Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa
uteketezaji wa taka kwa njia salama bila kuathiri mazingira. Warsha hiyo ya
siku moja imefanyika katika ukumbi wa NIMR jijini Dar es Salaam. Kulia ni
Mwakilishi wa Shirikika la Umoja wa Mataifa linalohusika na uendelezaji wa
Viwanda (UNIDO) Dkt. Stephen Kagbo.
Mkurugenzi Msaidizi Idara
ya Mazingira Bi. Magdalena Mtenga akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari
mara baada ya uzinduzi wa warsha ya mradi wa uteketezaji wa taka kwa njia
salama bila kuathiri mazingira. Mradi huo kwa nchi ya Tanzania utatekelezwa
katika Wilaya za Kigamboni na Ubungo.
OFISI ya Makamu wa Rais
kwa kushirikiana na UNIDO hii leo wamezindua warsha ya Mradi wa kudhibiti
kemikali zitokanazo na uchomaji wa taka katika maeneo ya wazi.
Akizindua warsha hiyo
iliyofanyika katika Ukumbi wa NIMR jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu
Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine amesema kuwa mradi huo unatarajia
kuja na mapendekezo ya namna ya kupunguza athari za uchomaji taka katika
mazingira.
Balozi Sokoine amesema
kuwa lengo kubwa la warsha hiyo ya wataalamu ni kujadili mbinu bora za uchomaji
taka bila kuathiri mazingira. “Tunategemea mradi huu utatusaidia sana sisi watu
wa mazingira katika kudhibiti uchomaji hovyo wa taka, uchomaji unaofanyika
maeneo ya wazi unazalisha kemikali ambazo zinadumu kwa muda mrefu katika
mazingira.” Alisisitiza Balozi Sokoine.
Naye Mkurugenzi Msaidizi
Idara ya Mazingira Bi. Magdalena Mtenga amesema kuwa jamii inapaswa kufahamu
kuwa taka ni mali na ni vema zikabadilishwa kuwa fursa, ikiwa ni njia bora ya
kusukuma mbele agenda ya uchumi wa viwanda.
“Uchomaji wa taka
unasababisha uzalishaji wa kemikali hatarishi kwa mazingira ambazo hudumu kwa
muda mrefu na sisi lengo letu ni kudhibiti hii hali ndio maana tumekuja na huu
mradi ili taka zirejerezwe na kutumika
kwa matumizi mengine” Mtenga alisisitiza.
Kwa upande mwingine
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na uendelezaji wa
viwanda (UNIDO) Dkt. Stephen Kagbo amesema uchafuzi wa mazingira ni suala
linalozikabili nchini nyingi barani Afrika hivyo ujio wa mradi huu utatoa fursa
ya kuja na teknolojia ya kisasa ya kuteketeza taka kwa namna bora bila kuathiri
mazingira.
Utekelezaji wa Mradi huo
utaanza katika Wilaya za Ubungo na Kigamboni na nchini nyingine zinazonufaika
na mradi kama huu ni pamoja na Botswana, Lesotho, Madagascar, Mozambique,
Swaziland na Zambia.
No comments:
Post a Comment