WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU WASITENGWE-MAMA MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 11 November 2019

WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU WASITENGWE-MAMA MAJALIWA

Mlezi wa Kikundi cha Wake wa Viongozi cha New Millenium Women Group, Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa  (kulia), Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako (wa pili kulia) na  Mwenyekiti wa kikundi hicho, Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu , Mama Tunu Pinda (wa tatu kulia) wakiwapa  chakula watoto wa kituo cha Watoto wenye ulemavu cha Buhangija wilayani Shinyanga baada ya kukabidhi majengo ya vyumba vinne vya madarasa na vyoo kumi, Novemba 10, 2019.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

MKE wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa ametoa wito kwa wazazi na walezi watoto wenye mahitaji maalumu  kutowaficha na kuwatelekeza na badala yake wawape nafasi ya kupata elimu kwa sababu ni haki yao ya msingi.

Mama Majaliwa ambaye pia ni Mlezi wa Umoja wa Wake wa Viongozi (New Mellenium Women Group), ametoa wito huo Novemba 10, 2019 wakati alipokabidhi majengo ya madarasa manne na matundu ya vyoo kumi kwa Kituo cha Watoto Wenye Ulemavu cha Buhangija mkoani Shinyanga yaliyojengwa na umoja huo.

Mama Majaliwa amesema si vyema kuwatenga au kuwakatia tamaa watoto wenye ulemavu kwani wao pia ni watoto sawa na watoto wengine, hivyo wanastahili kupewa haki zote bila kubaguliwa.

Amesema hatua waliyochukuwa akinamama wa umoja huo inaunga mkono jitihada za serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe  Magufuli za kuwapatia watoto wa kitanzanai elimu bure na katika mzingira mazuri.

Mgeni rasmi katika makabidhiano hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa, Joyce Ndalichako ameupongeza umoja  huo kwa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuwajali watoto wenye mahitaji maalumu.

Profesa Ndalichako amesema katika  kipindi  cha  mwaka  2019/2020  Serikali imetenga  jumla  ya  sh 3,809,758,460.00  kwa  ajili ya  kununua  na  kusambaza  vifaa  vya  kufundishia na  kujifunzia  pamoja  na  vifaa  visaidizi  kwa  ajili  ya wanafunzi  wenye  mahitaji  maalum  (wakiwemo Albino),  katika  shule  na  vitengo  vya  elimu  maalum.  

Waziri huyo ameongeza kuwa pamoja  na  juhudi  hizo  za Serikali, bado wanafurahi wanapopata  michango  kama  huo uliotolewa leo. "Wito  wangu kwenu tusichoke  kuwasaidia  hawa  watoto  wetu.  Napenda kuwakumbusha  na  kusisitiza  kwamba  Watu  wenye Ulemavu wanahitaji  msaada  mkubwa  kutoka kwenu."

"Tuwasaidie  na  tushirikiane  kuwapatia mahitaji  yao  muhimu  ikiwa  ni  pamoja  na  elimu, huduma  za  afya  na  mazingira  mazuri  ya kuwawezesha  kuishi  bila  ya  matatizo. Serikali  kwa upande  wake itaendelea  kujitahidi kwa  uwezo kutoa  fursa  zinazojali  mahitaji  yao."

Amesema madarasa  pamoja  na  vyoo alivyokabidhiwa  leo kwa niaba ya uongozi  wa  kituo  cha Buhangija na  Kikundi  cha  New  Millenium ni  tunu kwao na  wananchi  wa  Shinyanga  na  ni  sadaka kwa watoto wa Buhangija, hivyo,  ameutaka uongozi wa  Mkoa  na  Uongozi  wa  Kituo  kwa  pamoja washirikiane  kuyatunza  vizuri  ili yaweze  kutumika kwa  muda  mrefu.

Akitoa taarifa ya ujenzi huo kwa mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela amesema fedha zilizotumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ni sh. 65m,884,523/= ambapo kila chumba cha darasa kimejengwa kwa wastani wa sh. 16,471,130.

Amesema ujenzi wa vyumba kumi vya vyoo  unaendelea na ukikamilika utagharimu sh.26, 271,922.44 na kwamba vyoo hivyo vitakuwa vya kisasa vikiwa na maji ndani pamoja na masinki ya kunawia ili kukidhi mahitaji ya watoto wenye ulemavu.

No comments:

Post a Comment