Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande (kushoto) kiteta jambo na baadhi ya watu waliofika mahakamani hapo kwa ajili ya kufuatilia shauri hilo. |
Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande akizungumza jambo na wakili Faygrace Sadallah mara baada ya Mahakama kuahirisha kwa muda usikilizaji wa mashahidi wa upande wa Jamhuri. |
Wakili wa kujitegemea David Shiratu, akifurahia jambo na baadhi ya watu waliofika mahakamani hapo kufuatilia shauri hilo.]
Na Dixon Busagaga
MKEMIA kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Hadija Mwema ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Moshi kuwa Vinasaba (DNA) vya sampuli
zilizochukuliwa katika mwili wa anayetajwa kama Humphrey Makundi vimeshabihiana na Vinasaba
(DNA) vya Joyce na Jackson Makundi ambao
wanatajwa kama wazazi wa marehemu.
Dk. Mwema ambaye ni shahidi wa 12 katika shauri la mauji ya
kukusudia ya Mwanafunzi Humphrey Makundi aliyekuwa akisoma kidato cha pili
katika Shule ya Sekondari ya Scholastica aliieleza makama kuwa sehemu iliyotoa
majibu ya vipimo vya DNA ilikuwa ni Nyama na Nywele katika sehemu ya uume vilivyolinganishwa
na Ute wa mate pamoja na Damu vya Joyce na Jackson Makundi.
Eneo la sehemu ya nyama na Nywele katika eneo la uume ni
miongoni mwa sampuli zilizotumika kwa ajili ya vipimo kati ya sampuli 15 ambazo
10 kati ya hizo zilichukuliwa mwilini huku nyingine zikiwa ni viatu na nguo.
Baadhi ya sampuli nyingine zilizotajwa mahakamani hapo katika
ripoti ya vipimo vya DNA ni pamoja na Ngozi ya Kisigino, Mfupa wa Paja, Mfupa wa
Kifua, kipande cha nyama ya tako, viatu jozi mbili, maji mazito yanayopatikana
katikati ya mfupa vyote hivi vikiwa ni vya marehemu.
Mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na
Uhujumu Uchumi, Dar Es Salaam, Firmin Matogoro, shahidi huyo aliiomba Mahakama Kuu Kanda ya Moshi kupokea Ripoti ya Vipimo vya Vinasaba (DNA) iwe sehemu ya
kielelezo katika ushahidi wake ambacho kilipokelewa na kupewa namba nne.
Akiongozwa na Wakili wa serikali Mwandamizi, Abdalah Chavula, Mwema alieza kuwa baada ya kufanya vipimo vya Sampuli mbalimbali matokeo
yaliyoonesha zilichukuliwa katika mwili wa Binadamu.
Mapema Shahidi wa 11 katika shauri hilo linalovuta hisia za
watu, Jackson Daudi aliyejitamburisha kama mbebaji wa mizigo katika kiwanda cha
kutengeneza Saruji cha Moshi aliwasilisha Panga mahakamani hapo
lipokelewe kama kielelezo katika ushahidi wake.
Akiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Joseph Pande, Daudi
ambaye wakati huo alikuwa akifanya shughuli ya ulinzi katika Shule ya Sekondari
ya Scholastica iliyopo Himo katika Wilaya ya Moshi ambako alikuwa akisoma
mwanafunzi Humphrey Makundi.
Alieleza kuwa Novemba 9 mwaka 2017 alifika katika shule hiyo
akitokea Kahama, mkoani Shinyanga ambako alifanya kazi ya ulinzi katika kampuni
ya Solex Security Ltd kabla ya kukutana na mtu aliyemtaja kama mtoto wa Edward
Shayo ambaye alimuunganisha kwenda kufanya kazi katika shule hiyo.
Daudi aliileza Mahakama sababu za kuacha kazi katika kampuni
yake hiyo ya awali ilikuwa ni kutofautiana na muajiri wake baada ya kushindwa
kumlipa mshahara wa mwezi mmoja ndipo alipoamua kuchukua vitu katika kampuni
yake na kuvipelekea kituo cha Polisi.
“Baada ya kuelewana na mwajiri wangu na kunipa pesa na kutoka
kituoni ,nilikutana na mtoto wa Edward Shayo anaye ishi Wilaya ya Kahama ni
Traffic, akaniambia atanipeleka kufanya kazi kwenye shule ya baba yake,” alieleza
Daudi.
Alieleza kuwa Novemba 10, 2017
ikiwa ni siku ya pili tangu kufika shuleni hapo alikutana na Edward Shayo aliyewauliza kama walielewana bei ya kufanya kazi na majibu yake
yalikuwa ni hapana.
“Alituuliza, mlitaka mlipwe shilingi ngapi? tukamjibu shilingi laki mbili “alieleza Daudi huku
Wakili Pande akitaka kujua walikuwa wangapi ndipo akaeleza kuwa walikuwa wawili
yeye na mwenzake aliyemtaja kwa jina moja la Thomas.
Alieleza kuwa Edward Shayo anayetajwa kama mmiliki wa shule
hiyo aliwaambia kuwa atawalipa shilingi laki moja na wao walimueleza kuwa awalipe
kiasi cha shs laki moja na ishirini kiwango ambacho alikubaliana nacho na kutoa
maelekezo ya kumuona mtu aliyeitwa Chacha.
“Chacha alikuwa ni mlinzi, baada ya kumuona tukaambiwa nendeni
mkapumzike mida ya saa 12 twende tukaonyeshwe eneo la kazi, tulikabidhiwa nguo
za kazi," alieleza Daudi.
Daudi ambye mkewe anafanya kazi ya usafi katika shule ya
sekondari ya Scholastica alieleza kuwa utaratibu waliopewa haukuwa wa kulinda
wezi na kwamba walilinda wanafunzi wa shule na kwamba hata wangeingia wezi wangepambana nao.
“Thomas rafiki yangu alibaki pale getini, mimi na Chacha
tukaanza kuzunguka maeneo ya shule sikuwa na kitu chochote, Chacha alikuwa
akitumia Panga na Rungu," alieleza shahidi huyo.
Alieleza kuwa Novemba 17, 2017 baada ya kutoka eneo lao la kazi
walienda kupumzika na Chacha na baadae
mtu aliyemtaja kwa jina la Mcha Mungu liyekuwa mlinzi wa getini alifika na kuwaita bila ya kuwaeleza kuwa
wanaitwa na nani.
“Tuliendelea kulala, Mchamungu akatuita mara ya pili ,akaita
tena Chacha Chacha mnaitwa ,tukaulizwa tunaitwa na nani? Akatuanmbia mnaitwa na
maaskari ,tukaenda getini tukakuta askari wa kike “trafiki “ “alieleza Daudi.
Shahidi huyo alieleza kuwa baada ya kufika yule Askari
aliuliza anaitwa nani ndipo alipomtajia majina yake ya Jackson Evarlist Daudi
na kueleza kuwa sio yeye huku akiuliza Chacha ni nani.
“Alipouliza Chacha nikamnyooshea kidole huyo hapo, akauliza na
Mchamungu? Nikamnyooshea kidole huyo hapo na siku hiyo ilikuwa ni zamu ya
Mchamungu kukaa getini” alieleza Daudi.
Mnamo Novemba 18 ,2017 majira ya saa mbili za usiku ,Daudi
alieleza kuwa ilifika gari aina ya Landcruser ikiwa na vioo vyeusi ndipo
alipofungua mlango mdogo katika geti la kuingia shuleni hapo ndipo aliposikia
sauti ikimueleza kuwa hawaingii ndani.
“Walikuwa ni maaskari wakafungua mlango wa gari, wakamtoa
Chacha, Chacha akwaongoza maaskari paka pale Panga lilipokuwa ,Panga lilikuwa kwenye kabati ndani ya Chumba cha Mlinzi, kilichopo geti kuu la kuingia shuleni”alieleza
Daudi.
“Walivyokuta Panga askari wakaniuliza tangu nifike hapo
sijawahi kulishika hilo Panga au kulikamata nikasema hapana, nikaulizwa Panga la
nani? Chacha mwenyewe kwa kinywa chake akakili Panga la kwangu,” aliongeza Daudi.
Alieleza kuwa kuna Rungu lilikuwa juu ya meza ambapo pia askari
walitaka kujua endapo nimewahi kulishika na majibu yalikuwa ni hapana na kwamba
baada ya hapo walipiga picha Panga na Rungu kisha wakaongozana na Chacha wakiwa
na vitu hivyo.
Daudi alieleza muonekano wa Panga ulikuwa wa rangi nyeusi huku
likiwa imemeguka kidogo huku akiionesha mahakama Panga hilo na baadae kuiomba
mahakama itoe adhabu kutokana na Panga hilo.
Baada ya kutoa maelezo hayo Wakili Mkuu wa Serikali ,Pande
aliwasilisha ombi mbele ya mahakama kupokea Panga hilo liwe sehemu ya kielelezo
katika ushaidi wa Daudi jambo ambalo lilizua mabishano ya kisheria kwa pande
zote mbili.
Wakili wa kujitegemea, Gwakisa Sambo akiwasilisha ombi kwa
Jaji, Mfawidhi, Matogoro alieleza kupinga ombi hilo akieleza sababu ya kuwa
Wakili Pande si shahidi wa kutoa kielelezo hicho.
“Maombi yetu kwa upande wa prosecutor, ni mahakama hii na
mahakama zetu nchini ni shahidi pekee yake ambaye anaweza kuleta ombi hilo, hivyo
basi tunaomba ombi lake likataliwe.
Baadae alisimama wakili Pande na kuunga mkono hoja ya Wakili
Sambo huku akileza kuwa ni kweli anayetoa kielelezo ni shahidi lakini anayeomba
kielelezo kipokelewe ni upande wa Jamhuri na kwamba hivyo ni vitu viwili
tofauti.
Shauri hilo linaendelea katika Mahakama Kuu Kanda ya
Moshi,ambapo mashahidi wa upande wa jamhuri wameendelea kuwasilisha ushahidi
wao.
Shauri
la mauaji ya mwanafunzi Humphrey Makundi aliyekuwa akisoma kidato
cha pili katika sekondari ya Scolastika imeanza kusikilizwa
mfululuzo likimkabili mmiliki wa shule hiyo ,Edward Shayo,Mwalimu wa
nidhamu Labani Nabiswa na mlinzi wa shule ,Hamis Chacha.
Upande
wa Jamhuri katika Shauri hilo unawakilishwa na Wakili wa serikali Mkuu ,Joseph
Pande,Wakili wa serikali Mwandamizi ,Abdala Chavula,Wakili wa serikali
Mwandamizi ,Omary Kibwana na Wakili wa serikali Lucy Kiusa.
Upande
wa utetezi unawakilishwa na Wakili wa kujitegemea Elikunda Kipoko na Gwakisa
Sambo wanaomtetea mshtakiwa wa pili ,Wakili wa kijitegemea David Shilatu
anayemtetea mshitakiwa wa kwanza na Patrick Paul anaye mtetea mshtakiwa wa
tatu.
No comments:
Post a Comment