ILI kuokoa zaidi ya wanafunzi 1300 wanaosafiri kwenye maji
kila siku asubuhi kwenda shule katika visiwa vya Ukerewe jijini Mwanza, Waziri
wa Uvuvi na Mifugo Luhaga Mpina amesema serikali itajenga
bweni ili wanafunzi hao waishi shuleni.
Waziri Mpina alitangaza uamuzi huo wakati akipokea msaada wa
vifaa mbalimbali vya uokozi majini vilivyotolewa na Taasisi ya Vodacom Tanzania
Foundation kwa kushirikiana na Sukos Kova Foundation ambao pia wametoa mafunzo
ya uokozi na kujikinga na majanga kwa wanafunzi, walimu, wavuvi na wakazi
wengine wa visiwa hivyo.
Msaada huu unajumuisha makoti ya kujiokolea 1,568, vifaa vya kuzimia moto 21,
mablanketi ya kuzimia moto 21, pamoja na vifaa vya kutolea huduma ya kwanza 21
ikiwa na malengo ya kusaidia shule za sekondari na msingi kuwa na utayari wa
kukabiliana na majanga au maafa mbalimbali pindi yanapotokea. Pia simu za redio 8 pamoja na suti za majini
20 zimegawiwa kwa viongozi wa fukwe za maji.
“Nawashukuru sana Vodacom Tanzania
Foundation kwa msaada huu ambao utawaweka salama wanafunzi wa shule hizi,
lakini pia wakazi wa hapa wanaangukia katika wizara yangu maana wao ni wavuvi,
kwa maana hiyo nina jukumu kubwa la kuwasaidia, na hivyo natangaza kwamba
serikali itajenga bweni moja ili wanafunzi waanze kuishi hapo shuleni,” alisema
Waziri Mpina.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation Bi. Rosalynn Mworia aliunga mkono juhudi
za serikali kwa kuahidi kwamba taasisi yake itanunua magodoro na vitanda kwa
ajili ya bweni hilo pindi litakapokamilika.
“Tumefurahishwa sana na uamuzi wa
serikali wa kujenga bweni hilo, maana hii itaokoa vipaji vingi ambavyo
vingeweza kupotea aidha kwa kukata tamaa maana usafiri wa kwenda shule ni
mgumu, au kutokea kwa majanga ya majini, hivyo basi pindi bweni hilo litakapokamilika
sisi tutaleta vitanda na magodoro kwa ajili ya wanafunzi hao,” alisema Mworia.
Mwanafunzi Editha Fabian kutoka Bwiro
Sekondari alisema wamefurahishwa na uamuzi wa serikali maana utawafanya wasome
kwa bidii zaidi, “tutakuwa katika mazingira salama, hatutachoka maana muda
mwingi tutautumia kusoma badala ya kuwa safarini huku tukiwaza kuzama majini,”
alisema Editha.
Waziri Mpina pia aliziomba taasisi
zote mbili kuandaa mpango mkakati endelevu wa miaka mitatu ili kutoa elimu ya
majanga kwa wakazi wa kanda ya Ziwa Victoria, “mkifanya hivi mtafikia watu
wengi zaidi na pia kutakuwa na uendelevu wa juhudi zenu za pamoja, tafadhali
kaeni chini miliangalie hili kwa kina zaidi,” aliongeza Waziri Mpina.
No comments:
Post a Comment