MIZANI 78 ZAFUNGWA KUDHIBITI UZITO WA MAGARI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 27 August 2024

MIZANI 78 ZAFUNGWA KUDHIBITI UZITO WA MAGARI

Meneja wa Mazingira na Jamii wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Zafarani Madayi, akizungumza na waandishi wa waandishi wa habari kuhusu ushiriki wao kwenye wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani inayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Mzani wa kisasa wa Mikumi uliopo barabara kuu ya Morogoro – Iringa.

Moja kati ya gari la kusafirishia mizigi likipima uzito katika Mzani wa Mikumi uliopo katika Barabara ya Morogoro – Mikumi kabla ya kuendelea na safari.

SERIKALI imesema jumla ya mizani 78 zimefungwa nchini kwa ajili ya kudhibiti uzito wa magari ili kuzilinda barabara ambazo hugharimu fedha nyingi katika ujenzi wake.

Ameyasema hayo Agosti 27,2024 Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Mazingira Wizara ya Ujenzi Mhandisi, Kashinde Musa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wao kwenye wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani inayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Mhandisi Musa amesema kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara lakini moja kati ya changamoto zinazoharibu barabara ni suala la magari kubeba mizigo mizito zaidi ya uwezo wa barabara.

“Niwatake wadau wote wa usafirishaji nchini kuhakikisha wanafuata taratibu na kanuni za udhibiti wa mizigo barabarani ili barabara zetu ziweze kudumu kwa mujibu wa muda ule ambao umekusudiwa”amesema Mhandisi Musa

Ameongeza kuwa ili kupunguza ongezeko la ajali nchini wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2024/ 2025 imetenga bajeti kwa ajili ya kupunguza msongamano wa magari katika majiji matano.

Ametaja majiji hayo kuwa ni Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Dar es Saalam.

“Mradi huu utakapo kamilika tunatarajia utasaidia kupunguza ajali katika maeneo hayo lakini lengo letu ni kuhahakikisha mradi huu unakwenda nchi nzima,” amesema.

Hata hivyo amesema kuwa wizara imejikita katika matumizi ya teknolojia za kisasa kwa ajili ya kupunguza ajali katika maeneo mbalimbali ikiwemo ufungaji wa Kamera za usalama.


“Kuna mradi wa majaribu wa ufungaji wa kamera ambao tuliufanya katika mikoa ya Pwani na Morogoro mwaka 2016 ambapo tumebaini kuwa tangu wakati huo tulipofunga Kamera hizo ajali zimepungua kwa kiasi kikubwa sana hivyo lengo letu ni kufunga kamera hizo nchi nzima,” amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Mazingira na Jamii Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Zafarani Madayi, amesema kuwa kila mtu anao wajibu wa kutunza miundombinu ya barabara.


Amesema kuwa , wananchi wanapaswa kutunza miundombinu ya baraba na kuacha kufanya shughuli zozote za kibinadamu kwenye hifadhi ya barabara.

Aidha, amewataka wanachi kuacha kuchoma moto na majani kwenye barabara pamoja na kupitisha mifugo ili kuepusha kingo za barabara kumegeka. 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.


No comments:

Post a Comment