DK. REGINALD MENGI AFARIKI DUNIA, RAIS JPM AMLILIA...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 2 May 2019

DK. REGINALD MENGI AFARIKI DUNIA, RAIS JPM AMLILIA...!

Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi.

MWENYEKITI Mtendaji wa Makampuni ya IPP Dk. Reginald Mengi (76) amefariki dunia usiku wa kuamkia Mei 2, 2019.  Taarifa zaidi zinasema Dk. Mengi amefariki dunia akiwa Dubai Falme za Kiarabu. Hata hivyo taarifa hiyo haijatoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na chanzo cha kifo chake.

Dk. Reginald Abraham Mengi alizaliwa wilayani Hai, tarafa ya Machame Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo mara nyingi alikaririwa akisema amezaliwa kwenye familia masikini akichangia chumba anacholalal na mifugo mingine kama mbuzi.

Lakini pamoja na kuwa kwenye mazingira kama hayo, Dkt. Mengi hakukata tama, ndoto yake ya kufanikiwa kimaisha ilisukuma kusoma kwa bidii. 

Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ameguswa na msiba huo pia na ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter; Nimesikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee na Rafiki yangu Dkt. Reginald Mengi. Nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa ktk maendeleo ya Taifa letu na maono yake yaliyopo ktk kitabu chake cha I Can, I Will, I Must. Poleni wanafamilia, wafanyakazi wa IPP na Jumuiya ya Wafanyabiashara,".
Dk. Mengi alisomea masuala ya uhasibu nchini Uingereza na baada ya  kumaliza masomo yake alirejea nyumbani mnamo mwaka 1971 na kuajiriwa na Kampuni ya Uhasibu na Ukaguzi wa Mahesabu ya Coopers & Lybrand Tanzania (kwa sasa inajulikana kama PriceWaterHouseCoopers) hadi Septemba 1989 na katika kipindi hicho alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na Kiongozi mwenza.

Mnamo Oktoba 1989 Dk. Mengi aliondoka Coopers & Lybrand Tanzania na kujielekeza kwenye biashara zake binafsi na kuanzisha IPP Limited, ambayo kwa sasa ni kampuni kubwa binafsi nchini Tanzania.

Biashara ambazo Watanzania wa kawaida walizifahamu, ni pamoja na kumiliki vyombo vya habari mashuhuri kabisa nchini ITV/Radio One, Kampuni ya magazeti ya The Guardian  Limited, Kampuni ya kuzalisha vinywaji baridi ya Bonite.
Dk. Mengi pia chini ya kampuni yake ya IPP alikuwa akifanya biashara mbalimbali na hivi karibuni alisaini kandarasi ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza magari hapa hapa nchini, lakini pia kiwanda cha kutengeneza madawa ya binadamu na vingine vingi.

Dk. Mengi licha ya kushughulika na biashara zake, pia alipenda sana uhifadhi wa mazingira na hilo utalithibitisha ukifika nyumbani kwake Kinondoni na pengine kutokana na sababu hiyo ya kuwa mpenzi wa kuhifadhi mazingira, Serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa, ilimteua kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mazingira (NEMC).

Jamii itamkumbuka Dk. Mengi kutokana na moyo wake wa huruma na upendo, alisaidia makundi mbalimbali ya kijamii kama vile watu wenye ulemavu, ambapo kila mwaka alijumuika nao kwa chakula cha mchana na kubadilishana nao mawazo na lengo kuu likiwa ni kuwashajihisha kutokata tamaa kutokana na ulemavu wao bali wajione kuwa wanaweza kufanya jambo lolote kama wanavyofanya watu wengine.

Makundi mengine ambayo hayatomsahau Dk. Mengi kutokana na mchango wake wa hali na mali ni pamoja na taasisi za kidini (Waislamu na Wakristo), akina mama, vijana na Wazee lakini pia hata mtu mmoja mmoja, wakiwemo watoto wa mitaani.
Dkt. Mengi alipewa tuzo mbalimbali kutoka taasisi mbalimbali ukiwemo ubalozi wa Marekani ambao ulimtunuku tuzo ya Martin Luther king.

No comments:

Post a Comment