurugenzi huyo wa Tantrade, alisema changamoto nyingine zinazokwamisha tija ya zao hilo ni kutopimwa kwa udongo wa ardhi inayozalisha alizeti ndani ya mkoa wa Singida, huku suala la uaminifu baina ya mkulima na mnunuzi wanapotekeleza kilimo cha mkataba limekuwa ni pasua kichwa. Na kwenye eneo hilo mikataba mingi imekuwa ikiandikwa kwa lugha ya Kiingereza.
Akijibu baadhi ya hoja hizo, Dkt. Nchimbi huku akionyesha kufarijika na kufurahishwa na ujio wa Tantrade, na hatimaye mkutano huo uliolenga kuongeza uzalishaji na tija ya zao la alizeti ndani ya Mkoa wa Singida, alisema suala la VAT ni la kitaifa zaidi, lakini kuhusu tozo kwenye halmashauri litashughulikiwa. Hata hivyo alisema ushuru wa mashudu ulishaondolewa lakini anasikia kuna baadhi ya halmashauri bado zinatoza.
Kuhusu zao hilo mpaka sasa kukosa bei elekezi, Dkt. Nchimbi alisema kabla ya kupanga bei dira inapaswa kwanza kuundwa chombo cha kuratibu mwenendo mzima wa zao hilo. Aidha kuhusu matumizi ya lugha ya kigeni kwenye mikataba alisema mtu yeyote asilazimishwe kutumia lugha asiyoielewa.
“Tantrade tusaidieni kuhakikisha mafuta yetu ya alizeti yanakwenda kuchangia kwenye pato la nchi, kinachounganisha wana-Singida ni alizeti,” alisema Nchimbi.
Aidha, katika hatua nyingine, kupitia mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu ya ‘Badili Gia tumia mbegu bora za alizeti zenye tija’ Nchimbi aliwataka wadau wote wa alizeti ndani ya mkoa wa Singida kufahamu kuwa mkoa huo ulikabidhiwa fedha na SADC Dola elfu 20 kwa ajili ya kuinua zao la alizeti, wakati wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Chakula na Lishe, yaliyofanyika mkoani hapa.
“SADC walitoa fedha hizo, ni jukumu lenu kujua fedha zenu hizo zimekwenda wapi, pia Tantrade fuatilieni,” alisema Nchimbi.
No comments:
Post a Comment