MKUU wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaasa wafanyakazi mkoani Rukwa kupunguza matumizi ya simu za mikononi kwaajili ya shughuli binafsi nje na majukumu ya kazi hasa muda wa kazi wanapokuwa ofisini wakiendelea kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Amesema kuwa dhamira ya serikali ya awamu ya tano ni kumtumikia mwananchi kwa nguvu zote hivyo kila mfanyakazi anapaswa kuongeza bidii katika kufanya kazi, lakini kutumia simu na kuacha kuwahudumia wananchi kwa wakati mfanyakazi anakuwa anapata mshahara ambao hausmtahili kutokana na kutotumia muda wake alioajiriwa kwa ufanisi.
“ Ndugu wafanyakazi, hizi simu zimekuwa ni changamoto kubwa sana sehemu zetu za kazi, unakuta mtu badala ya kufanya kazi, hata kutoa huduma kwa mwananchi yeye “ana-chat” kwenye simu, vidole viko kwenye simu, yeye na simu, simu na yeye, kazi haziendi na kama zinakwenda basi zinakwenda kwa mapungufu, kunakuwa hakuna ufanisi na umakini, suala hili la simu tuliangalie sana ndugu waajiri pamoja na waajiriwa,” alisisitiza
Ameongeza kuwa wafanyakazi wamekuwa wakidai maslahi kuliko kupima uwajibikaji wao katika kazi ambazo wanapaswa kuzitekeleza na hali inayopelekea kuzorota kwa kazi nyingi kutokana na wafanyakazi kujishughulisha na matumizi ya simu za mkononi kuliko kuwajibika.
Ameyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kimkoa katika mkoa wa Rukwa yalifanyika katika viwanja vya mpira mji mdogo wa Laela, Wilaya ya Sumbawanga alipokuwa akitoa ufafanuzi wa maeneo nane yenye kulenga kuimarisha utendaji wa kazi ili kuleta maslahi kwa wananchi pamoja na wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi, ikiwemo uwajibikaji, kushughulikia kero za wananchi, uadilifu, usimamizi wa miradi, ubunifu, ushirikiano,kupambana na Rushwa,na kuunda mabaraza ya kazi.
Wakati akisoma risala ya wafanyakazi kwa mgeni rasmi katibu wa shirikisho la vyama huru vya wafanayakazi (TUCTA) Mkoani Rukwa Nashoni Kabombwe alisema kuwa kuna baadhi ya waajiri hawataki kabisa zoezi la kupata wafanyakazi bora kwenye taasisi zao lifanyike kwa kisingizio kwamba hawana fedha wala zawadi yoyote ya kuwalipa.
Katika kushinikiza hilo alisema, “kiwango cha zawadi kwa wafanyakazi bora zinazotolewa na baadhi ya waajiri ni kidogo na hakiendani na mabadiliko ya kiuchumi TUCTA inawataka waajiri kuanzia sasa kiwango cha chini cha zawadi kiwe shilingi 500,000 au kitu chenye thamani isiyopungua fedha hiyo.”
Kwa upande wake Afisa mfawidhi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) katika mikoa ya Rukwa na Katavi Oscar Ngaluka katika mwaka wa fedha 2017/2018 Tume ilipokea jumla ya migogoro ya kikazi 127, wakati iliyomalizwa katika hatua ya usuluhishi ni 93, na inayoendelea na migogoro ni 10 na kuongeza kuwa sekta inayoongoza kwa migogoro mahala pa kazi katika mikoa ya Rukwa na Katavi ni ujenzi wa barabara.
“Sababu zinazoweza kumfanya mfanyakazi afungue mgogoro wake katika Tume ni pamoja na kuachishwa kazi bila ya kuwepo sababu ya kufaa na utaratibu wala kosa, mwajiri kuzuia vyama vya wafanyakazi kutekeleza majukumu yao ya kichama, madai ya stahili mbalimbali na manyanyazo sehemu za kazi,” Alisema.
Kauli mbiu ya siku ya wafanyakazi ni “Tanzania ya Uchumi inawezekana, wakati wa mishahara na maslahi bora kwa wafanyakazi ni sasa” ambapo Tanzania nzima ina vyama vya wafanyakazi 31 huku Mkoa wa Rukwa ukiwa na vyama vya wafanyakazi 9.
No comments:
Post a Comment