WAZIRI MKUU ATEMBELEA KITUO CHA AFYA NKOWE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 19 November 2018

WAZIRI MKUU ATEMBELEA KITUO CHA AFYA NKOWE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa amembeba mtoto aliyezaliwa katika kituo cha Afya cha Mkowe wilayani Ruangwa  na Bibi Asia Abdallh (kushoto) wakati alipotembelea wodi ya wazazi katika Kituo hicho Novemba 18, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpongeza Bibi Niachia Kalembo kutoka kijiji cha Mtimbo wilayani Nachingwea ambaye ni mmoja  wa wazazi waliojifungua katika Kituo cha Afya cha Mkowe wilayani Ruangwa wakati alipotembelea kituo hicho, Novemba 18, 2018  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi  khanga Muuguzi wa Kituo cha Afya cha Mkowe wilayani Ruangwa, Grace Nanguka ikiwa ni zawadi ya watumishi wote wa Kituo hicho wakati alipokagua ujenzi na ukarabati wa Kituo hicho, Novemba 18, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kituo cha afya cha Nkowe na kuwataka wananchi wakilinde na kukienzi kwa kuwa ndio mkombozi wao kiafya.

Amesema kwa sasa wananchi hao hawana sababu ya kulipa nauli kwenda Ruangwa kufuata huduma za vipimo na matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo.

Waziri Mkuu ametembelea kituo hicho cha afya leo (Jumapili, Novemba 18, 2018) akiwa katika ziara yake ya kikazi Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Ametaja baadhi ya huduma zinazopatikana kwa sasa kwenye kituo cha Afya Nkowe ambazo awali hazikuwepo kuwa ni pamoja na upasuaji, maabara, mama na mtoto.

“Rais Dkt. John Magufuli anataka kila Mtanzania apate huduma za afya karibu na makazi yake ili asilipe nauli au kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.”

Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na huduma zinazotolewa kituoni hapo, ambapo amewataka watumishi waendelee kuwahudumia wananchi vizuri.

Baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika kituo hicho cha afya wameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya nchini, ambapo kwa sasa wanatibiwa karibu na makazi yao. 

Awali, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dkt. Paul Mbinga alisema kituo hiko kinahudumia jumla ya wakazi 5,264 wa kata ya Nkowe pamoja na wananchi wa kata za jirani za Chienjele, Nandagala, Likunja na Mnacho. 

Alisema baada ya kukamilika kwa mradi huo wananchi sasa wanapata huduma ambazo walikuwa wanalazimika kuzifuata katika hospitali ya wilaya zikiwemo za upasuaji, damu salama, maabara, kujifungua, kulaza wagonjwa na kuhifadhi maiti.

Dkt. Mbinga alisema mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya uliogharimu sh. milioni 500 umepunguza gharama kwa wananchi zinazoambatana kwenda kutibiwa katika hospitali ya wilaya ambayo ipo umbali wa kilomita 20. “Mradi huu umeimarisha mifumo ya huduma kwa watoto, wazee, watu wenye ulemavu na vijana.

Baada ya Waziri Mkuu kutembelea kituo hicho cha afya, alikwenda kukagua ujenzi wa gereza la wilaya ya Ruangwa pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya askari Magereza wa gereza hilo.

No comments:

Post a Comment