Na Prisca Ulomi, Mwanza
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb), amefungua mafunzo kwa mafundi simu za mkononi wa Kanda ya Ziwa wa kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.
Kamwelwe amefungua mafunzo hayo yatakayofanyika kwa mafundi simu za mkononi wa Kanda ya Ziwa wapatao 200 ambayo yamepangwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu kwenye Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam, Kampasi ya Mwanza.
Kamwelwe amewaeleza mafundi simu za mkononi kuwa wateja watakuwa hawana wasiwasi na wao kwa kuwa watakuwa wanaleta simu zao kutengenezwa kwa mafundi simu za mkononi ambao wamepata mafunzo yaliyotolewa na Serikali kupitia wataalamu wa DIT chini ya uratibu wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Tanzania (TCRA) ambao wamedhamini na kufanikisha uendeshaji na kugharamia mafunzo hayo kwa Kanda ya Ziwa.
“Ninyi ni mafundi ambao mtapata mafunzo na mtapatiwa miongozo, leseni na mmesajiliwa, mteja anapoleta simu yake kwako anakuwa hana wasiwasi kwa wizi na kwa wale ambao wanaiba simu na kuleta kwenu, nalo mtakuwa mmelimaliza kwa kuwa mtawabaini na kuwashughulikia kwa kushirikiana na mamlaka husika,” amesema Kamwelwe.
Kamwelwe amewataka mafundi simu kujiunga pamoja ili waweze kupewa leseni na Serikali kutoka TCRA ili waweze kuitumia kununua vifaa vinavyohitajika kutengenezea simu ya mkononi na vifaa vingine vya TEHAMA ambavyo vitakuwa vimeharibika na vinahitaji kufanyiwa matengenezo ambapo amewaeleza mafundi hao kuwa kama hawana mtaji wamuone.
Pia, ameongeza kuwa Serikali kupitia TCRA imeamua kuwajengea uwezo mafundi simu za mkononi ili kuweza kuwahudumia watanzania takribani milioni 34 wanaomiliki simu za mkononi na Serikali haiku tayari kuleta mafundi simu kutoka nje ya Taanzania ili kupitia mafunzo tuendelee kutoa ajira kwa vijana na tutaendelea kuwaweka kwenye vikundi maalumu ili muweze kusaidiwa kisheria kama ilivyo leo kwa kuwapatia mafunzo.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Kamwelwe, Katibu Mkuu wa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Dkt. Maria Sasabo amewaeleza mafundi simu za mkononi kuwa nae ni fundi kwa kuwa alisoma DIT akawa fundi mchundo ambapo amewahimiza mafundi hao na kuwatia moyo kuwa washirikiane vema na mafundi simu wa kike ambao wanapatiwa mafunzo na kuwaomba wakufunzi kuhakikisha kuwa wanawasaidia mafundi simu wa kike kushiriki kikamilifu na kuhitimu mafunzo hayo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amewaeleza mafundi hao kuwa wayape kipaumbele mafunzo hayo kwa kuwa masuala mbali mbali yatafundishwa ikiwemo ujasiriamali ili kurasimisha mafunzo na ufundi kwa mafundi simu ili kuchochea ukuaji na ongezeko la la watumiaji wa vifaa vya huduma za mawasiliano na simu za mkononi.
Kilaba ameongeza kuwa usalama na ubora wa vifaa vya mawasiliano ni jukumu letu sote ambapo mafundi simu ni sehemu ya utekelezaji na mafunzo haya yataendelea kutolewa na TCRA kwenye ofisi zake ikiwemo kwenye ofisi ya Kanda ya Kati ambapo amfunzo yatafanyika Dodoma, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Kaskazini (Arusha) na Kanda ya Zanzibar (Unguja).
Mkuu wa Mafunzo wa DIT, kampasi ya Mwanza, Dkt. Albert Mmari amesema kuwa DIT ilitoa mafunzo kama hayo kwa mafundi simu za mkononi wa Dar es Salaam katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita na sasa wamejiandaa kutoa mafunzo hayo Mwanza kwa mafundi hao wa Kanda ya Ziwa.
Mmari amewaomba mafundi hao kuhudhuria mafunzo hayo na washirikiane na TCRA kuwaelemisha wadau na wateja kupeleka simu zao za mkononi kwa mafundi simu waliopata mafunzo ili kulinda usalama na ubora wa simu zao na vifaa vingine vya TEHAMA.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Mafundi Simu za Mkononi wa Kanda ya Ziwa, Magua Manyanda amemshukuru Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa TCRA, Mhandisi Francis Mihayo kwa kuwakutanisha mafundi hao, kuwaweka pamoja, kusimamia uanzishwaji wa umoja wao na kuwaandalia mafunzo ili waweze kushirikiana na Serikali na mamlaka nyingine kudhibiti uhalifu unaosababishwa na simu za mkononi ambapo mafundi simu wako tayari kushirikiana na TCRA na Jeshi la Polisi kudhibiti wezi wa simu za mkononi na kupitia umoja huo, kwa fundi simu atakayebainika kushirikiana na wahalifu na genge la wezi ataondolewa mara moja kwenye umoja huo.
Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment