Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kulia) akipata
maelezo kuhusu bandari bubu kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu
Kawawa (mwenye koti nyekundu) wakati wa ziara yake ya kukagua bandari bubu hizo
wilayani humo. Anayesikiliza ni Msimamizi wa Bandari ya Bagamoyo, Witharo J.
Witharo.
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akitoa maelekezo kwa kamati
ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Bagamoyo kuhusu kudhibiti bandari bubu
zilizopo wilayani humo wakati wa ziara yake ya kukagua bandari hizo.
NAIBU Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameitaka Mamlaka ya Usimamizi
wa Bandari Tanzania (TPA) kusitisha mpango wake wa kurasimisha bandari bubu
zilizopo mkoa wa Dar es Salaam.
Hayo yameelezwa na
Nditiye wakati wa ziara yake Wilayani Bagamoyo ya kukagua bandari bubu zilizopo
ambapo amebaini uwepo wa bandari bubu zaidi ya kumi na tisa zinazosafirisha
bidhaa kwenye eneo la mwambao wa bahari
lililopo wilayani Bagamoyo. Amesema kuwa uwepo wa bandari bubu hizo ni kipenyo
cha baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi kwa kutumia bandari rasmi na
hivyo kupunguza mapato ya Serikali na kuihujumu nchi kwa kufifisha jitihada za
Serikali za kufikia uchumi wa kati na azma yake ya ujenzi wa viwanda, utoaji wa
huduma za afya, elimu, maji, umeme na ujenzi wa miudombinu ya sehemu mbali
mbali nchini.
Nditiye ameielekeza
TPA iache mara moja mpango huo wa kurasimisha bandari bubu zilizopo Mbweni na
Temeke kwa kuwa Dar es Salaam ipo bandari na itumike hiyo kwa shughuli za
usafirishaji wa bidhaa na abiria. “TPA wafute mara moja mpango wao wa
kurasimisha bandari bubu za Mbweni, Temeke kuwa bandari rasmi wakati kuna
bandari ya Dar es Salaam,” amesema Nditiye. Pia, ameongeza kuwa fedha
zilizotengwa na TPA kwa ajili ya mpango huo lipewe jeshi la bandari ili waweze
kununua vifaa kwa ajili ya kufanya doria ya kuimarisha ulinzi kwenye mwambao wa
bandari.
Amefafanua kuwa yapo
majahazi yanayofanya shughuli za usafirishaji ufukweni mwa bahari ya Hindi
kwenye mwambao upatao kilomita 300 kwenye eneo la Bagamoyo ambapo majahazi
yanashusha mizigo kinyemela. “Nimeshuhudia taratibu za nchi zikikiukwa na
kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Bagamoyo inapata changamoto ila
inawadhibiti kwa namna moja au nyingine japo yapo majahazi yanayoshusha bidhaa
na kuficha kwenye misitu iliyopo ndani ya bahari,” amesema Nditiye.
Pia ameielekeza
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini (TASAC) kufanya utaratibu wa kusajili
majahazi yasiyozidi ishirini kwenye eneo la Bagamoyo ili yaweze kuwahudumia
wananchi wa Bagamoyo na wengine wote watumie bandari Dar es Salaam. “Yapo
baadhi ya majahazi yamesajiliwa ila mengine yanafanya shughuli zake kinyemela
na yanaenda sehemu mbali mbali na baadhi yao wasio waaminifu wanatumia vibaya
vibali vyao na wanashusha mizigo baina ya saa tano na saa tisa usiku,” amesema
Nditiye. Amefafanua kuwa majahazi haya yanakiuka taratibu za nchi kwa
kuwawezesha wafanyabiashara kukwepa kodi na hivyo kupunguza mapato ya Serikali
na jitihada za Serikali za kufikia uchumi wa wakati.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Bagamoyo, Zainabu Kawawa amekiri uwepo wa bandari bubu zaidi ya 19 na
amemweleza Nditiye kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto za uwepo wa
bandari bubu ambazo zinatumia usafiri wa majahazi kuvusha bidhaa mbali ili
kukwepa ushuru wa mamlaka mbali mbali kwa mujibu wa sheria za taasisi husika
ambapo wanavusha sukari, mafuta ya kula, matairi ya magari, maziwa ya unga,
vitenge, khanga, vipodozi na wahamiaji haramu ambapo hadi sasa kuna wafungwa
wapatao 203 waliopo gerezani kutokana na uwepo wa wahamiaji haramu.
Kawawa amefafanua kuwa
majahazi hayo yanashusha mizigo nyakati za usiku wakiwa ndani ya bahari mara
nyingine bila kufika ufukweni kwa kufaulisha na kupakia kwenye mitumbwi ijulikanayo
kwa jina maarufu la ngwanda ili iweze kufikishwa nchi kavu kwa ajili ya
kusambazwa kwenye maeneo mbali mbali ili kukwepa kodi.
Amesema kuwa kamati ya
ulinzi na usalama imekuwa ikifanya doria kwenye maeneo hayo ili kudhibiti jambo
hilo japo wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kufanya doria baharini
na uwepo wa baadhi ya watumishi wa umma wachache wasio waaminifu ambao
wanashirikiana na wafanyabiashara kuihujumu Serikali kwa kutumia bandari bubu zinazotokana na uwepo
wa bahari ya Hindi wilayani humo ambapo bandari bubu hizo ni pamoja na bandari
bubu ya Mlingotini, Kasiki, Kaole, Magambani, Kilimani, Badeco, Msalabani,
Nunge, Mtailindi, Jicho Kuu, Mto Ruvu, Razaba, Gama, Kayanjo – shamba la
chumvi, Saadani, Kitongoji cha Gwaza, Changwahela na Duza.
Naye mmoja wa wamiliki
wa majahazi Khatib Ayubu Mwagala wa bandari bubu ya Mlingotini amekiri kuwa
majahazi yanatumika kusafirisha mizigo na abiria ambapo amesema kuwa, “naweza
kusafirisha wahamiaji waharamu 100 kwa mara moja na bidhaa kama vile mkaa, mbao
na mafuta ya kula”. Aidha, mkazi wa Bagamoyo mzee Ali Nassir Issa amesema kuwa
amekuwa akishuhudia mizigo mingi inashushwa kama vile viongozi wa mamlaka
husika hawaoni na wanakosa mapato.
Naye Afisa Mfawidhi
Msaidizi Bagamoyo, Noel Makere amesema kuwa katika Wilaya ya Bagamoyo kuna
bandari bubu nyingi na ni changamoto katika ukosefu wa mapato. “Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) ina kitengo cha kudhibiti magendo kinachofanya doria kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi hasa nyakati za usiku ili kudhibiti hali hii,”
amesema Makere. Ameongeza kuwa tumefarijika kwa maelekezo aliyotoa Naibu Waziri
Nditiye kwa kamati ya ulinzi na usalama na suala la usajili wa vyombo hivyo
itatusaidia kusimamia, kufuatilia na kuvitambua vyombo halali na visivyo halali
na itasaidia kukusanya mapato ya Serikali.
Naye Msimamizi wa
Bandari ya Bagamoyo, Witharo J. Witharo amesema kuwa bandari bubu ya Mlingotini
ina majahazi na mitumbwi midogo maarufu kwa jina la vingwanda ambapo inatumika
kusafirisha bidhaa kinyume na taratibu. Witharo ameiomba Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA) makao makuu iwapatie boti ya doria kwa kuwa fukwe hiyo iko wazi na kuna misitu ambapo bidhaa za
magendo zinapitishwa humo. Pia, ametoa rai kwa wateja kufika bandarini na
kutumia huduma za bandari zilizo rasmi na kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa
letu.
No comments:
Post a Comment