Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa
akisalimiana na Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Masele mara baada ya
kuwasili katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
|
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa TEMESA. |
NAIBU Waziri wa Ujenzi
Mhe. Elias John Kwandikwa ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme nchini(TEMESA),
kufanya kazi kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kieletroniki ili kuimarisha
usalama na kuongeza ukusanyaji wa mapato katika huduma zake.
Naibu Waziri Kwandikwa
amesema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua Mkutano wa Baraza la
Wafanyakazi wa TEMESA, na kusisitiza umuhimu wa kila mfanyakazi kufikiria
usalama na uboreshaji wa huduma katika eneo lake la kazi.
"...Hakikisheni
mifumo yote ya kimawasiliano na kimapato inaunganishwa pamoja ili iwe rahisi
kufuatilia ubora na uhakika wa huduma zenu nchini kote na hivyo kuwawezesha
kutoa huduma bora," amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.
Amewataka TEMESA
kuhakikisha inaongeza imani kwa wateja wake kwa kutoa huduma bora wakati wote
na kudhibiti rushwa na uzembe katika utendaji wa kazi wa siku kwa siku.
Aidha, Naibu Waziri
huyo amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TEMESA kuhakikisha watumishi wote wa wakala
huo wanapata fursa za mafunzo ili kuwiana na mabadiliko ya sayansi na
teknolojia yanayoendelea duniani na hivyo kutoa huduma yenye tija kwa wakati.
Naye Mtendaji Mkuu wa
TEMESA, Mhandisi Japhet Masele amesema taasisi yake imejipanga kukusanya madeni
ya huduma ilizozitoa kwa wakati na kupeleka huduma hizo pia katika maeneo ya
wilaya ili kuongeza wigo wa huduma zake kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa
TEMESA itaendelea kujenga vivuko vipya na kukarabati baadhi ya karakana zake
ili kutoa huduma bora na za haraka kwa wananchi.
Mkutano wa Baraza la
Wafanyakazi la TEMESA uliofunguliwa leo pamoja na mambo mengine umepitisha
dira, mwelekeo na makadirio ya bajeti ya wakala huo kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Imetolewa
na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment