Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (kulia) akikagua maendeleo
ya ujenzi wa bandari ya Nyemirembe iliyopo wilayani Chato, Geita. Katikati ni
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa
Wilaya hiyo Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon.
Wafanyakazi wa kampuni
ya mkandarasi ya V.J Mistry & Co. Ltd wakiendelea na kazi mbali mbali za
ujenzi wa bandari ya Nyemirembe iliyopo wilayani Chato, Geita wakati wa ziara ya
Naibu Waziri wa Uchukuzi n Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo
pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo.
NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amemfukuza msimamizi wa ujenzi wa bandari ya Nyemirembe iliyopo wilayani Chato mkoani Geita kwa kukosa sifa na utaalam wa kusimamia ujenzi wa bandari hiyo na miundombinu yake na kuagiza aondolewe mara moja kwenye eneo hilo.
Hayo yamejitokeza
wakati wa ziara ya Nditiye ya kukagua hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa bandari
hiyo na miundombinu yake ambapo mkandarasi wa kampuni ya V.J Mistry & Co. Ltd amepewa jukumu hilo na Serikali
kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ya kujenga bandari hiyo
kwa gharama ya shilingi bilioni 4.128.
Katika ziara hiyo,
Nditiye amebaini kuwa msimamizi wa ujenzi wa bandari hiyo Bwana Pravin Rabadhia
wa mkandarasi wa kampuni ya V.J Mistry & Co. Ltd, hana utaalamu, sifa wala
vigezo vyovyote vya kusimamia mradi huo unaogharimu matumizi ya fedha nyingi
zinazotokana na fedha za makusanyo ya kodi ya wananchi. Pia, alibaini uwepo wa
Bwana Dipak Chaganlal, mfanyakazi wa kampuni hiyo ya mkandarasi
aliyejitambulisha kwa Nditiye kuwa ana taaluma ya “storekeeper” akiwa msimamizi
msaidizi wa mradi wa ujenzi wa bandari hiyo.
Nditiye alielekeza
msimamizi huyo aondolewe eneo la mradi wa ujenzi wa bandari ya Nyemirembe na
mamlaka husika za vibali vya ajira, uhamiaji na mamlaka nyingine za manunuzi,
bodi za makandarasi nchini zimchunguze taaluma yake, uraia wake, uhalali wake
wa kufanya kazi ya kuwa msimamizi wa mradi huo kwa kuwa katika mahojiano nae
akiwa kwenye eneo la mradi huo, wasimamizi hao wenye asilia ya kiasia
hawakuweza kutoa maelezo yoyote ya kitaalamu kuhusu maendeleo ya ujenzi wa
bandari hiyo.
Nditiye ameelekeza
kuwa kazi hiyo ya ujenzi wa bandari ya Nyemirembe isimame kwa muda wa wiki moja
na amemtaka mkandarasi wa kampuni hiyo kufika na kuripoti ofisini kwa Mkuu wa
Mkoa wa Geita mara moja akiwa na wataalamu wanaohitajika kufanya kazi hiyo
kuendana na matakwa ya mkataba husika na kuhakikisha kuwa wafanyakazi na
vibarua wote wanalipwa fedha zao.
Ameongeza kuwa,
Serikali haiwezi kuvumilia jambo hili kwa kuwa tayari imemlipa mkandarasi
malipo ya awali ya asilimia 20 kuendana na makubaliano ya mkataba wa ujenzi huo
yenye thamani ya shilingi milioni 800 katika kipindi cha miezi miwili
iliyoishia ambapo hamna dalili yeyote ya mkandarasi ya kuonesha uwezo wa
kujenga bandari hiyo kwa kuwepo na ukosefu wa vifaa na wataalamu kwenye eneo la
mradi wa ujenzi wa bandari hiyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Geita Mhandisi Robert Gabriel akiwa kwenye ziara hiyo amesema kuwa Serikali ya
Mkoa wa Geita haiko tayari kufanya kazi na mkandarasi wa namna hii labda
wakafanyie kazi zao nje ya Wilaya ya Chato na Mkoa wa Geita kwa kuwa Serikali
imeifanya Wilaya ya Chato kuwa eneo la kimkakati la uwekezaji ili iweze
kuhudumia mikoa ya Geita, Simiyu na Kagera.
“tunapata hamasa kubwa kwa kuona
bandari ya Nyemirembe iliyokufa inafanyiwa kazi ili biashara ya usafirishaji wa
mizigo na abiria ifanyike na tutumie fursa zilizopo kwa kuwa Serikali
inabadilisha matumizi ya pori la akiba la Biharamulo na kuwa hifadhi ya taifa,
hivyo ujenzi wa miundombinu kutainua fursa na kuleta watalii,”amesema Gabriel. Naye
Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon akiwa katika ziara hiyo
alisema kuwa Chato ni kituo kikubwa cha uwekezaji, sekta ya utalii itatumia
bandari hii. Bandari iwe ya kutosheleza abiria 200 hadi 300 na tuangalie namna
ya kupanua eneo ili litoshe mahitai ya miaka 10 hadi 20 baadae.
Kaimu Meneja wa
Bandari za Ziwa Victoria Bwana Morris
Mtindichiusa amemweleza Nditiye kuwa, mkandarasi amesaini mkataba wa ujenzi wa
bandari ya Nyemirembe na miundombinu yake ikiwemo gati la kupakia na kupakua
mizigo, ujenzi wa jengo la abiria, ujenzi wa ghala la kuhifadhia mizigo, ujenzi
wa mnara wa tanki la maji, ujenzi wa vyoo, jengola walinzi, jengo la kuhifadhia
jenereta, uzio na mageti yake.
Ameongeza kuwa
mkandarasi ameanza kazi rasmi tarehe 2 Agosti, 2018 ambapo mkataba ulisainiwa
tarehe 13 Juni 2018 na mkandarasi alikabidhiwa eneo la mradi tarehe 17 Julai,
2018. Mkataba huo ni miezi 12, hivyo ujenzi wa bandari ya Nyemirembe na miundo
mbinu yake unahitajika kukamilika katika kipindi cha mwaka mmoja.
Amefafanua kuwa bandari
hiyo itakuwa na ghala la mizigo lenye uwezo wa kuhifadhi tani 3000 za mizigo na
jengo la abiria litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 200 hivyo watazingatia
maelekezo yaliyotolewa ili liweze kuchukua abiria 300. Pia, amesema kuwa kasi
ya ujenzi wa bandari hiyo na miundombinu yake ni ndogo na hairidhishi kwa kuwa
kwa kiasi cha fedha ambayo mkandarasi amelipwa alitakiwa awe amefikia asilimia
9 ya ujenzi badala ya asilimia 6 waliyofikia sasa.
Hivyo, ameahidi kuzingatia
na kutekeleza maelekezo yalitolewa ya kumuondoa msimamizi wa mradi huo kwenye
eneo la ujenzi wa bandari hiyo na kuhakikisha kuwa mkandarasi wa kampuni hiyo
anafika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chato
kuripoti na kujitambulisha ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa kampuni hiyo
inaweka msimamizi wa mradi mwenye utaalamu na ujuzi unaotakiwa
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment