1.
Mchezaji wa timu ya Wanawake ya kuvuta
Kamba ya Uchukuzi SC, Bi. Rachel Manyilizu (kulia) akipokea kombe la ubingwa kutoka
kwa Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Omar Hassan
‘King’ baada ya kuwavuta wenzao wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA),
katika mchezo wa bonanza lililofanyika hivi karibuni kwenye Viwanja vya Maisara
Zanzibar.
1.
Wanamichezo wakipita kwa furaha mbele
ya mgeni rasmi wa bonanza la michezo mbalimbali, Mhe. Omar Hassan ‘King’,
ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Bonanza
hilo limeandaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) na kuialika
Klabu ya Uchukuzi iliyopo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
(Sekta ya Uchukuzi) ya Tanzania Bara na lilifanyika hivi karibuni kwenye
viwanja vya Maisara.
Na
Mwandishi Wetu, Zanzibar
MAMLAKA
ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) imetakiwa kuendelea kudumisha ushirikiano
katika michezo na Klabu ya Michezo ya Uchukuzi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi). Katibu
Mkuu wa Wizara ya Vijana, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mhe. Omar Hassan ‘King’ ametoa kauli hiyo hivi karibuni kwenye
bonanza la michezo mbalimbali lililoandaliwa na ZAA na kufanyika hivi karibuni kwenye
viwanja vya Maisara na Gymkhana Zanzibar.
Mhe.
King amesema sasa umefika wakati kwa Wizara na taasisi za Tanzania Bara na
Visiwani kushirikiana katika michezo ili kudumisha undugu na ujamaa, kwani kwa
sasa michezo maarufu ya Pasaka imeanza kulegalega na haifanyi vyema.
“Nimefurahi
sana kwa bonanza hili hasa kwa kuwaleta wenzetu kutoka Tanzania Bara, na
ninazishauri serikali zote mbili kuweza kuangalia na kuhakikisha wanarejesha michezo
yenye mashirikiano kama ile ya Pasaka na mingine ipewe nafasi na kushirikisha
wachezaji wa pande zote mbili,” Amesema
sera ya michezo inazungumzia kuwepo kwa michezo katika Wizara na taasisi zake.
Mhe
King amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejiimarisha kwenye michezo kwa
takribani miaka mitatu iliyopita kwa kupitia ilani ya chama tawala na iliahidi
kujenga na kuimarisha viwanja vya michezo na sheria za vyama vya michezo na
wameweza kuboresha viwanja vya Amani, Gombani na Mao Zao tung.
Hatahivyo,
ameipongeza ZAA kwa kuandaa bonanza hilo lililoshirikisha wachezaji kutoka
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi) na kushindanisha
michezo zaidi ya 10, na kutaka liwe endelevu kwa kualikana ikiwa ni pamoja na
kupeana zamu ya uandaaji wa kila mwaka.
“Namna
ZAA walivyoandaa bonanza hili imeweza kuwazidi ZBC sio kwamba ninaisifu ZBC kwa
kuwa niliwahi kuifanyia kazi, bali walikuwa wamejiimarisha na kuingia mitaani
na kuanzisha kombe la ZBC Mapinduzi la watoto, na sasa wanakombe linaitwa
Yamleyamle,” amesema.
Amesema
Zanzibar inamichezo 36 na kati ya hiyo 32 inafanya vizuri na minne imepoteza
mwelekeo kwa kufanya vibaya, ambapo pia kumeundwa timu na vyama vingi vya
michezo.
“Michezo
na utamaduni ndio vilivyochangia kuleta Mapinduzi ya Zanzibar, kwani timu ya African
Sport kupitia vikundi vya asili vilivyokuwa maeneo ya Mwembe Msonge, wananchi
walikutana na kucaguzana na kuleta Mapinduzi hayo Januari 12,” amesema,
Mhe.
King amesema michezo inadumisha undugu, urafiki na afya kwani katika michezo
hakuna uhasama na huleta upendo baina ya wanamichezo, hivyo amewataka
wanamichezo na wananchi kwa ujumla kuendelea kujikita katika kucheza michezo
mbalimbali.
Amesema
Zanzibar inahistoria kubwa katika michezo na ilianza tangu mwaka 1875 kwenye viwanja
vya Maisara ambapo awali paliitwa Mnazi Mmoja, na palianzishwa kwa sheria
maalum. Katika mwaka 1875-1879 Manuari za Ujerumani na Uingereza walitumia
viwanja hivyo kwa ajili ya michezo, kwa kuwa wao ndio waliokuwa wakicheza na
sio Waafrika.
Hatahivyo,
amesema Serikali itaweka mazingira bora kwa kuhakikisha klabu za serikali
zinapata nafasi na kuweza kuwezeshwa kushiriki katika michezo mbalimbali.
Naye
Naibu Katibu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mhandisi Shomari
Omar Shomari, amesema bonanza hili la michezo ni moja ya maagizo ya viongozi wa
juu la kuwataka kuwa na ushirikiano baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Kwa
upande wa ZAA na wageni wetu bonanza hili linamanufaa zaidi kwani wafanyakazi
wenu wanafanyakazi saa 24, hivyo wanahitaji kupumzisha akili na mwili, kwani
hili bonanza sio anasa bali ni sehemu ya maisha yetu kwa kuweka afya zetu
vizuri, na ili tuwahudumie vizuri abiria wanaosafiri kwa ndege mnatakiwa kuwa
na furaha na nguvu wakati wote,” amesema.
Mhandisi
Shomari amesema kuanzia sasa bonanza hili litafanyika kila mwaka kwa ngazi ya Wizara.
Naye
Mkurugenzi wa Viwanja wa ZAA, Bi. Zaina Mwalukuta amesema ZAA inalengo la
kudumisha ushirikiano na wenzao wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)
na taasisi nyingine zinazohusiana na usafiri wa anga.
“Tunaomba
ushirikiano huu uendelee kila mwaka kwani bonanza litadumisha undugu na ujamaa,
na kuboresha afya ili kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo Kisukari,
shinikizo la damu na kupelekea kupata kiarusi, kwani wanamichezo watakuwa
wakifanya mazoezi mara kwa mara,”. Amesema Bi. Mwalukuta.
Hatahivyo,
amesema katika miaka ya 1980 na 90 michezo ilichukua nafasi kubwa katika mashirika
ya umma, lakini kwa sasa michezo hiyo imekufa na kubaki katika vyombo vya
ulinzi na usalama na baadhi ya mitaa pekee.
Amesema
ZAA itaendelea kuziunga mkono taasisi zinazoendeleza michezo, lakini pia
ameitaka wizara inayohusiana na michezo kuwasilisha ombi lao kwa serikali Kuu
la kutenga fungu maalum na muda kwa ajili ya ushiriki wa michezo.
Kwa
upande wa mmoja wa viongozi wa Uchukuzi SC, Bw. Joseph Peter amesema
wamejifunza mengi kutoka kwa wenyeji wao ZAA, ambapo mojawapo ni ushirikiano na
upendo wa hali ya juu walionao, na sasa ameomba ushirikiano huo udumu kwa
kuanzishwa kwa mabonanza ya mara kwa mara kwani michezo ni afya na itasaidia
wafanyakazi kufanya kazi kwa weledi wakiwa na afya njema.
“Sasa
inahitajika nguvu ya dhati kwa kuhakikisha mashirika yaliyokuwa na nguvu katika
michezo yanashirikishwa kwenye michezo kwa kuandaliwa Kombe na yafanyike
mashindano na mshindi akabidhiwe kombe ili mradi kuleta mashirikiano na
watumishi wengine wa Umma na Binafsi”.
No comments:
Post a Comment