|
Dk. Matomora Matomora. |
· *Amejenga
shule, hospitali na vyuo akizalisha ajira
Na Adam Mwambapa, Tunduru
TAKRIBAN mwendo wa saa 12 umbali wa kilometa 965 unanifikisha
KIUMA. Kitongoji kilichopo kijiji cha Milonde, Kata ya Milonde, Tarafa ya
Matemanga, Wilaya ya Tunduru na mkoa wa Ruvuma.
Dhumuni kubwa ni kukutana na Dk. Matomora Matomora.
Ambaye sifa zake zimeenea sehemu mbalimbali nchini na zaidi sanamikoa ya Kusini
kama, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Akiwa ni miongoni mwa watu wanaoguswa sana na hali duni
ya kiuchumi, za wakazi wa ukanda huo.
Ingawaje najisikia uchovuwa safari uliopitiliza, unaochangiwa
na kukaa kwenye gari muda mrefu huku nikiwa nimebadilisha mikao isiyokuwa na
idadi kamili.
Ila nafarijiwa na jambo moja, nalosi lingine zaidi ya
lengo la ujio wangukijijini hapo kutimia. Hili ndilo kuu.
Ninapoingia kwenye geti la mlango wa Kanisa la Upendo wa
Kristo Masihi (KIUMA), ambalo ndilo lililobeba jina la kitongoji. Siachi
kushangaa!
Kwa nini? Mbele yangu kulia naliona jengo lililo na
maandishi ‘KIUMACOMMUNITY HOSPITAL.’ Naelezwa
kuwa, hiyo ni hospitali yenye uwezo wa kualaza wagonjwa wapatao 100 kwa wakati
mmoja! Na kushoto kwangu ni jengo la Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi (KIUMA).
Wakati ndani ya ua ‘fence’, kumesheheni majengo ya nyumba za watumishi
ambao jumla ya idadi yao naelezwa ni 464, huku idadi kubwa ya wafanyakazi
wakiwa ni Waislamu.
Waama kwa hakika nastaajabishwa sana, kujua ukubwa wa
taasisi niliyoiendea na jitihada zilivyo za kukwamua tatizo la ajira nchini. Lakini pia kuna majengo yashule, viwanja vya michezo
mbalimbali, kumbi za mikutano na chakula, hosteli na vyuo mithili ya kijiji kinachojitegemea.
Ndimo mnamomeremeta kwa mwangaza
wa taa chekwaa. Napata ‘mgagasiko wa moyo,’ na maswaliyasiyo idadi.
Je, ni nishati ipi ya umeme
iliyofanikiwa kuangaza eneo lote hili, ambalo naambiwa lina umbali wa kilomita
tano mpaka sita za mraba? Au je, mradi wa umeme vijijini (REA) wameshafika eneo
hili? Najiuliza hivi,kwa kuwa ni umeme unaowaka humu ndani na si eneo lote la
kijiji.
Wenyeji hawaachi kunijulisha kuwa,ni
nishati itokanayo na jenereta kubwa sana iliyowekwa na Dk. Matomora kwa juhudi
zake, ndiyo iliyowezesha kupang’arisha hapo.
Napumzika kwa lengo la kutimiza ahadi
ya kukutana na Dk. Matomora siku ya kesho yake, ili aweze kunijulisha kuyaelewa
haya na mengineyo.
Ninapata bahati ya kukutana na
Dk. Matomora, anayeanza kueleza matatizo ya mikoa ya Kusini yalivyo na jinsi
wanavyojisikia kutengwa kimaendeleo tafauti na mikoa mingine nchini.
“Kimsingi sisi watu waKusini,
tumelelewa kwenye ‘culture’ moja ya muda mrefu bila kuingiliwa na watu kutoka
nje. Historia inayoanzia tangu tunapata uhuru, ambapo Tanzania ilikuwa na
Majimbo nane moja likiwa ni Kusini,”anaeleza Dk. Matomora.
Anasema kutengwa kwao kulianza
hata katika michezo. Wakati huo Majimbo yote nane yalikutana Dar es Salaam,
ilikuwa ni rahisi sana kwao Jimbo la Kusini kupangwa na timu nzuri ili ifungwe
tu; basi!
“Wazee wa Yanga na Simba wakati
huo ‘Sunlight’ walikuwa wakipangiwa na timu kali kidogo inayojua mpira, kwa
hiyo walikuwa wakifungwa goli nane au 11; na asubuhi saa 12 wanapanda gari
kurejea Lindi,”anaendelea kueleza.
“Hiki kikawa kipimo kizuri cha
unyonge wetu. Kwani hatukuwa na cha ziada kwetu. Tumepata uhuru sawa kwa hulka,
lakini Jimbo hili likagawanyika. Na wakati huohuo Makao Makuu ya Jimbo
yakapelekwa Mtwara…Mtwara na Lindi ni pua na mdomo, na kuna maendeleo kidogo.
Tatizo ni sisi hapa katikati tunaoripoti mkoa wa Ruvuma, ni nani atapaangalia
hapa?”anahoji.
Kwa mujibu wa maelezo yake
anasema hata ukienda kwenye idara yoyote ya Serikali, iwe wizarani au wilayani
kwa sasa, uulize ni lini na ni kiongozi yupi aliyewahi kuja hapa kwetu KIUMA au
Matemanga? Hutapata jibu.
Hii ni kwa sababu, hakuna
kiongozi yeyote anayewiwa au kuumizwa na hali ya unyonge wetu tulionao. Na
pengine sababu kubwa ni umbali ulipo.
|
KIUMA COMMUNITY HOSPITAL. |
Kadhia nyingine kubwa anayoiona
Dk. Matomora, iliyokuwa ikiwatenganisha na kuwatofautisha na wengine kutoka
mikoa mingine, ni idadi ya wanafunzi waliokuwa wakisoma Shule ya Sekondari
Mkwawa iliyokuwa Iringa enzi hizo.
Anasema kwa miaka ile 1964, jumla
ya idadi ya wanafunzi wote waliokuwa wanasoma shule ya Mkwawa ilikuwa ni400.
Hii ilikuwa nikutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.
Lakini kutoka Kusini walikuwa
wanafunzi saba tu; huku aliyetoka Tunduru akiwa ni mmoja tu ambaye ni yeye.
“Wanafunzi wa Tanga, Arusha na
Moshi walikuwa wakiletwa na mabasi manne, wakati wanafunzi wa Tabora na Mwanza
mabasi mawili na Mbeya basi moja; mabasi yaliyoingia hadi shuleni kuwashusha
wanafunzi ndani,”anaeleza na kuendelea:
“Lakini sisi tutokao Kusini, ilitosha
tu kuja nausafiri wa Relwe ambao nao haukutufikisha hadi shuleni.Wakawa wakitushusha
stesheni kulingana na uchache wetu,”anaeleza kwa uchungu.
Dk. Matomorwa ambaye pia ni
Askofu na muasisi wa KIUMA anasema, kitendo hicho ndicho kichochangia fikra
hasi, hasira wakati fulani na kuhoji kwa
nini sisi Kusini hali zetu ni duni kiasi hiki? Hali hii mpaka lini?
Anasema kuwa, wenzaowa Lindi, Songea,
Mtwara, Masasi na Ndanda walikuwa na maendeleo kidogo yenye tija tofauti na
huku kwao anakotambulisha kama Kusini Kati. Kwa sababu, maeneo hayo mengine wao
walikubali na kuwaruhusumapema Wamissionari waingie kwao.
Ndiyo maana huko Ndanda kuna
shule za tangu awali, Peramiho kuna huduma za hospitali tangu hapo.
“Liuli, Litembo, Lituhi na
nyinginezo, ni matokeo ya wenzetu kuwapokea Wamissionari awali na maendeleo
wanayojivunia. Sisi hapa,mtawala wetu mkuu chifu Mataka alihakikisha Wamissionari
hawaingii na zaidi sana alikuwa anawafukuza,”anaeleza Dk. Matomora.
Anazidi kutoa maelezo ya kina kwa
kusema, wakati huo ndiyo maana Serikali ya Kizungu ilishindwa kufanya lolote
lenye maendeleo kwetu…kwa kuwa, kwa huduma za kijamii Serikali ya Kizungu
iliwaachia Wamissionari.
Kumbe kuwakataa na kuwafukuza
Wamissionari enzi hizo, ilikuwa si tu kufifisha huduma za kijamii. Isipokuwa
ilikuwa ni kujikwamisha wenyewe kimaendeo pasipo kujua.
Lakini mbali na hayo, msomi huyu
ambaye alikuwa ni mwalimu wa shule ya udaktari katika Chuo Kikuu Cha Haidonberg
Ujeruman. Anasema, kipimo cha kujua hali ya umaskini katika jamii yoyote, ni
kuwianisha idadi ya watoto wanaozaliwa na vifo vinavyotokea.
Anasema mwaka 2008 kwa mujibu wa
takwimu za kitaifa, katika kila watoto 1000 waliokuwa wakizaliwa kote nchini,
ni watoto 900 waliokuwa wakiendelea hadi kukua.
Hali ambayo kimsingi, pamoja natakwimu
hizo ni ishara kuwa hali ya umaskini ilitishia usalama wa kuishi.
Hata hivyo, kwa wilaya za
Nanyumbu, Namtumbo na Tunduru wastani wa vifo kwa watoto 1000 waliozaliwa,
ilikuwa ni 200 mpaka 215…yaani ilikuwa ni zaidi ya nusu ya wastani kwa nchi
nzima.
Anaendelea kueleza kuwa si hilo
tu. Wakati huo idadi ya wakazi wote wa wilaya ya Tunduru ilikuwa 300,000 jumla
yao, basi kwa idadi hiyo wangetegemea kuona idadi ya wanafunzi wanaoanza darasa
la kwanza kuwa 3000 au na zaidi kidogo.
Hali haikuwa hivyo. Idadi ya
waliokuwa wakianza darasa la kwanza ilikuwa 800, na waliokuwa wakibahatika
kufanya mtihani wa kidato cha nne ni wanafunzi 160 tu! Na kati yao, ni
wanafunzi nane tu waliokuwa wakifaulu.
Anasema hilo pengine masikioni
mwa wengi ni lakawaida sana….lakini lingine lenye kuleta majonzi hata
tunapolisimulia, ni katika shule 20 zilizokuwa zikifanya vibaya sana kitaaluma;
shule 11 zilitoka Bara wakati shule tisa zilitoka Visiwani.
Ajabu ni hii…kati ya hizo 11,
shule saba zilizofanya vibaya sana zilitoka Tunduru. Ni habari zisizo njema
hata kidogo masikioni mwa yeyote.
“Ndipo wenzetu wa Brethlen Church
kutoka Ujerumani walipoguswa mno na hali ya kiumaskini tuliyonayo. Wakaanzisha
huduma inayojulikana na ‘WORD and DEED’, ikiwa na maana usiwape watu chakula
cha kiroho pekee lakini wasaidie pia kwenye matendo kwa kuwapatia huduma za
kijamii,”anaeleza kwa kirefu.
Ndipo hapo wakajiwa na wazo la
kuanzisha Chuo Cha Ufundi, kwa lengo la kuwakwamua vijana ili wasikae vijiweni.
Lakini pia kujaribu kuiondoa hali ya umaskini inayotishia maisha ya wengi.
Na wazo la pili lilikuwa, kwa
kuwa mfadhili wa KIUMA Dk. Ishman alikuwa na taaluma ya utabibu. Hivyo basi,
kwa kushirikiana na Dk. Matomora, ikawa rahisi kwao kuwaza kuanzisha hospitali
ambayo ndiyo taaluma yao.
Lengo ni angalau hospitali hiyo
ifanane-fanane na Peramiho au Ndanda. Wakizingatia kuwa eneo hili ni la
katikati, kwenda Peramiho ni mbali; lakini pia Ndada ni mbali, na watu wa eneo
hili hawana huduma hiyo muhimu.
Kwa msaada wa Mungu, mfadhili
akawasaidia kufungua Shule ya Unesi ‘Nursing School’, ambayo inatoa wanafunzi
800 kwa ngazi ya cheti. Haya ni maendeleo makubwa sana.
Mbali na kuweko kwa shule hiyo
kuna chuo cha useremala, chuo cha ufundi magari, shule ya ‘O level na A level’
na chuo cha Biblia. Ambapo naelezwa idadi ya Waislamu wanaosoma humo ni
asilimia 80; na asilimia zilizobakia ni Wakristo.
Mwisho Dk. Matomora anasema, si bahati mbaya kujenga na kuanzisha Kanisa la
Upendo. Lengo ni kupunguza hasira za ndani za binadamu, ambazo hazionekani wazi
tofauti na zile zinazoonekana.
“Kwa mfano, unaposema nchi yetu
ni yenye amani na wakati huohuo unasikia mapigano na vifo kule Kibiti. Inagwaje
haliko wazi sana, lakini chanzo cha yote yaweza kuwa ni hasira za baadhi ya
wenzetu zilizofichika,”anaeleza na kuongeza:
“Hivyo lengo letu ni kufanya
huduma ya upendo kwa jamii, pia mtu na mtu ili kwamba hasira isiyooneka ambayo
ni mbaya zaidi Mungu akaingilie kati na kuikomesha.”Anamaliza.
Naagana na wenyeji wangu na
kuahidi kurejea pindi nikijaaliwa kwa wakati mwingine, kwa mapenzi na neema ya
Mungu.
0765 937 378
amwambapa7@gmail.com
No comments:
Post a Comment