Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) kwenye ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete jijini Dodoma Septemba 27, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). |
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Juni, 2018 jumla ya viwanda 1,596 vimejengwa ambapo ni sawa na asilimia 61.4 ya lengo la kujenga viwanda 2,600 hadi Desemba 31, 2018 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la ujenzi wa viwanda 100 katika kila mkoa. Ameyasema hayo Septemba 27, 2018 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema kuwa viwanda hivyo vimejengwa kupitia agizo la Waziri wa Nchi OR- TAMISEMI kwamba kila Mkoa ujenge viwanda 100. Amesema tathmini ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuelekea uchumi wa viwanda, inaonesha kwamba mpaka sasa jumla ya hekta 367,077 zimetengwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya viwanda vikubwa, viwanda vya kati na viwanda vidogo.
“Nitoe wito kwenu kwamba mwendelee kupiga hatua nyingine mbele zaidi katika hili, tujue katika hekta hizo zilizotajwa ni kiasi gani kimerasimishwa kwa viwanda vipi, bidhaa zipi zinazalishwa, hali ya miundombinu ikoje na kuna mikakati gani ya kuiendeleza. Pia tufahamu ni ajira ngapi zilizozalishwa kutokana na uanzishwaji wa viwanda hivyo.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi na wasimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuwawezesha wananchi kushiriki katika kubuni na kusimamia miradi ya maendeleo na kuibua fursa za uwekezaji.
Pia kuanzisha na kuendeleza viwanda vidogo na vikubwa ili Tanzania iweze kufikia lengo la kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. “Tumieni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia vikundi vyao ili wawekeze katika viwanda vidogo vidogo vyenye kuleta tija na kuongeza pato la kaya ili kuutokomeza umaskini.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali katika Dira ya Maendeleo ya 2025 ni kuhakikisha Halmashauri zinakuwa na uwezo wa kujitegemea kimapato kwa zaidi ya asilimia 80 ifikapo 2025.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha lengo hilo linatimia. Serikali imeanzisha utaratibu wa kugharamia miradi ya kimkakati yenye lengo la kuziongezea halmashauri mapato ya uhakika na kupunguza utegemezi wa ruzuku.
“Hadi sasa, sh. bilioni 131.5 zimeidhinishwa kutekeleza miradi ipatayo 22 katika halmashauri 17 zilizokidhi vigezo kwenye mikoa 10. Hivi ninavyozungumza, tayari kiasi cha sh. bilioni 16.4 zimekwishapelekwa kwenye halmashauri hizo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi iliyokusudiwa.”
Waziri Mkuu amesema kuwa uchambuzi wa miradi mingine zaidi unaendelea na halmashauri zitakazokidhi vigezo zitapata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Amesisitiza kwamba fedha hizo zikatumike kwa ajili ya malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo. Amesema kwa sasa, hatutakuwa na utaratibu wa kutoa fedha bila kufahamu kwa kina fedha hizo zinakwenda kufanya nini na zitaleta mabadiliko gani.
“Nimesikia kwamba katika baadhi ya halmashauri fedha zilizokwishatolewa bado hazijaanza kutumika kikamilifu watu wanaendelea kujadili namna ya kuzitumia, niwakumbushe tu kwamba Mheshimiwa Rais hakutoa fedha hizo ili zikakae benki. Wakurugenzi wa Halmashauri mlisaini makubaliano ya matumizi ya fedha hizo, hivyo, zingatieni hilo.”
Waziri Mkuu amewataka Madiwani wasimamie matumizi ya fedha hizo ili halmashauri zipate miradi yenye ubora unaotakiwa, inayolingana na kiasi cha fedha kilichotolewa pamoja na inayokamilika kwa wakati.
Kauli mbiu ya Mkutano huo wa 34 inasema “Umuhimu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Kutoa Huduma na Ushiriki wa Wananchi Kupitia Fursa na Vikwazo Kuelekea Uchumi wa Viwanda”.
Amesema kauli mbiu hiyo, inatilia mkazo maneno ya awali ya Rais Dkt. Magufuli, kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa zipo karibu zaidi na wananchi na zinapaswa kutoa huduma na kuwashirikisha wananchi katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
No comments:
Post a Comment