![]() |
Muonekano wa sehemu ya
barabara ya Lindi - Dar es Salaam, eneo la Nanguruku ambalo limekatika kutokana
na Mvua kubwa zilizonyesha zikiambatana na Kimbunga Hidaya, Mkoani Lindi. |
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewatoa hofu na kuwahakikishia wananchi, wasafiri na wasafirishaji kuwa ameweka kambi Mkoa wa Lindi kuhakikisha anasimamia timu ya watalaamu wa Wakala ya Barabara (TANROADS) na makandarasi, kuhakikisha wanakamilisha kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara ya Lindi – Dar es Salaam ndani ya saa 72.
Waziri Bashungwa
ameeleza hayo, leo tarehe 6 Mei 2024 Nangurukuru Wilayani Kilwa wakati akikagua
na kusimamia zoezi la urejeshaji wa mawasiliano ya barabara yaliyokatika kwa
kuharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha zikiambatana na kimbunga Hidaya.
“Niendelee kuwatoa hofu
wananchi na wasafiri wanaotumia barabara hii inayounganisha mikoa ya kusini,
tangu jana nimepiga kambi huku, nilianzia Somanga na sasa hivi tupo upande huu
wa Nangurukuru, kama mnavyoona pande zote wanaendelea na kazi, bado tunaamini
ndani ya saa 72, kufikia Alhamisi tutakuwa tumekamilisha kazi ya kurudisha
mawasiliano ya barabara hii,” amesema Bashungwa.
Bashungwa amemuagiza
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta kuhakikisha anaongeza idadi ya
malori yanayosomba mawe pamoja na mitambo inayotumika kupakia mawe katika
magari ili kuongeza kasi ya kujaza vifusi katika eneo la barabara yaliyosombwa
na maji.
Aidha, Bashungwa
amesema kuwa pamoja na jitihada za kuagiza makalvati ya plastiki yanayotumika
katika dharura za kurejesha mawasiliano ya barabara, ameeleza kuwa ili
kukamilisha kazi hiyo kwa wakati watalazimika kutumia makontena kwa kuyakata
yatumike kama mbadala wa kalvati na kuwezesha maji kupita.
Kadhalika, Bashungwa
amewapongeza wahandisi kutoka TANROADS pamoja na makandarasi wote wanaoendelea
na kazi ya kuhakikisha mawasiliano ya barabara katika maeneo yote yaliyokatika
yanarejea.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya
Kilwa, Mohamed Nyundo amemshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuiwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa kuwa na vifaa vya kisasa vinavyotumika
kutabiri hali ya hewa ambapo vimesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa utabiri wa
matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafuriko makubwa na kimbunga Hidaya.
Kwa upande wake, Diwani
wa Kata ya Kivinje Singino, Jafari Bakari ameipongeza Serikali kwa kuchukua
hatua za haraka na dharura kwa kufanyia kazi changamoto zinazojitokeza ikiwa ni
pamoja na kuhamisha wananchi wanaokaa katika maeneo hatarishi.





No comments:
Post a Comment