WAZIRI DK MWAKYEMBE AMEWAHIMIZA VIJANA KUSHIRIKI KATIKA UCHUMI WA TANZANIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 11 November 2019

WAZIRI DK MWAKYEMBE AMEWAHIMIZA VIJANA KUSHIRIKI KATIKA UCHUMI WA TANZANIA

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza (wa tatu kushoto) akisisitiza jambo walipokutana na Mshindi wa dunia wa Ulimbwende wa Mitindo Winifrida Brayson (wa pili kushoto) leo Bungeni jijini Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe na Mkurugenzi wa Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi (KISUVITA) Habib Mrope (wa kwanza kulia).

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza kushoto) akiongea Mshindi wa dunia wa Ulimbwende wa Mitindo Winifrida Brayson (wa pili kushoto) leo Bungeni jijini Dodoma.
Na Eleuteri Mangi, Dodoma
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewahimiza vijana kushiriki katika tasnia ya ulimbwende ili waweze kushiriki katika kujenga uchumi wa nchi kupitia sekta ya sanaa. 
Waziri Dkt. Mwakyembe amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akimpongeza Mshindi wa dunia wa Ulimbwende wa Mitindo kwa watu wasiosikia (viziwi) Winifrida Brayson (Miss Deaf Top Fashion Model 2019) kwa mafanikio aliyoyapa kwenye mashindano hayo yaliyofanyikia kuanzia Julai 7 hadi 15 mwaka huu huko mjini St.Petersburg nchini Urusi.
“Mashindano haya lishafanyika mara tatu, kwa mara ya kwanza yalifanyika nchini Italia, Marekani na kwa mara ya tatu yamefanyika nchini Urusi, sisi tumeshiriki kwa mara ya kwanza ambapo tulimpeleka binti yetu Winifrida Brayson kushiriki, bahati nzuri amefika, tumeshinda katika mashindano hayo akaibuka ndio Miss World top fashion model nchini Urusi na ndio maana tukaona kwa mafanikio hayo makubwa aje Bungeni kutusalimia na tumpongeze.”
Waziri Dk. Mwakyembe amesisitiza kuwa Ndio tupo kwenye tasnia ya Ulimbwende ambayo ni mihimu kwa vijana wetu ambapo amesema Winfrida ni mtaalamu katika masuala ya fasheni na mitindo ambapo amemhimiza aendelee katika eneo hilo ili aweze kuzalisha vijana wengi ambao wanaweza kuwakilisha nchi yetu kimataifa na kushiriki katika uchumi wa nchi yetu katika upande wa fasheni.
Dk. Mwakyembe ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Mali Asili na Utalii iliratibu na kufanikisha safari ya Winifrida wakati wa mashindano hayo
Aidha, Waziri Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa Serikali ipo karibu na inandelea kusimamia sekta ya sanaa ili kuipeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano mbalimbali duniani.
“Wizara imefurahishwa na ushindi huo ukizingatia ni mara ya kwanza wanashiriki mashindano ya kimataifa ya aina hiyo na amempongeza washiriki huyo kwa juhudi alizoonesha ubunifu na hatimaye kurudi na ushindi nyumbani.” Waziri Dkt. Mwakyembe.
Kwa upande wake Mshindi dunia wa Ulimbwende wa Mitindo Winifrida Brayson ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kumuwezesha kufanikiwa kushiriki mashindano hayo na kusisitiza vijana wapate elimu ambayo ndio msingi wa maisha yao.
Aidha, Mlimbwende huyo akiwa nchini Urusi alishiriki na kufanikiwa kuwa miongoni mwa washindi 10 bora katika mashindano ya kimataifa kwa watu wasiosikia yaliyofanyika Julai mwaka huu na pia amekuwa mshindi wa Tamasha la nne la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalofanyika jijini Dar es Salaam mwaka huu.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi (KISUVITA) Habib Mrope amesema kuwa taasisi yao imeweka maleno ya kufanya vizuri ndani na nje ya nchi katika mashindano mbalimbali ambapo kwa mwaka 2020 mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika nchini Marekani.

No comments:

Post a Comment