JUMLA
ya Sh12.4 bilioni zimeshatolewa na Benki ya NMB kwa zaidi ya wafanyabiashara
6,011 ambapo wanufaika wamepewa Elimu ya fedha na uongozi.
Takwimu
hizo zimetolewa na Meneja Mwandamizi idara ya Biashara za Serikali Amanda
Feruzi kwenye mkutano wa Jumuiya ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa Ukanda wa Ziwa
Victoria (LVRLAC) unaoendelea kwenye Ukumbi wa Jiji la Dodoma.
Fedha hizo ni kati ya Sh13 bilioni ambazo
Serikali ilizitoa kwa NMB kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa
vijana, Wanawake na wenye ulemavu katika mfumo wa majaribio kwa Halmashauri 6.
Halmashauri
zilizochaguliwa kwa mfumo wa majaribio ni Majiji ya Dar es Salaam na Dodoma,
Manispaa ya Songea, Halmashauri za Newala, Bumbuli na Itilima.
Feruzi
amesema NMB ipo tayari kufanya kazi na Jumuiya hiyo kama ambavyo imekuwa na
ushirikiano na kufadhiri mikutano yao kila mwaka.
Amesema
benki imekuwa na ushirikiano na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya
uwezeshaji wananchi kupitia fedha zinazotengwa kwa Makundi ya Vijana, Wanawake
na wenye ulemavu.
"Benki
ya NMB ina ujuzi na uzoefu katika APF kwani imeweza kutoa hati fungani zake na
Taasisi nyingine zenye thamani ya Trilioni Moja ikiwa benki ya kwanza Tanzania
na Afrika Mashariki kutoa hati fungani ya Jinsia (Jasiri Bond) na Uendelevu
(Jamii Bond),ambazo zimevutia wawekezaji wa ndani na nje katika masoko ya
mitaji ya Kimataifa," amesema Feruzi.
Kwa
mujibu wa maalumu hiyo, NMB ilikuwa benki ya kwanza kuunganishwa katika mfumo
wa GePG ambako kazi kubwa ilifanyika katika ukusanyaji wa mapato ambayo
ilitokana na Uwekezaji mkubwa katika Teknolojia, bidhaa na huduma mbalimbali
hata kuifanya kuwa mstari wa mbele katika kubuni masukuhisho kwa wateja na
Serikali.
Akizungumza
mkutano huo ambayo uliwakusanya wajumbe 42 kutoka mikoa ya Mara, Mwanza,
Shinyanga, Simiyu, Geita na Kagera, Feruzi amewataka kutumia fursa iliyotolewa
na Serikali ya kutafuta mitaji kutoka kwa wawekezaji ili kuzalisha vyanzo vipya
vya mapato.
"Benki
inaishauri Serikali kupanua wigo wa kutafuta fedha za kutekeleza miradi ya
kimkakati kwa kushirikiana na Sekta binafsi kupitia uwekezaji kwa njia ya PPP
na APF," amesema Feruzi.
Ametaja
baadhi ya manufaa yatakayopatikana kupitia uwekezaji huo ni kutatua na kusaidia
maboresho ya Miundombinu kwa haraka, kupunguza utegemezi kwenye bajeti Kuu,
kuruhusu utekelezaji wa miradi mara moja na kushirikiana na kutumia uzoefu wa
Sekta binafsi katika kutafuta mitaji.
Akizungumza
kwenye mkutano huo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi) Reuben Kwagilwa, amewataka Wakurugenzi kote nchini kufanya
kazi kwa mashirikiano na Sekta binafsi huku akisisitiza kuitumia benki ya NMB
katika masuluhisho ya kifedha.
Naibu
Waziri amesema maeneo mengi kumekuwa na kulegalega katika matumizi ya fedha
jambo alilosema Serikali haitamvumilia mtumishi atakayebainika.
Nanyi
Wakurugenzi niwaagize kwamba mlipe madeni ya Jumuiya kwa wakati ili kusudi
muweze kujiendesha na mnaweza kufanikiwa mkishirikiana na NMB katika Mipango
yenu," amesema Kwagilwa.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri amewataka Wakurugenzi kusikiliza kero za wananchi
na kuzitatua badala ya kusubiri viongozi wa juu kuja kuwasikiliza wananchi.




No comments:
Post a Comment