Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi walioshiriki katika futari iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa Masheikh wa Mikoa ya Kanda ya Kati, Wazee wa Dodoma, Wabunge, Viongozi wa Dini, Wananchi, wawakilishi wa Taasisi mbalimbali na wafanyakazi wa NMB kwenye hoteli ya Dodoma, Mei 24, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania watumie Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kudumisha amani na mshikamano na kuwaombea viongozi wa kitaifa.
“Mwezi huu tuna majukumu makubwa ya kufanya ibada, kutubu dhambi zetu na kuomba rehma kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kudumisha mshikamano na kuwa wavumilivu.”
Waziri Mkuu alitoa wito huo Mei 24, 2019 aliposhiriki hafla ya futari iliyoandaliwa na benki ya NMB iliyofanyika katika Hoteli ya Dodoma.
Alisema kila wananchi aendelee kuliombea Taifa lizidi kudumisha amani na mshikamano. “Tuhakikishe tunatenda matendo mema yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu.”
Kadhalika, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuipongeza benki ya NMB kwa huduma bora wanazozitoa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwa na matawi mengi hadi vijijini.
Awali, Mkurugenzi wa benki ya NMB, Albert Jonkergouwalisema lengo la kuandaa hafla hiyo ya futari ni kuimarisha ushirikiano uliopo baina yao na wateja wao.
Mkurugenzi huyo alisema katika kipindi hiki Waislamu wanapaswa kumrudia Muumba wao na kumshukuru kwa mema yote anayowajalia waja wake.
“Mwezi wa Ramadhan ni kipindi muafaka cha kufuturu pamoja hivyo, nawashukuru wateja wetu kwa kujumuika nasi nawaomba muendelee kutumia huduma zetu.”
Alisema mkusanyiko huo unadhihirisha kuwa wao ni sehemu ya jamii ya Watanzania wote, hivyo aliwasisitiza wateja wa benki hiyo waendelee kutumia zaidi huduma za kidijitali.
Hafla hiyo ilihudhuliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson, Mashekhe wa Mikoa ya Kanda ya Kati (Dodoma, Singida na Manyara).
Wengine ni Wazee wa Dodoma, Waheshimiwa Wabunge , Viongozi wa dini, wananchi, Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali na Wafanyakazi wa NMB.
|
No comments:
Post a Comment