Mwezeshaji, na mwana TGNP, Gema Akilimali (kushoto) akishirikishana jambo na maofisa hao. |
Mmoja wa wawezeshaji katika semina hiyo akiwasilisha mada kwa washiriki. |
Mshauri wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi, Dk. Lucy Ssendi (kushoto) akichangia mada. |
Sehemu ya washiriki wa semina hiyo wakifuatilia majadiliano. |
TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu (UNFPA) leo imewakutanisha maofisa mipango na bajeti pamoja na maofisa wanaohusika na masuala ya kijinsia serikalini ili kuangalia namna wanavyoweza kuchochea mpango wa bajeti ya Serikali inayozingatia usawa wa kijinsia kwa kutumia nafasi zao nyeti.
Maofisa walioshirikia katika Semina hiyo ya siku mbili ni kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Akiwasilisha mada kwa maofisa hao, Mshauri wa Maendeleo ya Jinsia, Edward Mhina alisema zipo faida nyingi za Serikali kuandaa bajeti yake kwa mrengo wa kijinsia ikiwa ni pamoja na ongezeko la mapato katika bidhaa na huduma, ongezeko la muda wa kujiliwaza, ongezeko la uwezo wa kuishi maisha toshelezi (mfano kuongezeka furaha na afya njema, uwezo wa kushiriki maamuzi na ujuzi) na ongezeko la Uhifadhi wa mazingira.
Alisema sera za uchumi wa kitaifa huweza kuongeza tija iwapo Serikali itahamasisha uwepo wa viwango vya juu vya tija katika kilimo na elimu kwa wanawake, huku akitahadharisha uwepo wa athari kisera katika uchumi wa taifa endapo kutakuwa na mapengo ya kijinsia katika elimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa nguvu za pamoja TGNP Mtandao, Grace Kisetu awali akizungumza katika semina hiyo alisema lengo la kuchochea uwepo wa bajeti yenye mrengo wa kijinsia ni kuhakikisha mgawanyo wa rasilimali za taifa kwenye bajeti unayafikia na kunufaisha makundi yote kiusawa.
Aidha alisema mbali ya kutokuwepo na usawa katika mgawanyo wa rasilimali za taifa, takwimu zinaonesha kuwa hali ya ukatili wa kijinsia bado ipo juu kwani kwani asilimia 72ya watoto wa kike wa chini ya miaka 11 wamefanyiwa ukatili, huku takwimu hizo zikibainisha kwa kila wasichana 10 wa nne kati yao wamekumbana na ukatili wa kingono.
Afisa huyo aliongeza kuwa nchini Tanzania takwimu zinaonesha kuna takribani wanawake milioni 7.9 waliofanyiwa vitendo vya ukeketaji jambo ambalo ni ukatili kwa kundi hilo, hivyo kuainisha kuna kila sababu za kupaza sauti kuhakikisha vitendo vya unyanyasaji kiujumla vinapigwa vita kila uchao.
Naye Mshauri wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi, Dk. Lucy Ssendi alisema suiala la bajeti inayozingatia mrengo wa kijinsia lina umuhimu mkubwa kuanzia ngazi ngazi ya familia, hivyo kuwaomba maofisa waliopata fursa ya kushiriki semina hiyo kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri katika mabadiliko na kutoa mchango utakaoleta mabadiliko chanya kwenye nafasi zao.
No comments:
Post a Comment