BENKI ya NMB Plc imesema itaendelea
kusaidia jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kukuza
uchumi wa viwanda nchini Tanzania.
Akizungumza na vyombo vya habari
jana katika mkutano mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT)
unaoendelea jijini Dodoma, Mkuu wa Idara ya Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki
ya NMB, Filbert Mponzi, amesema benki yake imetengeneza program mbalimbali za kusaidia
kuchochea kasi ya uchumi wa viwanda nchini Tanzania.
Hata hivyo, amesema, benki ya
NMB ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 31, ni miongoni mwa taasisi chache
za fedha hapa nchini zinazofanya kazi kwa ukaribu sana na Serikali.
“Kwa mfano, NMB imekuwa mdhamini
mkuu wa mikutano mikuu ya ALAT miaka sita sasa, na kwa mwaka huu, benki imetoa udhamini
wa shilingi milioni 100. Hii inaonyesha utayari wetu katika kufanya kazi pamoja
na Serikali,” alisema.
Aidha, amesema NMB inafanya kazi
pamoja na wilaya na halmashauri zote nchini, ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo rafiki
kwa wafanyakazi wa Serikali.
“Lengo ni kuhakikisha huduma
za kifedha za NMB zinawafikia Watanzania wote nchini hususani wale wanaoishi katika
jamii za vijijini ambapo kunachangamoto nyingi za kimaisha na kiuchumi,” alieleza.
Amesema kwa sasa benki imetenga
kiasi cha shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kutoa mikopo rafiki kwa wajasiliamali
wa kati na wadogo nchini, lengo kuu likiwa ni kuchochea uchumi wa viwanda kupitia
sekta ya kilimo na mifugo.
“Uchumi wa viwanda unategemea
sana sekta ya kilimo na mifugo na hivyo, NMB itaendelea kuwa mstari wa mbele katika
kuwasaidia wajasiliamali wadogo wadogo kupata mikopo nafuu na rafiki ili waweze
kujikita katika miradi husika,” aliongeza.
Pamoja na hayo, amesema ili kuhakikisha
wajasiliamali wanufaika wa mikopo ya NMB wanafikia malengo yao, benki imefungua
vilabu vya biashara nchi nzima, ili kutoa mafunzo maalumu ya mipango biashara.
“Kutokana na usimamizi na utendaji
mzuri wa benki ya NMB, tumefanikiwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 98 kama gawio
kwa Serikali katika kipindi cha miaka saba iliyopita (2010 -2017),” aliongeza.
Mponzi aliongeza kuwa katika
kipindi cha miaka miwili iliyopita, benki imetumia zaidi ya shilingi bilioni
280 kutoa mikopo mbalimbali kwa wakulima na wachakataji wa mazao mbalimbali hapa
nchini.
Kwa upande wake, Meneja wa
NMB Kanda ya Kati, Msolo Mlozi, amesema benki imejipanga vyema kusaidia maendeleo
ya sekta mbalimbali katika kanda ya kati, hususani kipindi hiki ambacho Serikali
imehamishia makao yake makuu rasmi jijini Dodoma.
“Baada ya Serikali kuhamia jijini Dodoma kumekuwa na ongezeko
kubwa la watu, hali ambayo imepelekea pia ongezeko kubwa la mahitaji mengi ambayo
yanahitaji huduma bora na karibu za kifedha. NMB itaendelea kuboresha huduma zake
katika kanda ya kati ili kuchochea kasi ya maendeleo pamoja na kutoa huduma nzuri
zaidi kwa wateja wake,” alieleza.
Mlozi ameitaja baadhi ya mikakati ya benki hiyo katika kanda
ya kati kuwa ni pamoja na kusaidia wakulima wa alizeti, zabibu na mahindi, pamoja
na kutoa mikopo mingine rafiki kwa wajasiliamali.
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa (ALAT) wakipata maelezo walipotembelea banda la Maonesho la Benki ya NMB Ukumbi wa Dr. Jakaya Kikwete Jijini Dodoma jana- mkutano huo umedhaminiwa na benki ya NMB.
No comments:
Post a Comment