UJERUMANI YATOA MSAADA KWA WAKIMBIZI NCHINI TANZANIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 17 December 2018

UJERUMANI YATOA MSAADA KWA WAKIMBIZI NCHINI TANZANIA


UJERUMANI YATOA MSAADA KWA WAKIMBIZI NCHINI TANZANIA 



SHIRIKA
 
la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) leo limepokea mchango wa Euro milioni 3.25 kutoka Jamhuri ya Kifederali ya Ujerumani ili kusaidia kazi yake ya kuhudumia wakimbizi na watafutao hifadhi nchini Tanzania kwa mwaka 2018-2019.

“WFP inatoa shukrani za dhati kwa mchango huu mkubwa kutoka kwa Serikali na watu wa Ujerumani,” alisema Michael Dunford, Mwakilishi wa WFP nchini. “Ujerumani ni mshirika muhimu wa programu za WFP ambazo hutoa msaada wa chakula ulio muhimu sana kwa wakimbizi waishio nchini Tanzania.”

WFP hutoa mgao wa chakula cha kila mwezi unaojumuisha nafaka, kunde, mafuta ya mimea na chumvi na vilevile vyakula vya nyongeza vilivyoongezewa virutubisho kwa ajili ya akina mama wajawazito walio hatarini na akina mama wanaonyonyesha, watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, watu wenye utapiamlo wanaoishi na VVU/UKIMWI na wagonjwa waliolazwa hospitali. Licha ya hayo, biskuti zenye kutoa wanga wa kiwango cha juu pia hugawiwa kwa wakimbizi walio katika vituo vya muda.


Tanzania inawahifadhi takribani wakimbizi 290,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, hasa katika kambi za wakimbizi za Nduta, Nyarugusu na Mtendeli katika Mkoa wa Kigoma, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania. Zaidi ya asilimia 70 ya wakimbizi hawa wanatoka Burundi, na waliobaki wanatoka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Nchi yangu inajivunia kuiwezesha WFP kuwahudumia wale walio katika uhitaji ambao wamepata hifadhi nchini Tanzania,” alisema Dkt. Detlef Waechter, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania. “Ni muhimu sana kuweka sawa hali ya kisiasa nchini kwao kabla wakimbizi hawa hawajarudi nyumbani kwao kwa hiyari na usalama.”

Upungufu wa fedha ulilazimisha kupunguzwa kwa mgao wa chakula kati ya Februari, 2017 na Oktoba, mwaka huu, kwa hiyo, kuongezeka huku kwa misaada kutoka kwa wahisani, ikiwemo nchi ya Ujerumani, kumewezesha mgao huo kuanza kutolewa tena katika ukamilifu wake. WFP inaendelea kukusanya fedha ili mgao wa chakula usipunguzwe katika miezi ijayo. 


Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani linaokoa maisha katika maeneo yenye dharura na kuwaletea mamilioni mabadiliko kwa kuhamasisha maendeleo endelevu. WFP inafanya kazi katika zaidi ya nchi 80 duniani kote, likitoa chakula kwa watu walio katika machafuko na waliokumbwa na majanga, na kuweka misingi kwa ajili ya maisha bora ya baadaye.

No comments:

Post a Comment