WAZIRI MKUU AZIAGIZA HALMASHAURI KUTENGA MAENEO YA MICHEZO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 10 June 2019

WAZIRI MKUU AZIAGIZA HALMASHAURI KUTENGA MAENEO YA MICHEZO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wanamichezo wakati alipowasili kwenye uwanja wa Nangwada Sijaona mjini Mtwara kufungua Mashindano ya UMISETA, Juni 10, 2019. Wengine Pichani kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelsius Byakanwa, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako, na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Selemani Jafo wakati alipowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Mtwara kufungua michezo ya UMISETA kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Juni 10, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wachezaji wa timu ya soka  mkoa wa Tanga wakati alipofungua mashindano ya UMISETA kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara Juni 10, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagizahalmashauri zote za majiji na miji zihakikishe kuwa kuanzia sasazinatenga maeneo ya michezo na burudani kila zinapopima viwanja.

“Naagiza kuanzia sasa, maeneo yote yanayopimwa na halmashauri na miji yote nchini, lazima yazingatie uwepo wa maeneo ya michezo na burudani,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Juni 10, 2019 wakati akifungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za msingi na sekondari Tanzania, katika Uwanja waNangwanda Sijaona mkoani Mtwara. Zaidi ya wanafunzi 5,400 wanashiriki mashindano hayo.

Pia, amezitaka Halmashauri ziweke mpango madhubuti wa kuyaendeleza maeneo ya michezo na burudani sambamba na miundombinu inayozingatia mahitaji ya wote bila kubagua. Amesema katika baadhi ya maeneo kumekuwepo na uhaba wa viwanja vya michezo kwa sababu ya mipango miji isiyozingatia mipango endelevu ya sekta mbalimbali.

Hivyo, Waziri Mkuu ameagiza yafanyike marekebisho na hatua za haraka ili kutoa fursa ya ukuaji wa michezo na kusaidia wananchi kushiriki michezo, mazoezi na kupata burudani. Amesema ifikapo Septemba 30, 2019, kila halmashauri iwe imefanya mapitio ya maeneo yote yaliyokuwa yamepimwa kwa matumizi ya huduma maalum ikiwemo michezo, burudani, shule na ibada na kutoa taarifa kama yanatumika kwa ajili hiyo au vinginevyo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia irudishe na iimarishe mchepuo wa Elimu kwa Michezo Chuo cha Ualimu Butimba ili kupata wataalam zaidi. 

“Halmashauri ziendelee kuwaruhusu walimu mbalimbali nchini kuhudhuria mafunzo ya michezo katika chuo cha Mendeleo ya Michezo Malya ili kupunguza uhaba wa watalaam wa michezo katika shule mbalimbali na nchini kwa ujumla.”

Waziri Mkuu amesema michezo ni muhimu kwa wanafunzi kwa kuwa itawaepusha vijana na makundi yasiyofaa yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine visivyoendana na maadili ya Kitanzania.

Amesema michezo itawawezesha vijana kuwa na afya bora na kufanya vema katika masomo yao kwa kuwa ili waweze kusoma vema ni sharti afya zao ziwe njema. Pia sanaa itasaidia katika kuutambulisha utamaduni wetu ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. 

 “Kwa hiyo, ni vema tukatambua kuwa michezo na sanaa ni sehemu ya elimu bora. Hivyo, ni muhimu kutekeleza dhana ya elimu ya michezo ili tuweze kufikia maendeleo tarajiwa.”
  Kadhalika, Waziri Mkuu amesema sambamba na michezo iliyozoeleka, pia wanaweza kuibua michezo yao ya asili ambayo itautambulisha utamaduni wetu. “Nitoe wito kwa shule zetu, ziendeleze ubunifu wa kuibua vipaji vya sanaa na michezo ya asili katika maeneo yetu kwa lengo la kuenzi utamaduni wetu.”
Akizungumzia kuhusu mashindano ya mwaka huu ambayo yameshirikisha wanafunzi wengi zaidi wenye mahitaji maalumu, Waziri Mkuu amesema waendelee kuwahusisha wanafunzi wote katika michezo, sanaa na burudani bila kujali aina ya ulemavu walionao. Amesema jambo hilo ni muhimu kwa kuwa vipaji vipo kwa wote na fursa ndizo zitakazowawezesha kuonesha vipaji hivyo na kuvikuza.

Waziri Mkuu amewasisitiza wadau wote wa shule za msingi, sekondari, vyuo, sehemu za kazi na wizara, waweke mipango ya kudumu ya kuwashirikisha watu wenye mahitaji maalumu katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi bila ubaguzi wowote. 

“Hakikisheni baadhi ya vikwazo katika kushirikisha watu wenye mahitaji maalumu kwenye michezo vinaondolewa. Vikwazo hivyo ni pamoja na kutokuwepo kwa mipango endelevu katika maeneo mbalimbali na uwepo wa mitazamo hasi ya baadhi ya walimu, wazazi na viongozi katika maeneo yao dhidi ya uwezo wa wanafunzi wenye mahitaji maalum.”

Aidha, Waziri Mkuu ametuamia fursa hiyo kuupongeza Mkoa wa Simiyu kwa kuwa mmoja kati ya Mikoa ya mfano katika kutekeleza agizo lake la mwaka jana alilolitoa kupitia michezo hiyo la kuanzishwa kwa shule maalumu za michezo.

Mkoa wa Simiyu umejenga Shule ya Sekondari itakayokuwa kituo cha kukuza vipaji vya wanafunzi katika michezo. “Naagiza mwakani wanafunzi wote walioonesha vipaji katika michezo watakaofaulu Mtihani wa Elimu ya Msingi wapangwe katika shule hiyo ili wakakuze vipaji vyao.” 

Amesema bila ya kuwa na mipango ya kulea na kukuza vipaji kutoka ngazi za chini Taifa haliwezi kupata mafanikio katika michezo nchini. Kwani katika kipindi ambapo michezo hiyo ilisitishwa kiwango cha michezo ya aina mbalimbali kilikuwa chini sana.

“Tangu tumerejesha shughuli za michezo katika shule zetu tumekuwa na mafanikio makubwa sana ikiwemo kupata wachezaji wanaofuzu kucheza soka la kulipwa kwenye viwango vya kimataifa kama Mbwana Samatta (Genk –Belgium), Simon Msuva (Difaa El Jadid – Morocco), “

Wengine ni Shiza Kichuya (Enppi –Misri), Thomas Ulimwengu (JS Saoura – Algeria), Hamid Mao (Petrojet – Misri), Adi Yusuph (Blackpool –England), Hassan Kessy (Nkana – Zambia), Yahya Zaydi (Ismaily –Misri), Shabani Chilunda, (Tenerife – Hispania) Rashid Mandawa (BDF- Botswana), Farid Mussa ( Tenerife– Hispania).

Waziri Mkuu amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, jitihada zaidi zinahitajika ili kuwa na maendeleo ya kutosha katika shughuli za michezo nchini. Hivyo, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais TAMISEMI wakamilishe tathmini ya shule 56 za Serikali zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya michezo.

Ufunguzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, Maafisa Elimu kutoka mikoa yote nchini, walimu wa michezo pamoja na Maofisa wengine wa Serikali.

No comments:

Post a Comment