WAZIRI MKUU AAGIZA ENEO LA KUMBUKUMBU YA SOKOINE LIBORESHWE HARAKA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 10 April 2019

WAZIRI MKUU AAGIZA ENEO LA KUMBUKUMBU YA SOKOINE LIBORESHWE HARAKA

Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia mnara wa kumbukumbu ya Hayati Moringe Sokoine, uliopo Wami Dakawa wilayani Mvomero, akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam Aprili 10, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa akioneshwa ramani na Kaimu Mhandisi wa Wilaya Silva Mkonda, wakati akikagua mradi wa ujenzi wa Sokoine Memorial High School, wilayani Mvomero Morogoro akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam Aprili 10, 2019. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Steven Kebwe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa akikagua majengo ya shule ya Sokoine Memorial High School, wilayani Mvomero Morogoro akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam Aprili 10, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia mnara wa kumbukumbu ya Hayati Moringe Sokoine, uliopo Wami Dakawa wilayani Mvomero, akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam Aprili 10, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa mkoa wa Morogoro uhakikishe unaboresha eneo la kumbukumbu ya Sokoine lililoko Wami-Dakawa, wilayani Mvomero mkoani Morogoro.

Amewataka Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Steven Kebwe, Mkuu wa Wilaya ya Mvovero, Bw. Mohammed Utali na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw. Florent Kyombo wasimamie haraka uendelezaji na utunzaji wa eneo hilo ili kila mwaka pawe panafanyika shughuli ya kumbukumbu.

Ametoa agizo hilo Aprili 10, 2019 wakati akizungumza na viongozi wa mkoa na watumishi wa wilaya ya Mvomero mara baada ya kukagua ujenzi wa shule ya Sokoine Memorial High School na kutembelea eneo alipopata ajali Waziri Mkuu mstaafu, hayati Edward Moringe Sokoine, Aprili 12, 1984.

“Hili eneo ni maalum. Tulikubaliana ndani ya Serikali liwe sehemu ya kumbukumbu ya Mheshimiwa Edward Moringe Sokoine, na keshokutwa ni miaka 35 ya kumbukumbu yake lakini hakuna chochote ambacho kimeandaliwa hapa kwa ajili hiyo,” amesema.

“Eneo hili liko jirani kabisa na makao makuu ya Halmashauri ya Mvomero. Mngekuwa mmepaendeleza tangu Halmashauri ilipoanza, hata bustani mnayosema mnataka kuiweka ingekuwepo hapa.”

Amesema anashangaa kuona eneo hilo limetelekezwa wakati Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya wapo. “Hili eneo kama lingeendelezwa, naamini hata mbio za kumbukumbu yake zilizofanyika Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita, zingefanyika hapa. Hata wanafamilia wangekuwa wanapita hapa kwa ajili ya kumbukumbu hiyo,” amesema.

“Mkurugenzi wa Halmashauri hapa ni lazima pasafishwe, huku mbele pawe na bustani na hii miti ya mbele iachwe ili papendeze. Mkuu wa Wilaya una Kamati yako ya Ulinzi na Usalama, tumia watu wako ili zoezi hili likamilike,” amesisitiza

Wakati huohuo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema lengo la kuanzisha shule ya Sokoine Memorial High School lilikuwa ni kuweka kumbukumbu yake ili iwe ya kudumu. Amewapongeza kwa kutenga chumba maalum kwenye shule hiyo, ambacho kitatunza kumbukumbu zake.


Ameutaka uongozi wa mkoa na wilaya usimamie ujenzi huo ili yapatikane majengo ya kuanzia kutoa elimu na hatua nyingine zitakamilishhwa wakati wanafunzi wakiwa shuleni.

Shule hiyo ambayo ilianza kujengwa Juni 2017, kwa mfumo wa Force Account, hadi sasa ujenzi wake umeshatumia sh. bilioni 1.7. Ujenzi wa shule hiyo ulisimama Mei, 2018 kutokana na uhaba wa upatikanaji wa fedha.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw. Florent Kyombo inaonesha kuwa hadi sasa madarasa 16, vyoo matundu 16 na ofisi nne za walimu vimejengwa kwa gharama ya sh. 396,988,359 ambapo hadi sasa wanakamilisha uchomeaji wa madirisha pamoja na skiming kuta za ndani na nje.

Taarifa hiyo inaonesha pia kiasi cha sh. 899, 381,643 kimetumika kwa ajili ya ujenzi wa bweni lenye uezo wa kuchukua wanafunzi 256, ambayo hatua iliyofikiwa ni ujenzi wa kuta za ghorofa ya kwanza.

Kazi nyingine ambazo zimefanyika ni ujenzi wa bwalo la chakula (sh. 218,068,299) na ujenzi wa nyumba mkuu wa shule pamoja na nyumba mbili za walimu za two-in-one kwa gharama ya sh. 178,583,000.

No comments:

Post a Comment