TANZANIA NA SHIRIKA LA MAENDELEO LA CHINA KUENDELEZA USHIRIKIANO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 12 July 2024

TANZANIA NA SHIRIKA LA MAENDELEO LA CHINA KUENDELEZA USHIRIKIANO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.) akiwa na Bw. Zhao Fengtao, Mmoja wa Wakurugenzi wa CIDCA, mara baada ya mazungumzo yao. Beijing China. Julai 11, 2024.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.) na Bw. Zhao Fengtao wakiwa Ujumbe wa Tanzania na Ujumbe wa CIDCA mara baada ya mazungumzo yao. Beijing China. Julai 11, 2024.

TANZANIA itaendelea kushirikiana kwa karibu na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la China (CIDCA) linalosimamia Misaada na Maendeleo ya Kimataifa kwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali nchini.

Hayo yamebainishwa kwenye mazungumzo baina ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila A. Mkumbo (Mb.), na Bw. Zhao Fengtao kwa niaba ya Uongozi wa CIDCA, pembezoni mwa Mkutano wa Pili wa Ngazi ya Juu wa Jukwaa la Hatua za Dunia kwa Maendeleo ya Pamoja (Global Action For Shared Development) unaoendelea Jijini Beijing. 

Kwenye mazungumzo yao yaliyoangazia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, Prof. Mkumbo aliishukuru Serikali ya China, kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa Tanzania katika kusukuma shughuli za maendeleo.

Hatujasahau, tunathamini mchango wa China wa ujenzi wa Reli ya TAZARA, pia, mmekuwa mkituunga mkono kwa kuimarisha sekta ya rasilimali watu, ni jambo muhimu kwetu, kwani asilimia 49 ya watu wetu ni vijana wanaohitaji ujuzi na maarifa” Alisema Prof. Mkumbo. 

Vile vile, Waziri wa Nchi, ametanabaisha kuwa, Nchi ya China ni mshirika muhimu katika kusukuma agenda ya kuhamasisha uchumi wa viwanda vya kuongeza thamani ili kuinua mauzo ya bidhaa nje ya nchi badala ya malighafi. 

“Mmeendelea kuwa washirika wetu muhimu katika kusukuma agenda ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kujenga uchumi wa viwanda, hadi sasa mmefanya uwekezaji wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 10 kwenye eneo la viwanda” Aliongeza Prof. Mkumbo. 

Kwa upande wake, Bw. Zhao Fengtao, amemhakikishia Mhe. Waziri kuwa CIDCA litaendelea kushirikiana kwa kuzingatia vipaumbele vya Tanzania, vikiwemo vya sekta za kilimo, viwanda, madini na kuinua rasilimali watu.

Bw. Fengtao amesisitiza kuhusu kuimarisha ushirikiano baina Tanzania na CIDCA kwa kufanya kazi kwa karibu ikiwa ni pamoja na kubadilishana utaalamu kupitia miradi ya kuinua ujuzi na maarifa, kuimarisha mawasiliano ili kufanikisha malengo ya pamoja, na kufanya tathimini ya pamoja ya miradi ya maendelo inayotekelezwa kwa ushirikiano.   

Mheshimiwa Prof. Mkumbo yupo Beijing China, ambako anashiriki Mkutano wa Pili wa Ngazi ya Juu wa Jukwaa la Hatua za Dunia kwa Maendeleo ya Pamoja (Global Action For Shared Development). 

No comments:

Post a Comment