Muonekanao wa daraja jipya la Ruaha Mkuu mkoani Morogoro lenye urefu wa mita 133 ambalo kwa sasa ujenzi wake umefika asilimia 88. Kazi zilizobaki ni kujenga njia za maingilio katka daraja hilo.
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha wanajenga mageti ya kisasa kwenye maeneo ambapo barabara inakutana na reli ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika katika maeneo hayo.
Kasekenya, ametoa agizo hilo Mei 26, 2024 wakati akikagua mradi wa ujenzi wa barabaara ya Mikumi - Kidatu- Ifakara sehemu ya Kidatu - Ifakara (Km 66.9) kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa Daraja la Ruaha Mkuu na kusisitiza TANROADS kuwasiliana na TAZARA ili kulifanyia kazi suala hilo mara moja.
"Kuna haja kubwa ya kujenga mageti ya kisasa sehemu ambapo barabara inakatisha reli kwani maeneo mengine tayari wameanza kufanya hivyo, hii itasaidia kufunga njia au kuwasha taa endapo treni inapokuja na hivyo kutosababisha ajali", amesema Kasekenya.
Aidha, Mhandisi Kasekenya pia amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, kuhakikisha anamsimamia Mkandarasi Reynolds kutoka Nigeria aneyejenga mradi huo kuimarisha mifereji ya upande wa juu na chini ili kuzuia maji kutokwenda kwenye makazi ya watu na kusababisha madhara.
Kadhalika, Kasekenya ameeleza kuwa kuna haja ya TANROADS kufanya usanifu wa madaraja katika barabara ya Kidatu - Mikumi kwani yaliyopo ni madogo na membamba ili kusaidaia magari yanapokuja kutoka Mikumi kwenda Kidatu kupita bila kikwazo chochote.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amesema kuwa ujenzi wa mradi huo unaendelea vizuri na mkandarasi anatarajia kukamilisha ujenzi huo ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Ameeleza kuwa mradi huo ulikuwa na madaraja manne pamoja na daraja moja kubwa la Ruaha Mkuu ambapo ujenzi wa daraja hilo kwa sasa umefikia asilimia 88 na kwa sasa kazi iliyobaki ni kumaliza kujenga njia za maingilio.
Kuhusu ujenzi wa barabara hiyo, Mhandisi Kyamba amesema kuwa umefika asilimia 90 ambapo lami imejengwa kilometa 63 kati ya 66 na kilometa Tatu zilizobaki zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Naye, Mhandisi wa Barabara, kutoka Kampuni ya Kikandarasi ya Reynolds kutoka Nigeria, Thobias Ngise amesema kuwa mradi wote kwa sasa umefika asilimia 95 na kusisitiza kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha asilimia Tano zilizobaki kwa muda uliopangwa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.
No comments:
Post a Comment