KAMPUNI ya simu ya Halotel Tanzania imepanga kutumia kiasi cha milioni 200 kuboresha huduma za mtandao 4G kwa nchi nzima kupitia mtandao huo. Kauli hiyo imetolewa leo jijini Daar es Salaam na Naibu Mkurugenzi wa Halotel Tanzania, Nguyen Van Son alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla fupi ya kusherekea maadhimisho ya miaka mitatu ya kampuni hiyo.
"Hivi karibuni pia Halotel itawekeza kiasi cha Dola za Marekani Milioni 200 kwa ajili ya kuboresha huduma za mtandao na zaidi kuhakikisha inahimarisha mtandao wa 4G kwa wateja wake kote nchini, alisema Bw. Van Son.
Akifafanua zaidi juu ya uwekezaji wa kampuni hiyo, alisema mikakati mipya ni kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani Milioni 700 katika sekta ya mawasiliano nchini ikiwa na malengo ya kuwa nafasi ya pili na kuwafikia wateja zaidi ya Milioni 6 katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza.
Aliongeza kuwa pamoja na mipango, imekusudia kuendelea kuiboresha huduma ya utumaji wa pesa kwa njia ya Mtandao ijulikanayo kama ‘Halopesa’ sambamba na kitengo cha teknolojia ya mawasiliano ‘ICT’ kwa ajili ya wateja wa Mashirika Binafsi na Serikali kwa ujumla.
"Katika kipindi hiki cha miaka mitatu tunapoadhimisha siku hii, Halotel tayari imefanya uwekezaji unaofikia Dola za Marekani Milioni 500, ikiwa ndiyo kampuni inayoongoza kwa kuwekeza miundombinu ya Mawasiliano sehemu mbalimbali nchini inayowafikia asilimia 95 ya wananchi wote ikiwa na vituo 4,400 vya kupokea mawasioliano (BTS’s) kwa umbali wa Kilomita 18,300," alisisitiza Bw. Van Son.
Aidha alisema mpango wa biashara wa Halotel umelenga kuwafikia watu walioko pembezoni mwa miji huku ikitoa huduma kwa gharama nafuu za mawasiliano, ikiwa tayari imewafikia wananchi zaidi ya milioni tatu sambamba na milioni moja wengine waliojiunga na mtandao wa Halopesa.
"Tutaendelea kuboresha huduma zetu mbalimbali tukiwa na lengo la kuwafikia wateja zaidi ya Milioni 6 pamoja na watumiaji Milioni 3 wa huduma ya Halopesa baada ya miaka mitano kuanzia rasmi mwaka ujao , pamoja na kuboresha huduma kwa wateja wetu wakubwa kutoka Taasisi mbalimbali za kibiashara za Binafsi na Serikali."
"Tunaamini kuwa kupitia huduma hizi tutakuwa tumeisaidia Serikali na taasisi zote za kibiashara kuendeleza utoaji wa huduma zao kwa ufanisi wakati huu ambao pia tunatarajia kuandaa mfumo maalumu kwa wateja wetu utakaowawezesha kufanya biashara zao kwa ufanisi." Alisema katika mazungumzo yake.
Alisema kampuni hiyo inaamini itafikia malengo ya kuwa kampuni namba mbili inayotoa mawasiliano yenye tija nchini. Hata hivyo Halotel imekuwa ikishiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii inayoliwezesha Taifa kufikia malengo yake mbalimbali.
No comments:
Post a Comment