TUHUMA 13 ZA MKURUGENZI ILEJE KUCHUNGUZWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 24 May 2019

TUHUMA 13 ZA MKURUGENZI ILEJE KUCHUNGUZWA

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela (katikati) akiwasikiliza madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Ileje (hawapo pichani) katika kikao ambapo walitoa malalamiko ya kutoridhishwa na utendaji wa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Kulia kwake ni Katibuwa CCM Mkoa wa Songwe Mercy Mollel na Kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Ubatizo Songa.

Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Ileje wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela (hayupo pichani) katika kikao ambapo walitoa malalamiko ya kutoridhishwa na utendaji wa Mkurugenzi wa halmashauri ya Ileje.
MKUU wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela ameunda timu ya kuchunguza tuhuma 13 zilizo elekezwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ileje na kuelekeza kuwa timu hiyo ifanye uchunguzi huo kwa haraka.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela amefikia uamuzi huo mara baada ya majadiliano ya kikao cha pamoja na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje waliomuandikia barua wakiwasilisha tuhuma za kutoridhishwa na utendaji wa Mkurugenzi huyo.
“Nimefanya ziara Wilaya ya Ileje baada ya kupata barua kutoka kwa Madiwani wakimtuhumu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ileje, kabla ya kufanya maamuzi tumejadiliana na nimefikia uamuzi wa kuunda tume ambayo itachunguza tuhuma zote 13 walizowasilisha,” ameeleza Brig. Jen. (Mst) Mwangela.
Amesema kazi kubwa ya tume hiyo ni kuhakikisha wanapata ukweli na uhalisia juu ya tuhuma hizo huku akielezea kuwa moja ya tuhuma ni udhaifu katika kukusanya mapato.
“Kuna tuhuma ambazo tunaona zina ukweli mfano Ileje haijafanya vema katika suala la ukusanyaji wa mapato, sasa tumebakiza mwezi mmoja mwaka wa fedha uishe lakini wamefikia asilimia 58 tu ya makusanyo ambapo ni asilimia ndogo ikiwa lengo ni angalau zaidi ya asilimia 80 kwahiyo hapo kuna dalili za uvujishaji wa mapato,” amefafanua Brig. Jen. (Mst) Mwangela.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela ameongeza kuwa licha ya kwamba uchunguzi unaendelea ametoa maelekezo na mikakati ambayo itasaidia kuhakikisha kazi ya ukusanyaji wa mapato inaendelea vizuri.
“Lengo ni kukusanya vizuri kwahiyo katika kikao tumeweka mikakati itakayosaidia kukusanya mapato na tuna amini waendaji wote wa halmashauri ya Wilaya ya Ileje watafanya kazi kwa umakini mkubwa huku kamati ya fedha na mipango ya madiwani itasimamia hilo vema,” amesema Brig. Jen. (Mst) Mwangela.
Baadhi ya tuhuma ambazo Madiwani wamezielekeza kwa Mkurugenzi wa halmashauri ni pamoja na matumizi mabaya ya ofisi na tuhuma katika masuala ya nidhamu.

No comments:

Post a Comment