Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipotembelea eneo la maafa yaliyosababisha kuharibiwa kwa nyumba 336 katika vijiji vya kilyamatundu na kipeta. |
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo amezitahadharisha kaya ambazo bado hazijaweza kurudi katika makazi yao kutokana na nyumba zao kuezuliwa na upepo na mvua kali na kuwafanya kuishi kwa mikusanyiko katika majengo ya serikali juu ya usafi wa mazingira ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko kutokana na uchache wa vyoo katika maeneo hayo.
Amesema kuwa ili kuhakikisha mlipuko huo hautokei ni vyema waathirika hao wakajibana kwa ndugu ambao nyumba zao hazikuathirka na kusisitiza kuwa kujisitiri katika majengo ya serikali ni kwa dharura tu huku wakiendelea kutafuta ufumbuzi wa misaada kwa wadau mbalimbali wa ndani nan je ya mkoa ili kuweza kuzisaidia familia hizo kurudi kwenye makazi yao ya kudumu.
“Tusingependa wandelee kukaa pale, kuna atahari nyingine ya magonjwa ya mlipuko kuwaweka watu zaidi ya 200 sehemu kama ile, miundombinu ya vyoo haitoshi, kwahiyo pale ni pa muda mfupi, jamani wale watu si wana ndugu? Hatuwezi kubanana banana huko, naiachia Halmashauri ndio maana nikasema Mkurugenzi ashuke huku ayaangalie yote haya,” Alisisitiza.
Ameyasema hayo baada ya kuwatembelea waathirika wa mvua na upepo mkali waliohifadhiwa katika kituo cha kilimo kilichopo katika kijiji cha Kipeta, Kata ya Kipeta Wilayani Sumbawanga na kuwapatia misaada ya bati bando moja, gunia la maharage kilo 100, turubai moja, unga wa mahindi tani moja mahindi kilo 200.
Katika hatua nyingine amewatahadharisha wale waliopo katika kamati za maafa ngazi ya kata kuwa makini na misaada hiyo na kuacha fikra ya kuitumia misaada hiyo kwa maslahi yao binafsi na kusisitiza kuwa yeyote atakayejihusisha na tabia hiyo atawajibika kwake.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan haule alitoa taarifa fupi juu ya walichokifanya baada ya maafa kutokea na kusema kuwa maafa hayo yaliathiri vijiji vinne na kitongoji kimoja katika wilaya ya sumbawanga.
“Katika Wilaya yetu maafa haya pia yalitokea kwenye vijiji kama vinne pale (kijiji cha) Muze, kule (Kijiji cha)Msia tumepata taarifa shule ya msingi ya Msia yote imeanguka lakini pia katika kijiji cha Mpwapwa na kule Tunko na kwenye kata hii kuna vijiji viwili na kitongoji cha Kituku,” Alisema
Usiku wa tarehe 8 kuamkia tarehe 9.12.2018 Mvua iliyoambatana na upepo mkali iliweza kuharibu nyumba 336 na kujeruhi watu 49 na kusababisha kifo cha mtu mmoja katika kijiji cha Kipeta na Kilyamatundu vilivyopo kata ya kipeta, katika bonde la ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga.
No comments:
Post a Comment