NAIBU WAZIRI KANYASU AWANYOSHEA KIDOLE WATOA HUDUMA HOTELINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 4 March 2019

NAIBU WAZIRI KANYASU AWANYOSHEA KIDOLE WATOA HUDUMA HOTELINI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza  na  wahitimu 21 wa kozi ya ukalimu yanayotolewa bure kupitia mradi wa Trade Aid katika mji mkongwe wa kihistoria wa Mikindani uliopo  katika Manispaa ya Mikindani mkoani Mtwara ambapo Mhe.Kanyasu amewataka wahitimu hao mara watakapoajiriwa waende wakaoneshe utofauti wakawe  mfano bora  kwa kuchochea utalii katika mikoa ya Kusini.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akikabidhi cheti cha kuhitimu kwa Jum Abdallah ambaye ni mhitimu wa kozi ya ukalimu katika chuo cha Old Boma Mikindani mkoani Mtwara.

NAIBU
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu amewanyoshea kidole baadhi ya wahitimu wa masomo ya utalii wanaoajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini wanaoshindwa kutafsiri vyeti na elimu waliyoipata vyuoni kwa kutoa huduma bora kwa watalii nchini.

 Amesema bado kuna tatizo la watoa huduma wengi katika maeneo ya hoteli ambao ni wavivu, wasiojituma, wasio na ubunifu na wasiotumia lugha nzuri kwa watalii.

Akizungumza wakati wa mahafali ya 38 kwa wahitimu 21 wa kozi ya ukarimu yanayotolewa bure kupitia mradi wa Trade Aid, kwenye mji mkongwe wa kihistoria wa Mikindani uliopo  katika Manispaa ya Mikindani mkoani Mtwara, Mhe. Kanyasu amewataka wahitimu hao pindi  watakapoajiriwa waoneshe utofauti na kuwa mfano bora  kwa kuchochea utalii katika mikoa ya Kusini.

 Amesema mradi huo wa Trade Aid umekuwa ukitoa mafunzo hayo  kwa muda wa miezi sita kwa wanafunzi wenye elimu mchanganyiko kuanzia  darasa la saba na kuendelea lengo likiwa kuisaidia jamii ya Mikindani kuchangamkia fursa za utalii.

 Aidha, wanafunzi wanaohitimu mafunzo hayo kila mwaka huajiriwa moja kwa moja kwenye sekta ya hoteli nchini kutokana na ubora wao. Amesema watalii wengi wanaokuja nchini ni matokeo ya huduma bora na pale inapotokea wamehudumiwa vibaya hawawezi tena kurudi.

Hata hivyo, Mhe. Kanyasu amesema licha ya kuwa kuna vyuo vingi vinavyotoa mafunzo hayo kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada, bado watoa huduma walio wengi wamekuwa na uwezo mdogo wa kuwahudumia watalii kwa viwango vya juu ikilinganishwa na elimu waliyonayo.

Amesema licha ya wafanyabiashara  kujenga Hoteli za kitalii katika maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuwapata watoa huduma wenye uwezo wa kutoa huduma bora za kumfanya mtalii aongoze siku za kukaa nchini kutokana na huduma alizopata.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Mikindani, Mhe. Elias Mwanjise akizungumza wakati wa mahafali hayo ametoa wito kwa wahitimu hao pindi  watakapojiriwa wafanye kazi kwa bidii na maarifa ya hali ya juu hali itakayopelekea watalii wengi kuja nchini.

Pia amewataka  wazazi wasiwaozeshe binti zao wanaomaliza darasa LA saba na badala yake wachangamkie fursa hiyo ambayo ni nadra kupatikana katika maeneo mengine.

Naye Meneja wa Mradi wa Trade Aid nchini Tanzania,Barnabas Mwambe  amemweleza Naibu Waziri Mhe. Kanyasu kuwa wahitimu wanaomaliza katika Chuo hicho karibu wote wamekuwa wakiajiriwa  kutokana na ubora wao na jinsi walivyoandaliwa.

Amebainisha kuwa mkazo waliouweka Chuo hapo ni mafunzo kwa vitendo kuliko nadharia ili kuwajengea uwezo wahitimu kutoa huduma bora.

Mbali ya kutoa mafunzo hayo bure, Meneja Mradi huo amesema kuwa wamekuwa wakiwafungulia akaunti za benki pamoja na kuwawekea kiasi cha shilingi 150,000 kwa ajili ya nauli wakati wakitafuta kazi pamoja na kupewa  kadi ya mafao uzeeni.

Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo Bi. Husna Ally akizungumza wakati wa mahafali hayo amesema baada ya kuhitimu mafunzo ameanza kuona mwanga wa maisha kutokana na elimu ya darasa la saba aliyokuwa nayo.

No comments:

Post a Comment