WAZIRI Mkuu wa Jamhuri
ya Korea, Lee Nak-yon amemaliza ziara yake ya kiserikali ya siku tatu hapa
nchini na kusindikizwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu huyo wa
Korea ambaye ameondoka, Julai 23, 2018 saa 9.14 alasiri, ameelekea Oman ambako
atakuwa na ziara ya kikazi ya siku mbili. Aliwasili nchini juzi akitokea Kenya
ambako pia alikuwa na ziara ya siku mbili.
Katika uwanja wa ndege
wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Waziri Mkuu wa Korea Kusini alisindikizwa
pia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Augustine
Mahiga, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella
Manyanya na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam
Kabla ya kuondoka
alishuhudia burudani kutoka vikundi vya ngoma na matarumbeta uwanjani hapo. Mara
baada ya mgeni wake kuondoka, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizungumza na
wasanii waliokuwepo uwanjani na kuwapongeza kwa kujitokeza kutoa burudani kila
wakati wageni wanapoitembelea Tanzania.
“Tunawashukuru sana
wasanii kwa sababu mlikuja wakati wa mapokezi ya mgeni wetu na sasa mmekuja
tena kumsindikiza. Mgeni wetu amefurahia sana ngoma zetu na amesema atarudi
tena Tanzania.”
“Kwa niaba ya Ofisi ya
Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla, tunatambua kuwa mnajitoa muda wenu kila
mnapokuja kupokea na kusindikiza wageni ili kuweka sura nzuri ya Taifa letu
wakati wa kupokea wageni wetu, tunawashukuru sana,” amesema.
No comments:
Post a Comment