WAZIRI MKUU AONGOZA MAMIA KWENYE MAZISHI UKARA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 23 September 2018

WAZIRI MKUU AONGOZA MAMIA KWENYE MAZISHI UKARA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka shada la maua kwenye kaburi  la mmoja wa wananchi walifariki katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama katika katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye kijiji hicho Septemba 23, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima kwenye kaburi  la mmoja wa wananchi walifariki katika ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichozama   katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye kijiji hicho Septemba 23, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda, Renatus Nkwande akiomba katika  mazishi ya wananchi waliofariki dunia katika ajali ya Kivuko cha MV  Nyerere kilichozama katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Mazishi hayo yaliyoongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yalifanyika katika kijiji cha Bwisa kisiwani Bukara, Septemba  23, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapa pole wafiwa katika mazishi ya mwananchi waliofariki katika ajali ya Kivuko cha MV Nyerere kilichozama  katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Majaliwa aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi yaliyofanyika kwenye kijiji cha Bwisa  kisiwani Ukara Septemba 23, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuhusu juhudi zinazofanywa  na wahandishi za kukivuta kivuko cha MV Nyerere kilichozama katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe wakati aliposhiriki katika mazishi ya wananchi waliokufa katika ajali ya kivuko hicho kwenye kijiji cha Bwisa kisiwani Ukara Septemba 23, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Awataka Watanzania waiache Serikali na dola vifanye kazi yake

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza maelfu ya wakazi wa wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza na mkoa jirani wa Mara katika mazishi ya kitaifa ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya MV Nyerere Septemba 20, mwaka huu.

Waziri Mkuu ambaye ameongoza mazishi hayo Septemba 23, 2018 kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, amewataka Watanzania waiache Serikali na vyombo vya dola viendelee kufanya kazi yake.

“Wito wa Serikali kwenu wote, ni kuwasihi tushikamane na wenzetu waliopoteza ndugu zao, wakiwemo wazazi, kaka, dada na watoto. Ninaomba tuiache Serikali na vyombo vya dola viendelee kufanya kazi yake. Tuendelee kuwa wavumilivu,” amesema.

Akiwasilisha salamu za rambirambi kutoka kwa Rais Magufuli mbele ya wafiwa na waombolezaji, Waziri Mkuu amesema: “Mheshimiwa Rais alipokea tukio hili kwa mshtuko mkubwa na anawapa pole sana wafiwa wote pia anawaombea majeruhi wote wapate ahueni mapema.”

Amesema jumla ya watu 224 walipoteza maisha kutokana na ajali hiyo. Kati ya hao, miili 214 kati ya 219 iliyotambuliwa, ilichukuliwa na ndugu zao. Miili minne haikuweza kutambuliwa lakini ipo miili mitano ambayo ilitambuliwa na ndugu zao na hao ndugu wakaona ni vema wazikwe hapa eneo la tukio. Kwa hiyo leo tutawazika ndugu zetu tisa katika eneo hili,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua ya kuunda tume ya uchunguzi na kuahidi kwamba tume hiyo itatangazwa wakati wowote. “Tume ikikamilisha kazi yake, wote watakaobainika kuwa wamehusika watachukuliwa hatua mara moja,” amesema.

Ili kukabiliana na tatizo la usafiri lililopo, Waziri Mkuu amesema meli ya MV Nyehunge imeanza kutoa huduma ya usafiri wa muda badala ya MV Nyerere iliyokuwa ikitoa huduma kati ya bandari ndogo ya Bugolora, Ukerewe na kisiwa kidogo cha Ukara.

Amesema jitihada za kuivuta meli ya MV Nyerere iliyopinduka zinaendelea na kwamba maafisa wote wanaohusika na usafiri wa majini ambao walizembea kwenye suala hilo, wamekamatwa na wameanza kuhojiwa.

Akigusia chanzo cha ajali hiyo, Waziri Mkuu amesema inasadikiwa kivuko cha MV Nyerere kilibeba mizigo mingi kuliko uwezo wake ambao ni wa kubeba tani 25 za mizigo, magari matatu na abiria 101. “Hadi sasa inaonesha kulikuwa na watu zaidi ya 260, yaani 41 waliookolewa na 224 waliopoteza maisha,” amesema.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wote wa Ukara waliojitokeza kusaidia kazi ya uokoaji tangu ajali hiyo ilipotokea. Pia aliwashukuru wote waliotoa michango mbalimbali, watumishi wa hospitali za Bugando, Sekou Toure, Ukerewe, kituo cha afya cha Bwisya na timu nzima inayofanya kazi ya uokoaji na uopoaji wa miili kwa kazi kubwa waliyoifanya.

Wakati huohuo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama ametangaza namba ya tigopesa ambayo wananchi wanaweza kuitumia kutuma michango yao kwa ajili ya waliopatwa na maafa hayo.

“Tumefungua akaunti ya maafa kwenye Benki ya NMB tawi la Kenyatta lakini ili kurahisisha upokeaji wa michango kutoka kwa wananchi wa kawaida, tumesajili namba ya tigo yenye namba 0677-030-000 kwa jina la RAS Mwanza. Naomba wale wasioweza kwenda benki watumie namba hiyo,” amesema.


WANAWAKE WAONGOZA VIFO AJALI YA MV NYERERE

WAZIRI wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema hadi mazishi ya kitaifa yanafanyika, jumla ya watu 224 walikuwa wamepoteza maisha kutokana na ajali ya MV Nyerere iliyotokea Septemba 20, mwaka huu.

Akitoa taarifa ya tukio zima mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye ameongoza mazishi hayo Septemba 23, 2018, Waziri Kamwelwe amesema wanawake waliopoteza maisha jumla yao ni 126, wanaume 71, watoto wa kike ni 17 na wa kiume ni 10.

Awali, kabla ya ibada kuanza, idadi ya waliopoteza maisha ilikuwa 223 lakini mwili mmoja wa mwanamke ulipatikana mchana huu na kufanya idadi yao kufikia 224.

Amesema mipango ya Serikali ya muda mrefu ni kujenga kivuko kikubwa ambacho kitakuwa kikifanya safari zake kati ya bandari ndogo ya Bugolora iliyopo kisiwa cha Ukerewe na kisiwa kidogo cha Ukara.

“Tumefanya utafiti kwenye visiwa vidogo vyote na kubaini kuna mialo zaidi ya 140. Hii itaimarishwa ili iweze kufikika na vyombo vya usafiri ambavyo ni imara,” amesema.

Akitoa taarifa kuhusu tukio zima, Waziri Kamwelwe amesema ajali hiyo ilitokea Septemba 20, saa 7:48 mchana na taarifa zilifikishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza saa 8:10 mchana ambapo yeye na Kamati ya Ulinzi ya Usalama ya Mkoa walikimbia kuwahi eneo la tukio na kukuta watu watu 40 wameshaokolewa na wakazi wa kisiwa cha Ukara.

Amesema meli ya MV Nyerere ilijengwa mwaka 2004 na kufanyiwa ukarabati mkubwa mwaka 2013. “Julai mwaka huu, tulinunua injini mbili mpya na gear box zake,” amesema.

Mapema, akizungumza kwenye ibada hiyo ya mazishi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Bw. George Nyamaha aliiomba Mamlaka ya Usafirishaji Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) iongeze watumishi kwenye visiwa hivyo ili waweze kudhibiti matukio ya ujazaji abiria kwenye vyombo vya usafiri majini.

“Tunashukuru hapa Ukerewe tumeletewa mtendaji mmoja, lakini hawezi kufanya chochote kwa sababu hana hata chombo cha usafiri. Tuna visiwa 38 kwenye wilaya hii na kati ya hivyo, visiwa 34 kuna watu wanaishi ambao wanalazimika kusafiri ili kujipatia mahitaji yao. Sasa huyu mtendaji mmoja atafikaje kote huko?” alihoji.

Akifafanua adha ya usafiri kwenye visiwa hivyo alisema: “Ilugwa kuna watu zaidi ya 10,000 na huwa inachukua saa nne kutoka huko hadi kufika Nansio (makao maku ya wilaya ya Ukerewe). Watu wanatumia boti tu na ajali ni nyingi sana. Pia tunahitaji usafiri wa uhakika kutoka Kitale hadi Kweru ambako kuna wakazi zaidi ya 20,000” alisema.

Wakati huohuo, Mbunge wa Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi ambaye ni mzaliwa wa kisiwa cha Ukara, amesema wilaya ya Ukerewe inahitaji kupatiwa usafiri wa uhakika baina yake na visiwa jirani ili kuepuka maafa kama hayo yasitokee.

“Ukerewe tunahitaji chombo kizuri cha uhakika kinachoweza kustahimili maafa kama haya yasitokee. Ni kipindi kigumu kwetu wana Ukara, niombe tushikamane,” alisema.

No comments:

Post a Comment