MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari ametoa rai kwa wataalamu kutoka nchi za Kanda ya Afrika Mashariki kuboresha ushirikiano ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza hususani kipindi cha matukio ya hali mbaya ya hewa.
Mhe. Mshibe alisema hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Kamati ya Usimamizi wa Programu ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ya Utabiri wa Hali Mbaya ya Hewa kwa nchi Wanachama Kanda ya Afrika Mashariki, unaofanyika Dar es Salaam, 14-17 Mei, 2024.
Aidha, alisisitiza kuwa, mkutano huo umewaleta pamoja wataalamu kutoka nchi za Tanzania, Burundi, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan, Uganda, Djibouti, Somalia, Eritrea, Sudan Kusini pamoja na Wataalamu wengine kutoka vituo mbalimbali vya Kikanda vya WMO, hivyo kupitia ushirikiano huo huduma za hali ya hewa kwa nchi wanachama wa WMO Kanda ya Afrika Mashariki zinatarajiwa kuboresha huduma zake za hali ya hewa ili kupunguza athari zitokanazo na matukio ya hali mbaya ya hewa.
Akimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Kaimu Mkurugenzi wa TMA ofisi ya Zanzibar, Bw. Masoud Faki alisema kupitia programu hiyo ya Utabiri wa Hali Mbaya ya Hewa, TMA imeweza kunufaika na masuala mbalimali yakiwemo ya mafunzo kwa wataalamu na miongozo ya pamoja ya utendaji kazi ambayo imesaidia katika maandalizi ya utabiri katika ngazi ya nchi.
Bw. Masoud aliendelea kueleza kuwa mwaka 2019 Tanzania kupitia TMA ilichaguliwa na WMO kuendesha Kituo cha Kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri wa hali mbaya ya hewa kwa nchi zilizopo katika Ukanda wa Ziwa Victoria ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Katika hatua nyingine, mwakilishi kutoka sekretarieti ya WMO aliishukuru Serikali ya Tanzania kukubali kuandaa na kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu wenye lengo la kuboresha huduma za taarifa za hali mbaya ya hewa kwa nchi wanachama wa Kanda ya Mashariki, lengo ambalo linaenda sambamba na jitihada za Umoja wa Kimataifa.
No comments:
Post a Comment