Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amekabidhiwa mahindi hayo na kufikia uamuzi wa kuyagawa mara baaada ya kujiridhisha kuwa yaliingia nchini kinyume na taratibu na sheria, yametelekezwa kwa muda wa mwaka mmoja na wamiliki wake na bado yanafaa kwa matumizi ya chakula.
“Mahindi haya kisheria nimekabidhiwa baada ya wamiliki wake kushindwa kufuata sheria na taratibu za nchi yetu, yalitoka nchi jirani na yalikuwa yanapelekwa nchi nyingine jirani, TRA wameyataifisha na nimeona tuwagawie wanafunzi wetu na vituo vya watoto yatima wapate chakula kwakuwa mahindi haya tumejiridhisha pia kuwa yanafaa kwa chakula”, ameongeza.
Meneja wa Ushuru wa Forodha wa Kituo cha mpakani cha Tunduma John Masa amesema bidhaa zote zitakazobainika kusafirishwa kinyume cha taratibu zitataifishwa kama walivyofanya kwenye mahindi hayo baada ya kubaini kuwa yamesafirishwa kwa kukiuka sheria hivyo yamegawiwa kwa Mkoa ambao umetoa kwa wanafunzi na watoto yatima.
Nao baadhi ya wakuu wa shule za sekondari na wawakilishi wa vituo vya watoto yatima ambao wamepokea mahindi hayo ya chakula wameipongeza serikali kwa msaada wa mahindi ambao utasaidia upatikanaji wa chakula katika shule na vituo vyao.
No comments:
Post a Comment