WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametangaza tume ya kuchunguza ajali ya kivuko cha MV Nyerere yenye wajumbe saba ambayo itaongozwa na Jenerali mstaafu, George Waitara.
Akitangaza majina hayo kwenye kijiji cha Bwisya katika kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza Septemba 24, 2018, Waziri Mkuu amesema wajumbe hao wanapaswa kuikamilisha kazi hiyo ndani ya mwezi mmoja.
Amewataja wajumbe wengine kuwa ni Mbunge wa Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi, Mhandisi Marcelina Magesa, Wakili Julius Kalolo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Queen Mlozi.
Wengine ni SACP Camillus Wambura na Mkurugenzi wa Idara ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Bashiru Taratibu Hussein.
Amemwagiza Mkuu wa Majeshi, Jenarali Venance Mabeyo asimamie uundaji wa tume hiyo na kuainisha ni mahitaji gani yanatakiwa kwa haraka na pia afuatilie utekelezaji wake.
MV Nyerere ilipinduka na kuzama Septemba 20, mwaka huu ambapo hadi sasa jumla ya watu 41 wameokolewa na wengine 227 wamepoteza maisha baada ya miili mingine mitatu kupatikana leo asubuhi. Jana yalifanyika mazishi ya kitaifa ambapo miili tisa ilizikwa kwenye eneo la uwanja wa shule ya msingi Bwisya. Miili 214 ilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza itangazwe zabuni ya haraka ya kutengeneza kivuko kingine kipya chenye uwezo wa kubeba tani 50 za mizigo na abiria zaidi ya 200.
“Hili ni agizo la Mheshimiwa Rais, na mimi ninamuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe aitishe zabuni hiyo haraka sana. Kazi hiyo ifanywe mara moja ili kivuko kipya kiweze kutengenezwa na kusaidia wananchi wa eneo hili kwa haraka,” amesema.
Amesema kivuko kipya kikikamilika, itabidi kipangiwe ratiba za safari nyingi zaidi badala ya kwenda mara moja kwa siku ili kuondoka kero ilikuwa ikiwakabili wananchi hao.
No comments:
Post a Comment