Afisa Programu wa TenMet, Bi. Alistidia Kamugisha (kushoto) akichangia hoja katika mkutano huo na wanahabari. Kulia ni Bi. Edwick Mapalala. |
MTANDAO wa Elimu Tanzania (TEN/MET) umetoa kauli na kulaani vitendo vya udanganyifu kwenye Shule za Msingi nchini, vilivyofanywa na baadhi ya watendaji wa elimu hadi kusababisha Baraza la Mitihani Tanzania kufuta matokeo ya Darasa la Saba kwa baadhi ya shule.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania, Bi. Cathleen Sekwao alisema kitendo kilichofanywa na watendaji hao waliopewa dhamana ya kusimamia elimu ni sawa na kuhujumu juhudi kubwa za Serikali na wadau wengine wa elimu zinazofanyika kuinua kiwango cha elimu nchini.
Alisema kitendo cha wanafunzi hao kufutiwa matokeo ya mitihani kimewaathiri wanafunzi kisaikolojia na hisia na kuwapotezea uwezo wao wa kujiamini katika kufanya mitihani mingine, licha ya kwamba walioshirikishwa hawakuwa na uwezo wa kupinga wanachoelekezwa na walimu au viongozi katika jambo hilo.
"Ikumbukwe kuwa mtoto wa Darasa la Saba hana uwezo wa kupinga anachoelekezwa na viongozi au walimu wake hivyo huamini kila anachoambiwa afanye ni chema bila kujua madhara yake ya baadae. Ni dhahiri kuwa kitendo cha kufutiwa matokeo ya mitihani kimewaathiri watoto hao kisaikolojia na kihisia na hivyo kuwapotezea uwezo wao wa kujiamini katika kufanya mitihani mingine na safari yao ndefu ya kutimiza ndoto zao," alisema Bi. Sekwao.
Alipongeza uamuzi uliofanywa na Serikali kupitia Baraza la Mitihani kuwafanya warudie mitihani ni jambo jema, inaonesha dhahiri kwamba kuna nia ya kuwapa fursa watoto hao. Pamoja na hayo alishauri muda uliotolewa wa kurudia mitihani hiyo ni mdogo kuwawezesha watoto hao kujiandaa na kujijenga kisaikolojia ili kuwa tayari kufanya mtihani mwingine.
"...Tunapendekeza kuwa angalau wapewe mwezi mmoja wa kujiandaa na kujengwa kisaikolojia...Mtandao unaipongeza Serikali kwa kuweza kubaini kitendo hiki cha hujuma na kuchukua hatua za awali. Ni matarajio yetu kuwa uchunguzi utakapokamilika wale wote waliohusika watachukuliwa hatua stahiki za kisheria na kinidhamu ili iwe fundisho kwa umma," alisisitiza Bi. Sekwao.
No comments:
Post a Comment