RC APONGEZA KASI UJENZI HOSPITALI YA WILAYA NKASI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 22 April 2019

RC APONGEZA KASI UJENZI HOSPITALI YA WILAYA NKASI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akisaidia kuweka mchanga kwenye viroba kwa mmoja wa kinamama walioshiriki ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nkasi wakati alipotembelea kuona maendeleo ya ujenzi huo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Jaochim Wangabo akimpatia fredha ya 'kunywa maji' mmoja wa wakinamama kwa niaba ya wakinamama wenzie wanaoshiriki ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Nkasi kama vibarua.

MKUU
wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo amepongeza mshikamano uliopo katika uongozi wa wilaya ya Nkasi unaongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Mh. Said Mtanda baada ya kuona namna uongozi huo ulivyojipanga katika kuhakikisha maelekezo na maagizo ya serikali yanatekelezwa kwa wakati hasa maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nkasi.
Amesema kuwa mshikamano huo ni tunu kwa wanarukwa katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo na hasa linapokuja suala la utekelezaji wa upatikanaji wa huduma ambazo zinawagusa moja kwa moja wananchi waliokuwa wakisubiri huduma hizo kwa muda mrefu.
“Nimeona kwamba mmejipanga kwa kuleta vifaa, na kama hakuna vifaa ujenzi utasuasua, kuna mawe naona yanakwenda kwasababu yanahitajika kwa kasi kubwa, basi hilo eneo liwekewe nguvu kubwa sana, ndio eneo lenye hitaji kubwa kwa sasa na kama hakuna mawe tutashindwa kusogea hatua ya kuweka matofali hadi kufikia hatu ile ya linta,” alisema
Aliongeza kuwa hivi sasa mvua hakuna, hivyo ni wakati muafaka wa kuhakikisha vifaa vyote vinavyohitajika kwaajili ya ujenzi vinakuwa katika eneo hilo la ujenzi ili kila hatua ya ujenzi isikumbane na kikwazo cha kukosa vifaa na kutoa sababu ya mvua kuharibu barabara na hivyo vifaa kushindwa kufika.
Halikadhalika ametoa pongezi kwa namna vibarua wa ujenzi huo wanavyolipwa kwa wakati na kufanya kazi wakiwa wameridhika na malipo wanayopewa jambo linaloashiria kuwa ujenzi huo unakwenda bila ya dosari zozote na kuagiza kuwa hadi kufikia tarehe 10 Mei, 2019 majengo yote saba ya hospitali hiyo yawe yamefikia usawa wa linta ili kwenda na kasi ya utoaji huduma kwa jamii.
Mh. Wangabo ameyasema hayo alipokwenda kuona maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya wilaya inayojengwa katika makao makuu ya wilaya ya Nkasi mjini Namanyere ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa juu ya kuwataka Wakuu wa Mikoa kusimamia kwa karibu ujenzi wa hospitali hizo na hatimae kumalizika kwa wakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alisema kuwa ili kuhakikisha vibarua na wagonga kokoto wanalipwa na mafundi walioingia nao mkataba, wameweka utaratibu wa mafundi hao kuwalipa mbele yake, zoezi linalofanyika katika ukumbi wa ofisi yake ya wilaya na wakati huo huo wakitumia fursa hiyo kuwapatia wagonga kokoto hao vitambulisho vya ujasiliamali.
Imeelezwa kuwa ili majengo saba ya hospitali hiyo yakamilike yanahitajika matofali 78,000 huku hadi tarehe 18 Aprili,2019 matofali 58,000 tayari yameshafyatuliwa ili kuendelea na ujenzi huo.

No comments:

Post a Comment