Na Mwandishi Maalum
WATAALAM wa Afya moja nchini ambao ni wataalam wa sekta ya Afya ya binadamu, Afya ya wanyamapori, mifugo, mazingira pamoja na wanasheria wa sekta hizo, wameanza mchakato wa kuandaa sheria ya kudhibiti athari za vimelea hatarishi kwa jamii, sheria hiyo itasimamia ulinzi na usalama wa sampuli za vimelea hivyo.
Vimelea hatarishi vinaweza sambaza magonjwa kwa wanyama na binadamu iwapo ulinzi na usalama wake hautaimarishwa wakati wa kuvichukua kwa wanyama, binadamu na mimea au wakati wa kusafirisha vimelea hivyo na kuvipeleka maabara kwa ajili ya Uchunguzi pia wakati wa kuviharibu mara baada ya kuvifanyia uchunguzi.
Akiongea wakati wa mkutano wa Kamati ya Ufundi ya Usalama wa Afya na Ulinzi dhidi ya vimelea hatarishi vya magonjwa Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe amebainisha kuwa serikali kupitia Dawati la uratibu wa Afya moja lilipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inategemea sana utaalamu wa kamati hiyo kutoa maoni yatakayojumuishwa katika sheria zitakazo simamia udhibiti wa vimelea hatarishi.
“Serikali itaendelea kuilinda jamii ya watanzania dhidi ya majanga yanayoweza kusababishwa na vimelea hatarishi ambavyo husababisha magonjwa ya mlipuko na hatimaye kuleta majanga kwa jamii, kwa kulitambua hilo Ofisi ya Waziri Mkuu imeamua kuwakutanisha wataalamu husika ili watoe maoni yao juu ya udhibiti wenye nguvu ya kisheria” Amesema kanali Matamwe.
Nao waratibu wa masuala ya Ulinzi na Usalama wa vimelea hatarishi katika wizara ya Afya na Mifugo Bw. Jacob Lusekelo na Joseph Masambu walibainisha kuwa udhibiti wa vimelea hatarishi ni muhimu kuwa na nguvu ya sheraia kwani kumekuwepo na muingilianao mkubwa baina ya nchi mbalimbali, ambapo muingiliano huo hungeza milipuko ya magonjwa kwa afya ya binadamu, wanyama na mimea.
Afya Moja ni dhana inayojumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo na mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu, wanyamapori na mifugo. Kwa kutambua umuhimu huo Idara ya Uratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana Wizara ya Afya wameratibu mkutano huo kwa kupata wataalamu kutoka Shirika la DTRA na Ufadhili wa CDC.
No comments:
Post a Comment