
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Katambi.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Katambi, amesema Jeshi la Magereza Tanzania linaweza kuwa la mfano Afrika na Dunia, kupitia kazi za kuwarekebisha Wafungwa na kazi mbalimbali za uzalishaji ambazo linazifanya.
Mhe. Katambi ameyasema hayo Januari 27, 2026 wakati akizungumza na Maafisa na Askari wa Magereza, alipotembelea Makao Makuu ya Magereza jijini Dodoma, kwa ajili ya kujitambulisha ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa na kuapishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Aidha Mhe. Katambi amesema ana tambua kazi kubwa inayo fanywa na Jeshi la Magereza, ikiwemo mapinduzi makubwa katika matumizi ya teknolojia, kilimo, ufugaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia magerezani pamoja na mchango mkubwa linaoutoa katika maendeleo ya Taifa.
"Ninampongeza Mkuu wetu wa Jeshi CGP. Katungu na jeshi zima kwaujumla, mnafanya kazi kubwa sana hasa katika maeneo ya urekebishaji, matumizi ya nishati safi ya kupikia, matumizi ya teknolojia katika kilimo, mifugo na matumizi ya CCTV pamoja na mashine za kisasa za upekuzi (walk through scanners) katika Magereza yetu," alisema Mhe. Katambi.
Katika hatua nyingine Mhe. Katambi amepongeza ujenzi wa Magereza mapya 12 katika Wilaya ambazo hazikuwa na Magereza nchini, huku akiahidi kuboresha maslahi ya watumishi na kutoa maagizo mbalimbali ikiwemo kuhakikisha maeneo ya Magereza yanapimwa na kupatiwa hati pamoja na kuongeza uzalishaji ili jeshi lijitosheleze kwa chakula.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, amelipongeza Jeshi la Magereza na kusema kuwa litumie fursa za uwekezaji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na kutumia teknolojia katika kilimo na ufugaji.
Nae Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania, CGP. Jeremiah Yoram Katungu, amemshukuru Mhe. Katambi kwa kufanya ziara ndani ya Jeshi la Magereza na kueleza kuwa jeshi linaendelea na shughuli zake za msingi za kutoa hifadhi salama kwa wafungwa, kuandaa na kutoa program za urekebishaji, huduma za mahabusu na kutoa ushauri kwa Serikali.
Aidha, CGP. Katungu amesema, jeshi linaendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ikiwemo, kuandaa mitaala mipya, matumizi ya maafisa ustawi katika vituo vya magereza, maboresho ya Sheria na Muundo wa Jeshi, matumizi ya nishati safi ya kupikia magerezani, matumizi ya teknolojia na Mahakama mtandao.
Pamoja na mambo mengine, CGP. Katungu ameeleza Mafanikio ya Jeshi la Magereza ikiwemo ushirikiano uliopo kati ya Magereza na Chuo cha Uhasibu Arusha pamoja VETA uliopelekea kuwapatia vyeti Wafungwa zaidi ya 400 ambao wamehitimu mafunzo mbalimbali wakiwa gerezani.
"Tumeingia makubaliano ya ushirikiano na wenzetu wa VETA na Chuo cha Uhasibu Arusha, ambapo kupitia ushirikiano huo Wafungwa zaidi ya 400 wamenufaika kwa kupata vyeti baada ya kuhitimu mafunzo wakiwa gerezani, lakini pia tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Magereza katika nyanja mbalimbali ikiwemo vyombo usafiri, zana bora za kilimo, mafunzo kwa watumishi, ajira mpya pamoja na upandishaji wa vyeo," alisema CGP. Katungu.
Akitoa neno la shukrani Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza CP. Nicodemus Tenga, amemshukuru Mhe. Katambi kwa kutembelea Magereza na kumuahidi kuwa, jeshi litaendeleza ushirikiano na wizara ili kusukuma mbele maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akisema kuwa maelekezo aliyoyatoa yatakuwa chachu zaidi katika utendaji wa Jeshi la Magereza.

No comments:
Post a Comment