Dk. Ali Mohamed Shein. |
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein emesema kuwa dhamira
ya Serikali ya kununua Mtambo mpya wa uchapaji wa magazeti ni kuhakikisha
kiwango cha uchapishaji wa magazeti ya Zanzibar leo kinaongezeka.
Dk. Shein amesema hayo
Ikulu mjini Zanzibar, wakati akipokea taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa
Wizara Habari, Utalii na Mambo ya Kale kwa kipindi cha Julai 2018 – Juni 2019.
Amesema hatua ya Shirika
la Magazeti ya Serikali kuchapisha nakala 1,500 katika mtambo ya ZAGPA kwa siku
ni kidogo mno ikilinganishwa na uwezo mkubwa wa mtambo huo wa kuchapisha nakala
35,000 kwa saa moja.
Alisema kuwepo kwa
mtambo huo kunapaswa kwenda sambamba na kiwango kikubwa cha uchapishaji wa
magazeti ili yaweze kuwafikia wananchi hadi walioko mjini na vijijini.
Aidha, alisema kuna
umuhimu wa kuwa na Mawakala wa uuzaji na usambazaji wa magazeti Mikoani,
watakaokuwa na jukumu la kupokea magazeti hayo na kuyasambaza katika shehia
mbali mbali na kuwafikia wananchi.
Katika hatua nyengine, Dk.
Shein alieleza haja kwa baadhi ya vyombo
vya habari nchini kutumia vyema lugha ya
Kiswahili, katika utangazaji na uandishi wa habari akibainisha hali halisi kuwa Zanzibar Mjini ndio kitovu cha lugha
fasaha ya Kiswahili.
Hivyo alitumia fursa hiyo
kuuagiza uongozi wa Wizara hiyo kukutana na wahariri wa vyombo vya habari, kwa
lengo la kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo.
Aidha, aliitaka Idara ya Habari
Maelezo Zanzibar, kuweka utaratibu mzuri wa kutoa Vibali vya kupiga picha, na
kusisitiza umuhimu wa kufuatwa sheria za
nchi, hasa kwa wageni wanaokuja kufanya shughuli hizo hapa Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein
alisisitiza haja ya kuendelea kuzitunza na kuzihifadhi vyema nyaraka za
Serikali.
Dk. Shein alisisitiza
haja kwa uongozi wa Chuo cha Uandishi wa
Habari na Mawasiliano ya Umma kuharakisha
utekelezaji wa uamuzi wa serikali wa
kuanza maandalizi ya msingi ili kukiwezesha Chuo hicho kuunganishwa na Chuo
Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Akigusia uendeshaji wa shughuli
za makumbusho, Dk. Shein aliitaka Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale,
kuendelea kuishajiisha jamii ya Wazanzibari, ikiwemo wanafunzi, kutembelea
maeneo hayo ili kufahamu historia ya asili ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Shein
alisiitiza haja ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano mwema uliopo katika sekta
ya Utalii, kati ya Zanzibar na Indonesia kwa kushirikiana na Chuo cha Utalii
cha Bali cha nchini Indonesia.
Dk. Shein aliupongeza
uongozi wa Wizara hiyo kwa kutekeza
vyema majukumu ya kazi zake, sambamba na kuandaa kwa umakini mkubwa tarifa za
Utekelezaji wa mpango kazi.
Nae, Katibu Mkuu Kiongozi
na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, alisisitiza umuhimu
wa watendaji an wafanyakazi wa Serikali kufanya kazi kwa uadilifu na kutoa
pongezi kwa Wizara hiyo kwa mafanikio iliyoyapata sambamba na kuwasilisha vyema
mpango kazi wake.
Mapema, Waziri wa Wizara
hiyo, Mahamoud Thabit Kombo alisema katika
kipindi cha Julai – Juni 2018/2019 Wizara imefanikiwa kutekeleza miradi
mikuu mitatu, ukiwemo wa ujenzi wa Studio na Ofisi za ZBC Pemba, kupitia
Kampuni ya ujenzi ya Chuo cha Mafunzo Zanzibar, ambapo awamu ya kwanza ya kazi
hiyo inayohusisha ghorofa ya chini imekamilika.
Alisema awamu ya pili ya
ujenzi huo, Mkandarasi ataendelea na kazi itakayohusisha ujenzi wa ghorofa ya pili,
uwezekaji, upigaji wa palasta pamoja upakaji wa rangi.
Aidha, alisema katika
kipindi hicho, Wizara ilishughulikia mradi
wa kuimarisha maeneo ya kihistoria ya Fukuchani na Makamandume, mradi ulioogharimu
shilingi Milioni 850.
Alisema Wizara imeweza kulifanyia
matenegenzo makubwa eneo la kihistoria la Fukuchani, ili kurudisha sura na
haiba yake ya awali.
Alisema matengenezo ya
eneo la kihistoria la Mkamandume yanaendeleo, ukilenga kuziimarisha kuta za
asili katika pande tatu za jengo hilo pamoja na kuvirudisha baadhi ya vivutio
vya asili vilivyomo ndani ya eneo hilo.
Vile vile, alisema katika
kipindi hicho Wizara ilishughulikia mradi wa kuimarisha Utalii kwa wote,
ukihusisha ujenzi wa kituo cha Utalii katika eneo la Kwa Bihole Bungi, mradi
utakaotumia shilingi Bilioni 1.3 hadi kukamilika kwake.
Alisema hatua ya kwanza
ya ujenzi zimeanza chini ya Mkanadarasi Quality Building Contarctor, na kubainisha kuwa
pale utakapomalizika utaongeza vivutio vya utalii nchini, kuimarisha utalii wa
ndani na kimataifa, pamoja na kuongeza ajira kwa jamii, hasa vijana.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na
uongozi wa Wizara ya Katiba na
Sheria na kuipongeza kwa utekelezaji mwema wa majukumu ya kazi sambamba na
uwasilishaji mzuri wa taarifa ya mpango kazi.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kuishauri Wizara hiyo kuzingatia haja ya kuwa na utaratibu maalum katika
utengenezaji wa sheria mpya, ili kuwepo mustakbali mwema wakati ssheria hiyo
itakapohitaji kufanyiwa marekebisho au kufutwa kabisa.
Nae, akiwasilisha taarifa
ya utekelezaji ya Mpango kazi kwa
kipindi cha Julai 2018 – Juni 2019, Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Khamis
Juma Mwalimu alisema pamoja na mambo mengine Wizara imefanikiwa kuimarisha
mfumo wa sheria kwa kufanya mabadiliko ya utendaji kazi wa mahakama,Ofisi ya
DPP, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Polisi, Mafunzo na wadau wengine wa sheria ili
kuwajengea uwezo katika utoaji haki.
Alisema katika
utekelezaji wa majukumu yake, Wizara ilikabiliwa na changamoto ya uhaba wa
watendaji hasa baada kuigaiwa kwa iliokuwa Ofisi ya Rais, Katiba,Sheria na
Utumishi wa Umma na Utawala bora, pamoja na kuanzishwa kwa Idara mpya ya msaada
wa kisheria.
Aidha, alisema katika
kulipatia ufumbuzi suala hilo, Wizara inakusudia kuajiri watendaji kutoka
katika Kada tofauti ili kukidhi mahitaji ya Wizara.
No comments:
Post a Comment