SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), leo limezinduwa Kituo cha Huduma kwa Wateja katika eneo la Kijitonyama jijini Dar es Salaam ikiwa ni jitihada za kusogeza huduma bora kwa Wananchi za shirika hilo.
Akizinduwa kituo hicho, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Ndugu, Benjami Sitta amelipongeza shirika hilo kwa kuendelea kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kusogeza karibu zaidi na Wananchi.
Alisema ulimwengu wa sasa umetawaliwa na maendeleo makubwa ya Sayansi na Teknolojia ambapo dunia imekuwa kama Kijiji, hivyo kuitaka TTCL kutumia vyema faida hiyo ya Maendeleo ya kiteknolojia kwa kuhakikisha kuwa Huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji ya Wateja.
"...Sina shaka na uwezo katika Eneo la Huduma kwa Wateja ila nashauri msibweteke, endeleeni kuwa mfano bora kwa wengine. Kituo hiki kiwe wazi muda wote uliopangwa, bidhaa zote za TTCL na T PESA zipatikane, Watumishi watakaotoa huduma hapa wawe na Weledi, wazingatie Lugha nzuri, ucheshi na Maadili ya kazi. Kwa kufanya hivyo, wateja wenu watageuka mabalozi wa kulitangaza Shirika letu kwa Wadau wengine.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation ambaye ni Afisa Mkuu wa Masoko na Mauzo, Ally Mbega alisema uzinduzi wa Kituo hicho cha Huduma kwa Wateja ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitatu (Strategic Business Plan 2016-2019) ambao umeweka msisitizo mkubwa katika kuboresha eneo la Huduma kwa Wateja.
Aidha aliongeza kuwa uzinduzi wa Kituo hicho unaonesha kwa vitendo jinsi gani TTCL mpya ilivyojipanga vyema kuhakikisha huduma zake zinawafikia Wateja katika mazingira mazuri, nadhifu,yanayovutia na kubeba hadhi ya Shirika.
"Kukamilika kwa Kituo hiki cha Huduma kwa Wateja kunaongeza idadi ya Maduka/Vituo vya Huduma kwa Wateja vipya na vilivyoboreshwa kufikia 13 ambavyo vimejengwa kwa viwango vya hali ya juu na kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya utoaji bora wa Huduma kwa Wateja," alisema Bw. Mbega.
Pamoja na hayo alibainisha kuwa, TTCL itaendelea kuboresha Maduka na Vituo vyake Nchi nzima, sambamba na Ofisi za Mikoani na Wilayani ili ziweze kuwa mahali bora kwa Watumishi wa TTCL kutoa huduma na Wateja wote watakaofika kupata huduma za aina mbalimbali.
Baadhi ya watoa huduma wa Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) cha Kijitonyama jijini Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja. |
Sehemu ya wafanyakazi wa TTCL pamoja na wageni waalikwa wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Kijitonyama jijini Dar es Salaam. |
No comments:
Post a Comment