Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb). |
Na Peter Haule, Dodoma
SERIKALI imefanikiwa kuwarejeshea wafanyabiashara na wawekezaji
Kodi ya Ongezeko la Thamani-VAT baada ya uhakiki wa madai yao kwa lengo la
kuimarisha kipato cha mtu mmoja mmoja na uwekezaji nchini.
Hayo yamesemwa bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa
Viti maalum, Mhe. Khadija Nassir Ali, aliyetaka kujua namna Serikali
ilivyojipanga kurejesha Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa wawekezaji ili
kuimarisha uwekezaji.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, Serikali imelipa zaidi ya asilimia 90
ya VAT kwa watu waliokuwa wakidai Serikali baada ya kufanyika kwa uhakiki wa
madai hayo, uhakiki unaendelea kwa asilimia kumi iliyobaki ili kujiridhisha
kabla ya kufanya malipo.
“Tulikua na changamoto kubwa ya udanganyifu kwenye eneo la
urejeshwaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani, hivyo Serikali ilianza mkakati wa
kujiridhisha na kila muamala unaoletwa ili kuweza kuirejesha kwa wazalishaji,
wanunuzi pamoja na viwanda vilivyopo nchini”, alieleza Dkt. Kijaji.
Aidha, akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Busega, Mhe. Dkt.
Raphael Chegeni, aliyetaka kujua maana ya dhana ya ukuaji wa uchumi kwa
kuoanisha na Maisha ya wananchi, Dkt. Kijaji alisema kuwa dhana hiyo
inatafsiriwa kwa kuangalia upatikanaji, ubora na gharama ya huduma za jamii
zinazotolewa na Serikali.
Alisema baadhi ya huduma hizo ni pamoja na elimu, afya, maji,
umeme na miundombinu ya usafiri na usafirishaji inayosaidia kupunguza gharama
za usafirishaji wa bidhaa na na matengenezo ya vyombo vya usafiri.
Dhana nyingine ya kutafsiri ukuaji wa uchumi na maisha ya
wananchi ni ushiriki wa wananchi wenyewe katika shughuli za kiuchumi hivyo
ukuaji wa uchumi ni matokeo ya ushiriki wa wananchi katika uzalishaji mali na
huduma.
Alisema kuwa wananchi wanaoshiriki katika shughuli za uchumi
wananufaika kwa tafsiri ya dhana ya ukuaji wa uchumi kupitia huduma za kijamii
zinazotolewa na Serikali pamoja na matokeo ya shughuli zinazofanywa na
mwananchi.
Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kufanya jitihada za kuweka
mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara ili kila mtanzania aweze kutumia
kikamilifu fursa zilizopo katika uzalishaji na huduma.
Naibu Waziri Dkt. Kijaji alisema kuwa uwekezaji katika viwanda
utaongeza ajira na uzalishaji katika Sekta ya kilimo kwa kuwa Sekta hiyo
inaajiri idadi kubwa ya watu nchini.
No comments:
Post a Comment