Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, akiwa katika picha ya pamoja na
wafanyabiashara wa mafuta wa Uganda mara baada ya kukutani nao jijini Mwanza.
SERIKALI imewahakikishia
wafanyabiashara wa mafuta kutoka uganda kuwa imejipanga kutatua changamoto zote zilizopo kwenye usafirishaji ili kupunguza gharama za
uchukuzi kati ya Tanzania na nchi hiyo.
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, amesema hayo
wakati wa kikao maalum kilichowakutanisha wafanyabiashara wa Mafuta wa Uganda
na taasisi za Uchukuzi za Tanzania na kusema kuwa Serikali inatekeleza hayo kwa
kuboresha miundombinu ili kuvutia wafanyabiashara wengi zaidi
“Niwahakikishie
kuwa changamoto zote zilizoainishwa baada ya majumuisho ya ziara yenu ya siku 5
nchini tutazifanyia kazi", amesema Naibu Waziri Nditiye.
Aidha,
Naibu Waziri Nditiye ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu
ikiwemo upanuzi wa bandari,ukarabati wa reli na ukarabati wa meli ili mizigo
inayokwenda Uganda kupitia bandari ya Dar es Salaam ifike kwa wakati.
Kwa
upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya Meli, Eric Hamis amesema mpaka sasa
tayari wamesafirisha zaidi ya tani elfu kumi na tano za Uganda kwa kutumia meli
ya MV Umoja na kusema kuwa wamejipanga kusafirisha mzigo mkubwa zaidi kabla ya
mwaka wa fedha kuisha.
Sisi
kama Kampuni ya meli tuliifanyia ukarabati meli ya MV Umoja na imekuwa
ikisafirisha mzigo wa Uganda na niwahakikishie kuwa kupitia ziara hii na
jitihada nyingine tunazozifanya tutapata wafanyabishara wengine ambao
watasafirisha mizigo yao kwa kutumia meli hii” amesema Hamis.
Kwa
upande wake Mchumi Mwandamizi kutoka Wizara ya Ujenzi ya Uganda, Gerald
Akini, amemwahidi Naibu Waziri Mhandisi Nditiye kuwa yale ya kisera
yanayohusu Uganda atayafikisha katika ngazi husika ili yafanyiwe kazi ili
kuimarisha ushirikiano uliopo kibiashara.
Bw
Gerald ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa utayari wake wa kuwapokea
wafanyabiashara na kuweka mazingira mazuri ili watumie bandari ya Dar es
Salaam.
Aidha,
ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ikiwemo kupunguza
vituo vya mizani,ujenzi wa reli ya kisasa,uboreshaji wa bandari na kuahidi
kuendeleza ushirikiano kwa kushawishi wafanyabiashara wengi zaidi kutumia
bandari ya Dar es salaam.
Wafanyabiashara
wa mafuta kutoka nchini Uganda wamefanya ziara ya siku 5 nchini ambapo
wametembelea bandari ya Dar es salaam, Tanga,Mwanza pamoja na kukagua
miundombinu ya reli na meli za kampuni ya meli na kuridhishwa na hatua
zinazochukuliwa na Tanzania kuimarisha biashara baina ya nchi hizo.
No comments:
Post a Comment