TMA NA DONDOO MUHIMU ZA HALI YA HEWA KUANZIA JUNI-AGOSTI, 2024 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 27 May 2024

TMA NA DONDOO MUHIMU ZA HALI YA HEWA KUANZIA JUNI-AGOSTI, 2024

 Dondoo muhimu za hali ya hewa kipindi cha Juni-Agosti (JJA), 2024

TAARIFA hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa hali ya joto, upepo na mvua katika msimu wa Juni hadi Agosti (JJA), 2024; Ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao. Kwa kawaida, kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti (JJA), hutawaliwa na hali ya baridi na upepo mkali kwa maeneo mengi ya nchi. Kwa muhtasari, mwelekeo wa msimu wa JJA, 2024 unaonesha kuwa: 


a) Mwelekeo wa hali ya joto 

i. Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kusini-magharibi na yale ya kusini mwa nchi.


ii. Vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza mwezi Julai.


b) Mwelekeo wa hali ya upepo

i. Msimu wa Kipupwe 2024 unatarajiwa kutawaliwa na upepo wa wastani hadi upepo mkali utakaovuma kutoka kusini-mashariki katika maeneo mengi na vipindi vichache vya upepo wa kusi katika ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.

c) Mwelekeo wa mvua

i. Vipindi vya mvua vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani, nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

d) Athari  

i. Magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza, ingawa kwa kiasi kidogo.


ii. Hali ya vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya macho. 


1.0 MATARAJIO YA VIWANGO VYA JOTO KWA MIEZI YA JUNI HADI AGOSTI, 2024

Katika kipindi cha msimu wa Kipupwe (JJA), 2024 hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kusini-magharibi, kusini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na kanda ya kusini. Aidha, vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai. 

1.1 Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu):

Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi. Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 oC na 20 oC.

1.2 Ukanda wa pwani ya kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba):

Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi. Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 23oC na 26oC kwa maeneo ya mwambao wa pwani na visiwani, na kati ya nyuzi joto 17oC na 23oC katika maeneo ya nchi kavu. Hata hivyo, maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 17oC. 

1.3 Nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):

Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi. Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 oC na 20 oC. Hata hivyo, maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 15 oC. 

1.4 Kanda ya magharibi (Mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma):

Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 oC na 20 oC. Hata hivyo, maeneno ya kusini mwa mkoa wa Katavi yanatarajiwa kuwa na hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali chini ya nyuzi joto 15oC.

1.5 Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):

Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 11oC na 17oC.

1.6 Ukanda wa pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi):

Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 17 oC na 22 oC.

1.7 Kanda ya kusini (Mkoa wa Ruvuma):

Hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10oC na 18 oC.

1.8 Nyanda za juu kusini-magharibi (Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro):

Hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 7 oC na 15 oC. Hata hivyo, katika maeneo yenye miinuko, kiwango hicho kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 7 oC. 

Kielelezo 1: Mwelekeo wa viwango vya joto la chini katika msimu wa JJA, 2024. Kielelezo 2: Wastani wa muda mrefu (1991-2020) wa viwango vya joto la chini kwa msimu wa Juni hadi Agosti.

2.0 MWENENDO WA UPEPO KWA KIPINDI CHA JUNI HADI AGOSTI (JJA), 2024

Kwa kawaida msimu wa Kipupwe hutawaliwa na upepo wa kusi. Hata hivyo, msimu wa JJA, 2024 unatarajiwa kuwa na upepo wa wastani hadi upepo mkali utakaovuma kutoka kusini-mashariki na vipindi vichache vya upepo wa kusi katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu. Kwa ujumla, upepo wa wastani unatarajiwa kushamiri katika maeneo mengine ya nchi.


3.0 MWELEKEO WA MVUA KWA KIPINDI CHA JUNI HADI AGOSTI, 2024

Kwa kawaida kipindi cha msimu wa Kipupwe (JJA) kinatawaliwa na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, vipindi vichache vya mvua vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria (mikoa ya Kagera, Geita, Simiyu na Mara), kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, nyanda za juu kaskazini-mashariki (mikoa ya Arusha na Kilimanjaro) pamoja na ukanda wa pwani (mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).

4.0 MIFUMO YA HALI YA HEWA

Katika kipindi cha msimu wa Kipupwe (JJA), 2024, hali ya joto la bahari katika ukanda wa tropiki ya kati ya bahari ya Pasifiki inatarajiwa kuwa ya wastani hadi chini ya wastani, ikiashiria kuelekea hali ya La Niña hasa mwisho wa msimu. Hali hii inatarajiwa kuwa na mchango hafifu katika mifumo ya mvua hapa nchini.

Kwa upande wa Bahari ya Hindi, joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa kuendelea kuwepo katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Afrika Mashariki) ikilinganishwa na joto la Bahari upande wa mashariki mwa Bahari ya Hindi (Pwani ya Indonesia). Hali hii inatarajiwa kuimarisha mifumo inayosababisha mvua katika maeneo ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo jirani.

Aidha, upepo unatarajiwa kuvuma kutoka misitu ya Kongo kuelekea nchini, hali hii inatarajiwa kuimarisha mifumo inayosababisha mvua hasa katika maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na ukanda wa Ziwa Viktoria. Na kwa upande mwingine, mifumo ya mgandamizo mkubwa wa hewa iliyopo katika kizio cha kusini mwa Afrika (Mascarene High) inatarajiwa kuimarika na kupelekea vipindi vya upepo mkali wa kusi.

5.0 ATHARI NA USHAURI 

Kutokana na mwelekeo wa msimu wa Kipupwe kama ulivyoainishwa kwenye taarifa hii, zifuatazo ni athari na ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali:

5.1 Athari

Katika msimu huu, magonjwa yanayohusiana na hali ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza, ingawa kwa kiasi kidogo. Pia, vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya macho na magonjwa mengine yanayohusiana na hali hiyo. 

5.2 Ushauri

Tahadhari za kiafya zichukuliwe ili kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi na vumbi. Kutokana na hali ya ukavu inayotarajiwa katika maeneo mengi katika kipindi hiki, maji na malisho yanapaswa kutumika kwa uangalifu ili kupunguza athari zinazotarajiwa. Aidha, wakulima wanashauriwa kulima mbogamboga na mazao ya mizizi kama vile viazi katika maeneo oevu na pia katika maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua katika kipindi hiki cha msimu wa Kipupwe. Hata hivyo, sekta za ujenzi, madini na uchukuzi zinaweza kunufaika kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa.

Angalizo:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) itaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejesho. Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia na kuzingatia utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Imetolewa: 27 Mei, 2024

Na: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

No comments:

Post a Comment