NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amezionya na kuzitaka Taasisi za Uhifadhi kuacha tabia ya kuwabughudhi wananchi wanaoishi katika vijiji na vitongoji 366 vilivyokutwa ndani ya Hifadhi katika maeneo mbalimbali nchini mpaka hapo maamuzi ya Kamati ya Mawaziri saba iliyoundwa kushughulikia suala hilo itakapokamilisha kazi iliyopewa na kuwasilisha ripoti kwa Mhe. Rais.
Hatua hiyo ni kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wakiwemo wakulima na wafugaji wanaoishi katika vijiji na vitongoji hivyo kudai kuwa wamekuwa wakisumbuliwa na mifugo yao kukamatwa mara mara kwa madai ya kukutwa imeingia ndani ya Hifadhi.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kisondoko ambacho ni miongoni mwa vijiji vilivyomo ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, Mhe. Kanyasu amezitaka taasisi hizo kufuata na kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali kuhusu wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.
Aidha, Mhe. Kanyasu ametumia fursa hiyo kuwaonya wananchi ambao wamekuwa wakivamia maeneo mapya ya Hifadhi kwa kisingizio cha kauli aliyoitoa Mhe. Rais kuacha mara moja na kwamba yeyote atakayekamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
"Wananchi ninao walenga ni wale tu ambao walikuwa wakiishi Hifadhini kabla ya kauli ya Rais aliyoitoa mwanzoni mwa mwaka huu" Alisisitiza.
Hata hivyo, Mhe Kanyasu amebainisha kuwa Kamati ya Mawaziri saba iliyoundwa na kuzunguka nchi nchi nzima imebaini kuwa kuna zaidi ya vijiji 820 ambavyo vimo ndani ya Hifadhi mbali ya vile 365 vilivyobainishwa awali na kuwasihi wananchi wasiendelee kuvamia maeneo mengine.
Mhe.Kanyasu ameowanya baadhi ya askari wa wanyamapori wanaoomba rushwa Kutoka kwa wafugaji pindi wanapokamata mifugo yao ili waweze kuiachia waache mara moja tabia hiyo akisisitiza kwamba askari yeyote atakayethibitika atachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa mujibu wa Sheria za utumishi wa Umma.
Mkuu wa wilaya ya Kondoa, Mhe. Sezaria Makota amewataka wananchi hao kuendelea kuwa walinzi wa maeneo hayo huku wakisubili hatma ya taarifa ya kamati ya Mawaziri saba itakayotolewa hivi karibuni.
"Baada ya taarifa hiyo mtajua hatma yenu na kama hapa mtabaki au mtahamishwa na kama mtahamishwa tutajua tutawapeleka eneo gani kwa ajili ya malisho na kilimo." Alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Wananchi, Mwenyekiti wa kijiji cha Kisondoko, Ismail Said amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa baadhi ya askari wa wanyamapori wamekuwa wakikamata mifugo yao na kuomba rushwa na pale makubaliano yanaposhindikana huondoka na mifugo yao. Amesisitiza kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikichochea chuki baina ya wananchi na askari hao jambo linalorudisha nyuma jitihada za Uhifadhi nchini.
No comments:
Post a Comment