WAZIRI MHAGAMA AWAFUNDA WATUMISHI WA OFISI YA WAZIRI MKUU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 18 March 2019

WAZIRI MHAGAMA AWAFUNDA WATUMISHI WA OFISI YA WAZIRI MKUU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akihutubia watumishi wa Ofisi yake walioshiriki katika mkutano wa baraza la wafanyakazi la ofisi hiyo uliofanyika Machi 18, 2019 katika Ukumbi wa mikutano wa ofisi hiyo Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama pamoja na Waziri wa Nchi ofisi hiyo anayeshughulikia Uwekezaji Mhe. Angella Kairuki wakikata utepe nyaraka za utendaji kazi kwa viongozi wa baraza la wafanyakazi wa ofisi hiyo wakati wa mkutano wa baraza lao.

Sehemu ya wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia ujumbe kutoka kwa Katibu Mkuu Ofisi hiyo, anayeshughulikia Bunge na Waziri Mkuu Bi.Maimuna Tarishi wakati wa kikao hicho.
NA MWANDISHI WETU
WATUMISHI wa Ofisi ya Waziri Mkuu Uratibu, Sera, Bunge na Uwekezaji wamehimizwa kutumia muda wao wa kazi kwa umakini katika kutekeleza majukumu yao kwa wakati na ufanisi wa hali ya juu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi cha Ofisi hiyo kilichofanyika Machi 18, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo Jijini Dodoma.
“Ni wajibu wa kila mtumishi kuzingatia maadili na weledi katika kuhakikisha utumishi wa umma unaheshimika na kuwajibika kwa ufanisi kwani hakuna haki pasipo wajibu, hivyo kila mtumishi azingatie hayo ili kuwa na utendaji wenye manufaa kwa ofisi na Serikali kwa ujumla,” alisema Mhagama.
Aidha Waziri Mhagama ameziagiza mamlaka zinazosimamia nidhamu katika Wizara hiyo kutosita kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wasiotimiza wajibu wao katika maeneo yao ya kazi ikiwemo watumishi wazembe na wenye tabia ya kuchelewa kazini.
“Serikali ya Awamu ya Tano ya Mhe. Dk. John Pombe Magufuli,inasisitiza utendaji uliotukuka na bidii kwa kuzingatia adhima ya HAPA KAZI TU, hivyo kila mmoja ajitathimini kwa kina kuona namna anavyoenenda na endapo akaona kuna kasoro arekebishe mapema kabla hatua za kinidhamu hazijachukuliwa juu yake,”alisisitiza Waziri Mhagama.
Naye Waziri wa Nchi ofisi hiyo anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki alipongeza watumishi wa ofisi hiyo kwa mafanikio yanayoonekana katika Ofisi hiyo na kutoa wito kwa watumishi kuendeleza jitihada hizo ili kuwa na mazingira mazuri kwa wawekezaji nchini.
“Kipekee niwapongeze watumishi wa Ofisi hii kwa kuendelea kutekeleza vizuri majukumu ya kila siku kwa weledi kwa kuzingatia ukubwa wa ofisi hii, na tuendelee kutekeleza vya ufanisi ili kuvutia wawekezaji nchini waweze kuona fursa na kuwekeza,”alieleza Waziri Kairuki.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ofisi hiyo anayeshughulikia Bunge na Waziri Mkuu Bi. Maimuna Tarishi alimshukuru mgeni rasmi kwa kuwafungulia kikao na kuongezea kuwa Ofisi ya waziri Mkuu inapaswa kuwa mfano katika kusimamia shughuli za mabaraza ikiwa ni sambamaba na kuwataka waajiri kuendelea kuyathamini mabaraza kwa vitendo kwa kuhakikisha kunakuwa na matokeo chanya yenye kuimarisha utendaji wa kazi za kila siku.
“Nawaomba watumishi kuzingatia na kutekeleza wajibu wenu katika majukumu yenu ya kila siku, kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizoainishwa katika mikataba ya ajira nasi tunatoa shime kwa  waajiri kuendelea kuzingatia umuhimu wa kuundwa kwa mabaraza haya na kuyatumia kwa usahihi kama ilivyokusudiwa,” asisitiza Bibi Tarishi

No comments:

Post a Comment